Tuesday, August 25, 2015

Nimekikuta Kitabu Changu Kinameremeta Dukani

Mchana huu nimemaliza kusahihisha mtihani wa kumalizia muhula wa somo langu la "African Literature." Nimekwenda chuoni kuwarudishia wanafunzi daftari zao, nikiwa na furaha ya kuwa na wiki mbili tatu za "uhuru," kabla ya kuanza muhula mwingine.

Baada ya kurudisha daftari, niliingia katika duka la vitabu. Nilizunguka kidogo tu humo ndani nikaona kitabu changu cha Matengo Folktales kimewekwa mahali pa wazi, pamoja na vitabu vingine vichache. Kinaonekana pichani chenye rangi ya manjano na ramani ya Afrika.

Huu ni utaratibu wa duka letu la vitabu. Kila wakati wanachagua vitabu vichache na kuviweka sehemu hizo za wazi ili viweze kuonekana kirahisi kwa wateja. Kufuatana na utaratibu uliopo, kitabu kitakuwa hapo kwa siku kadhaa, na hata wiki kadhaa, kabla ya kurudishwa sehemu yake.

Katika duka hili la chuoni St. Olaf vinapatkana vitabu vyangu vyote. Mbali ya wanafunzi, waalimu, na wafanyakazi wengine wa chuo, wageni wanaokitembelea chuo hupenda kuingia katika hili duka la vitabu, ambalo huuza pia bidhaa mbali mbali, kama ilivyo kawaida katika maduka ya vitabu ya vyuo vya Marekani.

Kila ninapoviona vitabu vyangu katika duka hili, mawazo hunijia, hasa kuhusu namna vitabu hivi vinavyowafaidia wa-Marekani. Vinawafaidia kielimu, kwa kuwa vinatumika katika masomo. Vinawafaidia kibiashara, kwa kuviuza, na vinachangia ajira hata kama ni kiasi kidogo sana, kwa wachapishaji, wasafirishaji, na wahudumu wa duka kama hili la Chuo cha St. Olaf. Nawazia mambo ya aina hii.

4 comments:

NN Mhango said...

Hakuna furaha kama hii kwa mwandishi kukuta kazi yake kwenye sehemu ambapo umma unaweza kuiona tena ikiwa kwenye hali nzuri kama ulivyokuta kitabu chako. Najua unavyojihisi na kiasi cha furaha uliyo nayo.

Mbele said...

Ndugu Mhango\

Shukrani kwa ujumbe. Ninategemea kuwa haya tunayofanya katika uandishi yanachangia kuwapa moyo vijana na waandishi chipukizi, kwamba kwa jitihada ya dhati isiyo na kikomo, chochote kinawezekana. Hilo moja. La pili ambalo ningependa vijana na waandishi chipukizi walizingatie ni kuwa mafanikio si sababu ya kupunguza juhudi, bali ni kichocheo cha kufanya makubwa zaidi. Mafanikio ya kweli katika uandishi ni kujieleza vizuri iwezekanavyo na kuwagusa wasomaji vilivyo.

Alex said...

Hongera sana Prof. Mbele, huwa nasoma na kurudia kitabu chako, "Africans and Americans Embracing Cultural Differences" najiona kama nipo marekani.

Mbele said...

Ndugu Alex,

Shukrani kwa ujumbe wako. Nakumbuka tulivyokutana Sinza, ulipokifuata hicho kitabu. Nakumbuka simulizi yako katika blogu ya BongoCelebrity.

Nimekuwa na bahati ya kuwa na wasomaji wengi wa aina yako, ambao kweli mnasoma maandishi yangu, nami natambua wajibu wa kuwarudishia heshima kwa kujitahidi kuandika kwa ubora zaidi.

Hapa nilipo, nakaribia kumaliza uandishi wa kitabu cha kuendeleza yaliyomo katika hicho kitabu unachosoma. Insha Allah, nitamaliza uandishi na kuchapisha mwaka huu. Sitawaangusha nyinyi wasomaji wangu. Mtakipenda. Tuombe tu uzima.