Tuesday, August 18, 2015

Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma Inaendelea

Siku chache zilizopia niliandika katika blogu hii kuhusu warsha tuliyokuwa tunaisibiri hapa chuoni St. Olaf juu ya jamii na taaluma. Warsha hiyo ilianza jana; tulijadili sura kadhaa za kitabu cha Martha C. Nussbaum, Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities.

Kitabu hiki kinaelezea namna mwelekeo wa elimu ya juu unavyochepuka kutoka katika hali yake ya asili na unavyoingia katika mkondo wa kibiashara. Malengo ya elimu, ambayo yanapaswa kuwa kumjenga mtu na jamii katika tabia ya kutafakari, kuhoji mambo, kujitambua, na kuwa na mahusiano mema, ya ushirikiano na kusaidiana, yamekuwa yakibadilika. Malengo hayo sasa ni kuwaandaa watu kwa ajira na uzalishaji wa mali.

Not for Profit kinaongelea umuhimu wa elimu katika demokrasia. Kwa kuiingiza elimu katika mfumo wa biashara, tunahujumu demokrasia na mahusiano bora ulimwenguni. Nilifurahi kusoma katika kitabu hiki nadharia za mabingwa niliowasoma nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Socrates, Jean Jacques Rousseau, Johann Pestalozzi, na John Dewey. Ningefurahi zaidi iwapo nadharia za Paulo Freire zingekuwemo pia, kwani huyu ni mwelimishaji maarufu aliyeonyesha njia ya kuifanya elimu kuwa nyenzo ya mapinduzi.

Nilifunguka akili niliposoma kuwa Rabindranath Tagore alikuwa mwelimishaji, sio tu kinadharia, bali kwa kuanzisha na kuendesha vyuo. Tangu zamani nilimfahamu Tagore kama mwandishi maarufu wa riwaya, tamthilia na mashairi, aliyepata tuzo ya Nobel mwaka 1913. Niliwahi kufundisha kitabu chake maarufu, Gitanjali, hapa chuoni St. Olaf. Lakini sikuwa nimefuatilia mchango wake ulivyoelezwa katika Not for Profit.

Leo tumejadili sura kadhaa za kitabu cha Stanley Fish, Versions of Academic Freedom: From Professionalism to Revolution. Fish anafafanua vizuri dhana ya uhuru wa taaluma, kwa kuangalia mitazamo mbali mbali iliyopo kuhusu dhana hiyo. Ameweka wazi masuali muhimu kuhusu dhana ya uhuru wa taaluma. Kwa mfano, uhuru wa taaluma ni haki ya kikatiba? Kwa nini waalimu katika elimu ya juu wanaamini wana haki ya kuwa na uhuru wa taaluma mpana kuliko uhuru walio nao wananchi wengine? Wanafunzi nao wanao au wanastahili uhuru huo?

Fish anaongelea pia masuala ya mtazamo wa kisiasa wa waalimu katika vyuo vikuu, na uhusiano wa maadili na uhuru wa taaluma. Tulipokuwa tunajadili suala hilo la maadili, profesa mwenzetu mmoja alielezea alivyowahi kukataa kuchora michoro ya kuboresha muundo wa ndege za kivita za jeshi la Marekani.

Kama ilivyokuwa jana, mjadala wa leo ulikuwa mzuri na wa kuelimisha. Nimefurahi kuvisoma vitabu viwili nilivyovitaja hapo juu. Kesho tutajadili Professors and their Politics, kitabu kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons.

No comments: