
Jana ilikuwa siku tuliyoingojea kwa hamu kubwa. Ilikuwa ni siku ya kuonyeshwa filamu ya "Papa's Shadow" hadharani, ingawa wote walikuwa waalikwa. Kwa kuwa mimi ni mhusika mkuu katika filamu hiyo kama mzungumzaji sambamba na Mzee Patrick Hemingway, uwepo wangu ulikuwa muhimu.
Nilijikuta niko miongoni mwa kadamnasi iliyoniona maarufu. Nina hakika kuwa huu utakuwa mzigo maishani, kwani nitategemewa kujua mengi juu ya Hemingway kuliko inavyowezekana. Hiyo jana tu masuali magumu yalikuwa yanaelekezwa kwangu. Hata hivi, hii ni changamoto nzuri ya mimi kuendelea kujielimisha.
Baada ya filamu kuonyeshwa, watu walikuja na kunishukuru sana kwa mengi niliyosema juu ya Hemingway. Mtu mmoja, kwa mfano, aliyejitambulisha kwangu kama mwalimu wa "high school," alinionyesha daftari ambamo alikuwa ameandika mambo yaliyomgusa zaidi katika filamu, na alisema kuwa amepata hamasa ya kuanza kusoma tena maandishi ya Hemingway.
Hapa kushoto niko na binti yangu wa kwanza, Deta, ambaye hajawa na fursa nyingi za kushuhudia shughuli zangu. Hii ni kutokana na majukumu ya kazi, sawa na mama yake. Lakini jana ilikuwa fursa nzuri, na sote tulifurahi.
Hapa kushoto niko na binti yangu wa pili, Assumpta. Huyu ndiye aliyeanzisha utani kuwa baada ya filamu hii ya "Papa's Shadow," nijiandae kutua Hollywood.
Hapa kushoto tuko na Jimmy Gildea, mtengeneza filamu. Alikuwa mmoja wa wanafunzi 29 waliokuja Tanzania kwenye kozi yangu ya "Hemingway in East Africa," Januari, 2013.
Nimefanikiwa katika mambo mengi maishani, hasa katika masomo, na yote yameniletea furaha. Lakini nimefurahi zaidi kwa uzinduzi wa filamu hii na kwa jinsi nilivyowashirikisha watoto wangu. Waliyojionea na kuyasikia hiyo jana watayakumbuka.
No comments:
Post a Comment