Sunday, June 7, 2015

Nimetoka Kanisani Kusali

Ni Jumapili, saa sita na kidogo mchana. Nimetoka kanisani kusali. Mimi ni m-Kristu wa kawaida, m-Katoliki. Namwabudu Mungu na ninaamini kuwa yeye ndiye anayeongoza maisha yangu. Katika raha na matatizo, ninamtegemea yeye. Ninamshukuru kwa kunipa uhai siku hadi siku.

Namshukuru Mungu kwa kunipa akili na utashi nitafakari mambo na kujiamulia. Ninamshukuru kwa jinsi anavyotuneemesha, kwa kuwaumba wanadamu wa kila aina, wenye dini mbali mbali, tamaduni na lugha mbali mbali. Dunia inapendeza kwa tofauti hizo, sawa na maua yanavyopendeza, kwa uwingi wa tofauti za rangi.

Namshukuru Mungu kwa yote aliyoyaweka duniani: nchi kavu, bahari, milima, mabonde, mito, miti, majani na maua. Ametuwekea wanyama wa kila aina, ndege na wadudu, jua, mwezi na nyota, mvua na upepo, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana.

Vyote ni mazao ya uumbaji wa Mungu. Ninaomba niwe na moyo wa kuwapenda wanadamu wote na vyote alivyoumba Mungu. Ninaomba niwe mtu mwema, mwenye kutambua na kuzingatia kila siku kuwa Mungu amenipa uhai, akili, na vipaji, si kwa ajili yangu, bali kwa manufaa ya walimwengu bila kujali tofauti zao, za taifa, kabila, dini, jinsia, umri, utamaduni, lugha, na kadhalika.

Kuwa kanisani, kujumuika na waumini wenzangu, ni fursa ya kujikumbusha imani ya dini yangu, kuwaombea walimwengu wote, wabarikiwe. Sasa, baada ya kutoka kanisani, ninajisikia mwenye faraja, moyo mkunjufu, na ari ya kuendelea na majukumu yangu.

2 comments:

Anonymous said...

Ahsante Mungu akubariki

Mbele said...

Ndugu Anonymous uliyeandika December 15, 2015 at 10:26 AM, shukrani kwa ujumbe wako. Kama unavyoona, hayo mawazo niliyoandika yanapishana kwa kiasi kikubwa na Imani za waumini wengi wa dini, ambao, badala ya kujitahidi kuona sura ya Mungu katika wanadamu wote, wana tabia ya kujiona wao ni bora kuliko wengine, tabia ya kubaguana kwa misingi mbali mbali, kama vile taifa, kabila, rangi, dini, na jinsia.

Ninaamini kwamba huo mtazamo nilioelezea hauendani na mtazamo wa wengi. Ni mtazamo ambao nimekuja kuuona umeelezwa vizuri zaidi katika waraka wa Papa Francis, "Laudato Si," na sala yake iliyomo katika waraka huu, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Narudia kukushukuru, nawe Mungu akubariki.