Wednesday, June 3, 2015

Nadharia ya Uandishi

Uandishi ni nini? Je, kila uandishi ni uandishi wa kweli? Uandishi wa kweli ni nini? Naona haya ni masuali ya msingi. Ningependa tuyatafakari. Waandishi wengi maarufu wameandika kuhusu masuala hayo. Katika kitabu chake, Letters to a Young Novelist, Mario Vargas Llosa, mwandishi maarufu kutoka Peru, aliandika:

The defining characteristic of the literary vocation may be that those who possess it experience the exercise of their craft as its own best reward, much superior to anything they might gain from the fruits of their labors. That is one thing I am sure of amid my many uncertainties regarding the literary vocation: deep inside, a writer feels that writing is the best thing that ever happened to him, or could ever happen to him, because as far as he is concerned, writing is the best possible way of life, never mind the social, political, or financial rewards of what he might achieve through it.

Nitafsiri kwa ki-Swahili:

Utambulisho mahsusi wa wito wa uandishi labda ni kwamba wale wenye wito huo huutambua uandishi kama tunu kubwa kuliko zote, bora kuliko chochote wanachoweza kukipata kutokana na juhudi yao. Hiki ni kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho ingawa nimezingirwa na masuali yaletayo wasiwasi kuhusu wito wa uandishi: ndani ya nafsi yake, mwandishi hujisikia kuwa uandishi ni kitu bora kabisa kumtokea au kinachoweza kumtokea, kwa sababu kwa mtazamo wake, uandishi ni mkondo bora kabisa wa maisha, bila kujali manufaa ya kijamii, kisiasa, au kifedha anayoweza kuyapata kwa uandishi.

Kama ilivyo tafsiri yoyote, tafsiri yangu hainasi kila kipengele cha ujumbe wa mwandishi, hasa tukizingatia kuwa tafsiri yangu ni tafsiri ya tafsiri, kwani Mario Vargas Llosa aliandika kwa ki-Hispania. Hata hivi naamini kuna mambo muhimu yanayojitokeza. Mfano ni msisitizo kuwa uandishi kwa wenyewe ni tunu ya thamani kuliko zote. Ni kama kusema kuwa uandishi wa kweli ni ule unaomletea mwandishi faraja kamili na kumfanya asijali matokeo mengine ya uandishi wake, kama vile sifa na fedha.

Nilipokinunua kitabu hiki cha Mario Vargas Llosa, miaka michache iliyopita, nilianza kukisoma nikakutana na dhana fulani ambazo nilishakutana nazo katika maandishi ya Shaaban Robert. Waandishi maarufu wa lugha yoyote ni watu wenye utajiri wa fikra. Hili ni fundisho kwa waandishi chipukizi.

Wakati huu ninaposoma Letters to a Young Novelist, ninasoma pia The Naïve and the Sentimental Novelist, kitabu cha Orhan Pamuk, ambacho nilikinunua hivi karibuni. Orhan Pamuk ni mwandishi maarufu wa U-Turuki, ambaye alipata tuzo ya Nobel. Kitabu chake hiki nacho kinaelezea mtazamo wake kuhusu uandishi. Niliwahi kumtaja mwandishi huyu katika blogu hii, katika kulalamika kuwa maisha hayaturuhusu kusoma vitabu vyote muhimu.

2 comments:

NN Mhango said...

Mwalimu Mbele nakubaliana nawe. Licha ya uandishi kuwa tunu ni kama ugonjwa au moto unaowaka kiasi cha kutaka mwenye kuubeba aendelee kuuchochea. Nakumbuka zamani mke wangu alikuwa akinilalamikia nilipokuwa nikiandika makala kali sana. Alikuwa anauliza, "Kwani usipoandika utakufa?" Mara zote nilimjibu ndiyo. Maana nisipofanya hivyo, nguvu inayonisukuma na kuniwezesha kuandika inaweza kuupasua moyo wangu. Kwa machache tu, kuandika si tunu bali moto unaowaka kwenye nafsi na moyo wa mwandishi. Hata akijitahhidi kuupuuzia haumpuuzii. Nakumbuka niliandika kitabu changu cha kwanza Dear Mothers mwaka 1989. Hadi sasa sijawahi kukichapisha na sijui hata mswada wake niliouacha Tanzania kama bado upo salama.

Mbele said...

Ndugu Mhango, ni sawa kabisa unavyosema. Uandishi wa kweli ni huu unaouelezea kama moto. Siku nyingine, panapo majaliwa, nitaleta mawazo ya Ernest Hemingway ambayo yako katika mkondo huo huo.
Nilianzisha mada hii kwa mategemeo kuwa kuna wanaotafiti au kusomea nadharia za fasihi, nikataka wapate mambo ya kuyatafakari. Na kwa kweli, huwa Napata ujumbe mara moja moja kutoka kwa waandishi chipukizi wa Afrika Mashariki wakiulizia hili au lile.
Mada hii nilitaka wazingatie hasa wale wanaoandika wakiwa tayari na ndoto ya kuwa maarufu, au duku duku na mategemeo ya kazi zao kuingizwa kwenye mitaala ya masomo. Mtazamo aliouelezea Mario Vargas Llosa unajenga hoja kwamba hili ni tatizo, nami ningeweza kuongezea kuwa ni sehemu ya tatizo ambalo wanafalsafa huliita "alienation." Yaani mtu unafanya shughuli kama mashine, bila nafsi yako kufungamana na shughuli yenyewe.
Kinachotakiwa ni kwa uandishi kuwa sehemu ya nafsi ya mwandishi, na uandishi wa aina hiyo unakuwa na uhalisia, kwa ki-Ingereza wanaita "authenticity."