Monday, June 8, 2015

Mhadhiri wa Algeria Amefurahi Kupata Kitabu

Jana, niliporejea kutoka kanisani, nilikuta ujumbe katika ukurasa wangu wa Facebook kutoka kwa Samir Zine Arab, mhadhiri wa "African Literature and Listening Skills" katika chuo kikuu cha Hassiba Ben Bouali Chlef, Algeria. Alikuwa anashukuru kupata nakala ya kijitabu changu, Notes on Achebe's Things Fall Apart ambayo nilimtumia siku kadhaa zilizopita.

Ujumbe wake, ulioambatana na picha inayoonyesha kitabu pamoja na bahasha niliyotumia, kama inavyoonekana hapa kushoto, ameusambaza kwa marafiki zake wa Facebook ambao mimi ni mmoja wao. Amenigusa kwa namna alivyoandika:

Dear friends, brothers and sisters! Today I'm the happiest man on earth! This morning I received a lovely book from a great professor Joseph Mbele! Thank you so much dear!!

Pamoja na ujumbe huu, Mwalimu Samir ameniandikia pia ujumbe binafsi ambao nao umenigusa sana. Kwake na kwangu imekuwa ni furaha. Ninavutiwa na watu wa aina ya huyu mwalimu, ambao wana duku duku ya kutafuta elimu. Aliposikia tu kuhusu kijitabu changu, alikitaka.

Ninafurahi kuwa wanafunzi Algeria watapata fursa ya kuyafamu na kuyatafakari mawazo niliyoandika katika kijitabu hiki, ambacho Mwalimu Samir alikitamani tangu nilipokitaja katika Facebook, tarehe 11 Mei. Taarifa zaidi za kijitabu hiki niliandika katika blogu hii. Tangu nilipoandika taarifa hiyo, kuna kitu cha ziada ambacho nimefanya. Nimechapisha kijitabu hiki kama kitabu pepe, yaani "ebook."

No comments: