Friday, June 19, 2015

Mteja Nimefurahia Huduma

Leo nilipeleka gari langu kwenye kituo cha Car Time hapa mjini Northfield kubadilishiwa "oil." Kwa hapa Marekani, inashauriwa kubadili "oil" kila baada ya kuendesha gari maili 3000. Sijui utaratibu wa Tanzania.

Kama ilivyo kawaida, nilipokewa vizuri, nikakaa sehemu ambapo wateja hungojea huduma. Baada ya dakika kama ishirini hivi, mtu aliyenipokea sehemu ya mapokezi alifika nilipokaa akachuchumaa kwa heshima zote na kuniambia kuwa mafundi walikuwa wamegundua kuwa gari langu linahitaji pia "tire rotation."

Kwa kuogopa kuwa labda ingekuwa gharama ambayo sikujiandaa kuimudu, nilimwuliza kwa utaratibu iwapo itakuwa gharama kiasi gani. Alinijibu kuwa hiyo "tire rotation" haitanigharimu. Nilimjibu kuwa nashukuru kwa huduma hiyo.

Dakika kama kumi tu baadaye. huyu jamaa aliiniita, kuniambia kuwa gari lilikuwa tayari. Alinikabidhi ufunguo na bili yangu, nikalipia, kisha nikashukuru na kuondoka zangu.

Huu ndio utamaduni niliouona hapa Marekani wa kuhudumia wateja. Nimewahi kuandika kuhusu huduma ya Car Time katika blogu hii,. Kila mahali nilipopita, hapa Marekani nimeona utamaduni huu wa kumjali mteja.

Sio mimi pekee mwenye uzoefu huo. Katika mahojiano yangu na Deus Gunza, m-Tanzania mwenzangu, tuliongelea suala hilo, tukakubaliana kuwa huu ndio utamaduni tunaouona hapa Marekani. Kwa upande wangu, nimejionea kuwa hata ukiingia baa, kama mhudumu yuko sehemu nyingine, ni kawaida kumwona meneja anakuja kwenye meza yako, kusafisha na kukuhudumia.

Katika baa za Tanzania, sijawahi kumwona meneja akifanya jambo kama hilo. Utamwona amekaa mahali anapiga gumzo na ulabu na marafiki zake, na akiona mteja umeingia na unangojea huduma, atakachofanya ni kuwaita wahudumu na kuwafokea kwa kukukalisha bila huduma. Sijawahi kumwona meneja akichukua kitambaa na kusafisha meza kwa ajili ya mteja na halafu kumletea kinywaji. Ni kama mwiko.

Kwa nini ninasimulia yote hayo? Ni kwa sababu nina nia ya dhati ya kuwasaidia wafanya biashara na watoa huduma wa Tanzania. Huduma bora kwa mteja ni msingi muhimu wa mafanikio. Hii imani kwamba mafanikio yanatokana na kwenda kwa mganga kusafisha nyota au kupata dawa ya mafanikio ni upuuzi.

Sijaona kampuni yoyote hapa Marekani inayoenda kwa waganga kutafuta dawa. Dawa muhimu ya uhakika ni kumridhisha au kumfurahisha mteja. Kama unauza bidhaa, uhakikishe bidhaa yako ni bora. Na kama biashara yako ni ya kutoa huduma, kama ile ushauri, uhakikishe huduma yako ni bora. Kwa vyovyote vile hakikisha mteja ameridhika au amefurahi. Huyu atakuwa mpiga debe wako. Ukimwudhi ataeneza habari kwa wengine na biashara yako itadhurika. Wataalam wanasema kuwa matangazo haya ya mdomo wanayofanya wateja ni msingi mkuu wa kufanikiwa au kuanguka kwa biashara.

