Tuesday, June 23, 2015

Imekuwa Siku ya Mafanikio Makubwa

Leo imekuwa siku ya mafanikio makubwa. Kwanza nilienda Chuo Kikuu cha Winona na binti yangu Zawadi nikatoa mhadhara. Nilitumia hadithi za jadi kujadili namna wahenga wetu walivyozielewa dhana za uongozi na uwajibikaji.

Baada ya kuelezea kwa ufupi jinsi Afrika ilivyokuwa chimbuko la binadamu, lugha, sayansi, tekinolojia, na falsafa, nilisimulia hadithi mbili zilizomo katika kitabu changu cha Matengo Folktales, kuthibitisha namna wahenga wetu walivyoyatafakari masuala ya jamii. Hadithi hizo ni "The Monster in the Rice Field" na "Nokamboka and the Baby Monster."

Baada ya kurejea kutoka Winona, tulijiandaa kwenda Excelsior, kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya "Papa's Shadow." Filamu hii inamhusu mwandishi Ernest Hemingway, na kwa kiasi kikubwa ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, kuhusu maisha, uandishi, na fikra za Hemingway.

Matokeo ya mazungumzo yetu yalivyo katika filamu yamewasisimua sana watazamaji. Nilitegemea hivyo, kutokana na kwamba inaleta mtazamo mpya juu ya Hemingway.


Mtengenezaji wa filamu ni Jimmy Gildea, ambaye alikuwa mwanafunzi wangu katika kozi ya "Hemingway in East Africa," niliyofundisha Tanzania mwezi Januari mwaka 2013. Anaonekana pichani hapa kushoto akiwa nami na binti zangu.

3 comments:

mandela pallangyo said...

Ama kweli inavutia sana. Nafurahi sana nnapo ona watanzania tukifanya vitu vizuri na kukubalika nchi za watu. Ngoja nasi tusome kwa bidii uenda nikaja kutoa ushamba siku moja

Mbele said...

Ndugu Mandela Pallangyo

Nimefurahi kuuona ujumbe wako, na kuona kuwa nimeweza kuwa chachu ya wewe kutaka kufanikiwa. Penye nia pana njia.

Mimi nimetoka mbali. Niliamua tangu ujana wangu kuzingatia usomaji wa vitabu na kutafuta elimu. Hiki kilikuwa kipaumbele kwangu. Mara kwa mara, wa-Tanzania hawakunielewa, kwa kuwa sikuweka kipaumbele katika utajiri wa vitu, kama vile magari. Nilizingatia kuwa hazina kubwa kuliko zote ni elimu. Niliwekeza katika elimu.

Leo, kutokana na uwekezaji huu wa tangu ujana wangu ninaona matunda yake. Mfano hai ni jinsi ninavyoitwa huko na huko hapa Marekani kutoa mihadhara na ushauri, kama ninavyoripoti katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza. Nimejikuta katika nchi ya watu wanaothamini elimu na utaalam wa mtu, wala hawajali kama unatembea kwa baiskeli au kwa mguu. Ni tofauti na Tanzania.

Sisemi hayo kwa kubabaisha. Nilifundisha Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976. Hapa Marekani nilianza kufundisha mwaka 1991. Ninakwenda Tanzania mara kwa mara, na hata ninapokuwa hapa Marekani, nina mawasiliano na wa-Tanzania muda wote. Kwa hivi ninajua ninachosema.

Kila ninapokutana na vijana Tanzania, nawaambia wazingatie elimu. Wasiyumbishwe.

NN Mhango said...

Kaka nimefurahi kusikia kuwa binti yako ametoa mhadhara. Mtoto wa nyoka ni nyoka. Kuwarithisha watoto maarifa na ujuzi ni jambo jema sana. Nami binti wangu wa kwanza Nthethe anaanza chuo mwezi wa tisa baada ya kuchelewa mwaka mmoja ili ajiandae.