
Baada ya mkutano, nilipotoka nje kuelekea sehemu nilipopaki gari, alinikimbilia dada Latonya anayeonekana katika picha hapa kushoto, ambayo tulipiga miaka mitano iliyopita kwenye tamasha la Afrifest. Ni m-Marekani Mweusi kutoka Chicago, ila anaishi Minneapolis. Tulifahamiana miaka ile kwa kuwa naye alikuwa katika bodi ya Afrifest Foundation.
Hatukutegemea kama tungeonana leo, ghafla namna ile. Kwa hivi tulifurahi sana. Lakini hakupoteza muda, alianza kunihoji kwa nini siandiki sana katika blogu yangu ya ki-Ingereza kama zamani. Alisema, akimaanisha maandishi yangu ya kiSwahili, "Tunaona unaandika sana, na tunajua unaandika mambo ya maana, ila hatujui unachoandika. Inakuwa kama unatusahau marafiki zako wa-Marekani Weusi."
Kwa kweli, ingawa mazungumzo yalikuwa ya kirafiki, na hata kiutani, niliona kuwa alikuwa anaongea kwa dhati. Na sisi wa-Afrika ambao tunaishi Marekani tunafahamu kuwa wako wa-Marekani Weusi wengi ambao wanategemea sisi wa-Afrika tuwe na mshikamano nao, kama ndugu. Kwa hivi, sikuyachukulia malalamiko ya Latonya kama mzaha. Nilijikuta nikikiri kosa na kuahidi kuwa nitakuwa naandika kama zamani. Alivyowataja wa-Marekani Weusi hakuwa anatunga hadithi. Ninafahamu kuwa wanasoma maandishi yangu.
Latonya mwenyewe ni mmoja wa wafuatiliaji wa dhati wa maandishi yangu. Hapo pichani, anaonekana ameshika kitabu changu cha Africans and Americans:Embracing Cultural Differences, mara baada ya kukinunua. Maneno aliyoniambia leo yameniingia. Nilimwambia hivyo, nikaahidi kujirekebisha.
1 comment:
Ni jambo la kutia moyo sana unavyoona unaungwa mkono na watu wa mataifa. Pia hii inachochea ari na hamasa ya kuandika zaidi.
Pongezi sana mwaalimu.
Post a Comment