Leo, niliporejea kutoka Car Time, nimemwelezea binti yangu Zawadi na mama watoto yote yaliyojiri, kwa furaha kubwa. Halafu jionee nilivyoandika hapa katika blogu. Nimekuwa mpiga debe wa Car Time bila wao kunilipa. Na ndivyo ilivyo katika maisha yetu. Utamsikia m-Tanzania anaisifia simu yake mpya ya "iPhone" au "smartphone" au "laptop" yake au kitu kingine, bila kutambua kuwa anaipigia debe kampuni ambayo haimlipi chochote, haimjui na wala haichangii uchumi wa Tanzania bali inajitajirisha. Tuna uwezo mkubwa sisi wateja. Laiti tungeutumia kuzitangaza bidhaa na huduma za ki-Tanzania.

Nimejifunza mengi katika kuishi hapa Marekani. Hili nililolieleza ni jambo moja. Ni elimu ambayo ninaitumia katika kuendeleza kampuni yangu ya ushauri ya Africonexion. Ninazingatia sana umuhimu wa kutoa huduma bora, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

2 comments:

NN Mhango said...

Kaka una bahati. Ingekuwa Tanzania hiyo huduma ya tire rotation ungechajiwa hata kama inatolewa bure. Wenzetu wana ustaarabu wa kupigiwa mfano hasa ukilinganisha na ushenzi unaofanyika nyumbani. Mfano huku ukinunua kitu na kukuta kuwa ima hukihitaji au hakifai au mwenzio alishanunua kingine unamrejeshea aliyekuuzia. Jaribu hilo nyumbani. Hatapokea hiyo bidhaa zaidi ya kukurushia mitusi. Rafiki yangu toka Nigeria alisema kuwa ukirejesha bidhaa dukani kwao utaambulia kipigo. Huwa najiuliza: Ni lini tutafikia kiwango hiki cha utu na huduma bora? Ajabu hata watawala wetu wanapokuja huku wakatendewa hivi hawaendi kurudufu hili. Badala yake sijui huwa wanajifunza nini?

Mbele said...

Ndugu Mhango, ni kweli usemavyo. Hapa Marekani, ukinunua kitu, una uhuru wa kukirudisha kwa sababu yoyote ile, au hata kama huna sababu. Unachohitaji ni kuonyesha risiti tu, ambayo ulipata uliponunua. Uamuzi ni wako, kwa mfano labda unataka kitu kile kile ila rangi tofauti, au saizi tofauti, au unataka kurudishiwa pesa zako. Wanaheshimu kabisa matakwa ya mteja, na unapoondoka wanakuambia karibu tena.

Tanzania kuna vituko, ambavyo tumeishi navyo tangu zamani. Kwa mfano, kuna risiti nyingi ambamo kumeandikwa wazi kuwa kitu kikishanunuliwa, huwezi kukirudisha. Risiti yenyewe inasema hivyo. Kama umelizwa basi wewe ulie tu.

Unaingia katika maduka mengi Tanzania, au sehemu ya kupatia huduma, hata kama ni ofisi, na unapokelewa kama vile wewe ni kero fulani. Ni nadra kukaribishwa vizuri. Mara kwa mara, nimewakalisha chini mameneja na wahudumu kwenye baa na kuwapa mhadhara kuhusu thamani halisi ya mteja, hata kama ananunua soda moja tu na kwenda zake.
Watawala wetu nao ni sifuri. Mengi wanayaona huku ughaibuni, kwa mfano usafi wa miji, lakini wakisharejea Bongo, wanaidhika wala haiwasumbui kuona mitaro michafu, malundo ya takataka kila mahali, mifuko ya plastiki inapeperushwa na upepo mitaani, migahawa iko pembeni mwa mitaro, na kadhalika na kadhalika.
Huwa nashangaa kwa nini wanaitwa viongozi, wakati hakuna wanachoongoza wala wanayemwongoza. Ni watawala, kama unavyosema. Pamoja kwenda shule, hawatambui hata suala la msingi la umuhimu wa usafi katika mazingira.
Uchafu wa mazingira, kwa mujibu wa wanafalsafa fulani ni kioo cha uchafu wa moyoni. Moyo ya ukatili wa watoa huduma na jamii kwa ujumla ni moyo huo huo unaoleta na kudumisha ukatili dhidi ya mazingira.