Tuesday, June 9, 2015

"Song of Lawino:" Utungo wa Okot p'Bitek

Sisi tuliosoma sekondari miaka ya mwishoni ya sitini na kitu na kuendelea tunaukumbuka utungo wa Okot p'Bitek, Song of Lawino, ambao ulichapishwa na East African Publishing House, mwaka 1966. Ni utungo uliotusisimua sana kwa namna mhusika wake mkuu, Lawino, alivyozielezea tofauti baina ya utamaduni wa asili wa kabila lake la Acholi, akifananisha na utamaduni wa ki-zungu ambao mume wake anaukumbatia. Lawino ana mtazamo wa aina yake, na anatumia lugha ya ucheshi na kejeli.

Tuliosoma somo la"Literature" katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya sabini na kitu tulikuwa na bahati ya kufundishwa utungo huu na mwalimu Grant Kamenju wa Kenya, ambaye ufundishaji wake ulikuwa wa kusisimua fikra. Alitumia nadharia za akina Karl Marx, Frantz Fanon, Eldridge Cleaver, na wengine wa kimapinduzi katika kuchambua ujumbe wa Lawino.

Alitujengea msimamo wa kuutambua ukoloni mamboleo kama alivyouelezea Fanon, hasa katika The Wretched of the Earth na Black Skin, White Masks. Kitabu cha Cleaver, Soul on Ice, kiliibua masuala yanayowasibu wa-Marekani Weusi kwa ustadi na namna ya kusisimua sawa na alivyofanya Fanon. Kiungo cha yote kilikuwa Song of Lawino.

Mambo mengi yanayotokea leo Tanzania, Afrika, na kwingineko katika hii inayoitwa "Dunia ya Tatu," katika nyanja kama uchumi, siasa, na utamaduni, yalielezwa vizuri na Frantz Fanon. Baadaye yameelezewa vizuri na wengine pia, kama vile Walter Rodney na Ngugi wa Thiong'o.

Nimeamua kuleta ujumbe huu leo kwa sababu maalum. Kwa siku kadhaa, nimekuwa nikiurekebisha mswada wangu, "Notes on the Song of Lawino," ambao ninatarajia kuuchapisha baada ya siku chache. Niliuandika miaka ya mwanzoni ya tisini na kitu, nikawa nnaurekebisharekebisha, na kisha nikauweka kando mwaka 1994. Siku chache zilizopita, nilipata hamasa ya kuanza kuushughulikia tena hadi niuchapishe, kwa kufuata mkondo wa Notes on Achebe's Things Fall Apart.

No comments: