Thursday, August 20, 2015

Tumemaliza Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma

Leo, hapa chuoni St. Olaf, tumemaliza warsha yetu kuhusu jamii na taaluma. Nimeshaandika kuhusu warsha hii katika blogu hii. Tumehitimisha warsha kwa kujadili kitabu cha George Yancey, Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education. Lakini, kabla ya kuongelea mjadala wa leo, napenda kwanza kugusia mjadala wa jana.

Jana tulijadili sura za 1, 5, na 8 za Professors and Their Politics, kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons. Insha zilizomo katika kitabu hiki zinabainisha vizuri aina mbali mbali za mitzamo ya kisiasa inayoongoza fikra, utafiti, uongozi, na mambo mengine katika vyuo vikuu vya Marekani. Kitabu hiki kinajadili soshiolojia ya wanataaluma, kwa kuchambua mahusiano miongoni mwao na siasa zinazoendesha vyuo. Kinatoa mwanga juu ya mahusiano baina ya wanataaluma na jamii kwa ujumla, ikiwemo ushiriki wa waalimu na wahitimu katika masuala ya siasa za Marekani.

Tulisoma pia maandishi mengine ambayo hayamo katika kitabu hiki, tukayajumlisha katika mjadala. Andiko mojawapo ni "The Coddling of the American Mind." Mjadala ulikuwa wa kufikirisha na kuelimisha, sawa na mijadala ya siku mbili zilizotangulia.

Leo, tulijadili sura ya 2, 5, na 8 za Compromising Scholarship. Kwa kiasi fulani, mambo yaliyojitokeza leo ni mwendelezo wa yale tuliyoyajadili jana, ingawa kitabu hiki kinakwenda mbali katika kutufanya tujitambue kwamba tunapoangalia suala lolote, tunaliangalia kwa kutumia misingi, mitazamo, au kasumba tulizo nazo vichwani. Kwa mtu ambaye anafahamu angalau kiasi falsafa ya watu akina Immanuel Kant, au nadharia za kisasa za fasihi, msisitizo kwamba sisi sote tuna misingi hiyo vichwani mwetu, kitabu hiki si kigumu kukielewa.

Mjadala wa leo ulionekana kuamsha hisia za ndani na hamasa miongoni mwa wengi wetu. Labda ni kwa sababu ya aina ya masuala tuliyokuwa tunazungumzia, au labda ni kwa sababu tumezoeana baada ya siku tatu za kukaa pamoja na kujadili masuala, mjadala wa leo haukuwa wa kawaida. Ingekuwa warsha inaendelea kesho na keshokutwa, kwa mfano, joto la mjadala lingezidi kupanda.

Nimejifunza mengi katika warsha hii. Kama nilivyosema awali katika blogu hii, nafurahi kujipatia vitabu muhimu bila gharama, ambavyo nitavisoma kwa wakati wangu. Elimu ya bure namna hii, na vitabu muhimu, ni marupurupu adhimu ya ualimu.

No comments: