Saturday, June 13, 2015

Nimenunua "Muhammad:" Kitabu cha Deepak Chopra

Jana nilipita kwenye duka la vitabu hapa Chuoni St. Olaf nikanunua kitabu kiitwacho Muhammad kilichotungwa na Deepak Chopra. Nilikiona juzi, nikawa nakiwazia, na jana nikaenda kukinunua.

Deepak Chopra ni mwandishi maarufu, ambaye mawazo yake na mtazamo wake huwagusa watu sana. Ni mhamasishaji na mtoa ushauri kuhusu masuala mbali mbali ya maisha. Ninajua hayo, ingawa sina na wala sijasoma kitabu chake hata kimoja.

Katika kukiangalia kitabu hiki cha Muhammad, nimeona kuwa Deepak Chopra ameandika pia kitabu juu ya Yesu na Buddha. Nikizngatia umaarufu wa mwandishi huyu, naona nijitahidi kusoma angalau hiki nilichonunua.

Ninacho kitabu kingine kiitwacho Muhammad: A Biography of the Prophet, kilichotungwa na Karen Armstrong. Nilikipenda, na niliwahi kuandika juu yake katika blogu hii. Nikiona kitabu hiki cha Deepak Chopra kimenifaa, nitakiongelea pia.

Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa yoyote kutoa maoni yake. Ni uwanja huru kwa mijadala ya mada yoyote. Mara kwa mara ninaandika kuhusu vitabu, vyangu na vya wengine, vikiwemo vitabu vya dini. Nina msimamo wangu kuhusu dini mbali mbali, kuhusu misahafu na kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini. Ninasema hayo ili mgeni katika blogu hii aelewe kwa nini leo ninaleta taarifa kuhusu kitabu kinachohusu dini tofauti na yangu.

No comments: