Sunday, June 28, 2015

Tamasha la Vitabu Mankato Limefana

Leo, nikiwa na binti yangu Zawadi, tulikwenda Mankato kushiriki tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival. Niliandika habari za tamasha hilo katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Nilipeleka vitabu vyangu vinavyoonekana mtandaoni, pamoja kijitabu kiitwacho Africans in the World. Vile vile tulipeleka "t-shirt" kama hizo tulizovaa pichani, zenye nembo ya kampuni yangu ndogo Africonexion: Cultural Consultants. Tunajifunza mengi katika kukutana na watu wanaofika kwenye meza yetu. Hatujui nini kitamvutia mtu fulani na kwa nini. Lakini watu hujieleza. Tunasikia habari nyingi, nyingine za kushangaza, zinazomfanya mtu anunue hiki au kile.

Inatufurahisha kuwaangalia watu wakipita kwenye meza mbali mbali kuangalia vitabu, kuongea na waandishi, wachapishaji na wengine wanaokutana nao katika tamasha. Nasi tunapata fursa ya kukutana na watu mbali mbali. Leo, kwa mfano, wamefika watu kwenye meza yetu ambao wametuambia wamefika Afrika: Botswana, Tanzania, na Namibia. Tunahisi walivutiwa na "t-shirt" tulizovaa, zenye ya ramani ya Afrika. Kila mmoja ametusimulia habari za safari yake. Tulijua kuwa tutakutana na baadhi ya watu tuliokutana nao wakati nilipotoa mihadhara katika Chuo cha South Central, katika maandalizi ya safari ya Afrika Kusini. Kama tulivyotarajia, walikuwepo watu kadhaa.Hapa kushoto anaonekana kiongozi wa safari ya Afrika Kusini, mwalimu Becky Fjelland Davis, ambaye ni mwandishi. Alishiriki tamasha. Mwingine ni Paul Dobratz ambaye alihudhuria shughuli zote nilizofanya wakati wa ziara yangu Chuoni South Central. Naye alikuwemo katika safari ya Afrika Kusini. Binti yangu nami tulifurahi sana kusikia habari za safari.
Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, watu wa rika mbali mbali huhudhuria matamasha haya ya vitabu. Wanayathamini sana, na mahudhurio huwa makubwa.

Daima ninaguswa ninapowaona wazazi wakiwa na watoto wao. Ninaguswa na jinsi wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.


Imekuwa siku ya furaha sana kwa binti yangu na mimi. Tumefurahi kukutana na kuongea na watu wa aina aina, tuliowafahamu na ambao hatukuwafahamu. Tumerudi na kumbukumbu nyingi.

No comments: