Tuesday, June 30, 2015

Mambo ya Tamasha la Vitabu Mankato

Kila tamasha la vitabu au utamaduni ninaloshiriki huwa na mambo mengi ya kuelimisha na kuburudisha akili. Kukutana na watu na kuongea nao ni sababu muhimu ya ushiriki wangu katika matamasha hayo. Juzi katika tamasha la Deep Valley Book Festival, binti yangu Zawadi nami, tunaoonekana pichani hapa kushoto, tulikutana na kuongea na watu mbali mbali.

Kati ya hao alikuwepo mama mmoja ambaye si rahisi kumsahau. Alifika mezani petu, na wakati tunasalimiana alinyanyua nakala ya Matengo Folktales, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, Notes on Achebe's Things Fall Apart, na Africans in the World, akasema anavinunua.

Wakati wote alikuwa anatuelezea kuwa alikuwa na binti yake ambaye aliishi China kwa miaka nane kisha akaenda Namibia, na kwamba ameipenda Namibia tangu  mwanzo. Alituambia tumwekee vitabu vyake, na kwamba binti yake angefika baadaye.

Yapata nusu saa kabla ya tamasha kwisha, huyu binti alikuja. Tuliongea naye, akatuambia jinsi alivyoipenda Namibia akifananisha na China. Mama yake naye akaja. Akaulizia vile vitabu tulivyomwekea, tukavichukua chini ya meza tulipovihifadhi, tukampa. Aliziangalia "t-shirt," akainyanyua moja na kuilipia. Kwa kuwa alinunua vitu vyote hivi: vitabu vinne na "t-shirt," tulimpunguzia bei, ingawa hakutegemea. Tulisahau kupiga picha pamoja naye na binti yake, kwa kumbukumbu.

Huyu mama hapa kulia ni mwalimu Becky Fjelland Davis wa Chuo cha South Central, Mankato. Ni mpenzi wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na mpiga debe wake mkuu. Nami nilinunua kitabu chake, Jake Riley: Irreparably Damaged.

Huyu mwenzake alijitambulisha kwangu na binti yangu hiyo jana, akasema kwamba alihudhuria mhadhara wangu Chuoni South Central, "Writing About Americans." Huku akiusifia mhadhara ule, alinunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.


Nimeona niiongelee tena picha hiyo hapa kushoto, ingawa nilishaigusia juzi. Huyu mama ni Becky, ambaye nimemwongelea hapa juu. Huyu bwana, Paul Dobratz, ambaye alikuwa katika msafara wa Becky wa Afrika Kusini, alitusisimua, akishirikiana na Becky, kwa habari kem kem na michapo ya safari yao.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Paul kwenda Afrika, lakini Afrika iliuteka moyo wake kiasi kwamba anataka kwenda tena. Nimekutana au kuwasiliana na wa-Marekani wengi ambao wakishafika Afrika wanatekwa mioyo hivi hivi. Mwandishi Ernest Hemingway alikumbwa na hali hiyo wakati alipokuwa akizunguka Tanganyika mwaka 1933-34, kama alivyoandika katika Green Hills of Africa. Yeye na mke wake Pauline walijawa na hisia za kuipenda sana Tanganyika, kiasi kwamba hawakupenda kuondoka. Kwa maneno yake mwenyewe: "We had not left it, yet, but when I would wake in the night I would lie, listening, homesick for it already.”

No comments: