

Nilivyoingia ndani, nilijikuta sehemu hii inayoonekana kushoto, ingawa ni kubwa na pana zaidi ya hii inayoonekana pichani. Wakutubi wengi wapo katika eneo hilo, tayari kuwasiaida wateja, na sehemu ya maulizo ambayo ni kubwa pia, iko eneo hili. Unapokuwa sehemu hii, kwa mbele yako na pembeni kuna maeneo yenye vitabu, majarida, kompyuta nyingi na hifadhi mbali mbali za taarifa, kama vile CD, DVD na na kaseti.
Niliulizia kilipo chumba cha mkutano, nikapita katikati ya makabati ya vitabu vya kila aina hadi mwishoni kabisa.

Hiyo jana ilikuwa ni Jumamosi, na ilikuwa ni alasiri. Jua lilikuwa linawaka vizuri, na walikuwepo watu wengi katika maktaba, watu wa kila rangi, na kila rika. Wwnginw walikuwa wanasoma vitabu, wengine wanaazima, wengine wanatumia kompyuta, na wengine walikuwa wanarudufu maandishi.
Nilivyoangalia hali hii, ya watu wengi kuwemo maktabani wakati wa alasiri, Jumamosi, niliwazia hali ya Tanzania. Nilijiuliza ni wapi katika Tanzania unaweza kuona hali hii, tena Jumamosi mchana. Ni wapi unaweza kuwaona watu wa rika mbali mbali wamejaa maktabani wanajisomea. Hata huyu dada Latonya niliyekutana naye jana hapo nje ya maktaba alikuwa anakuja maktabani na akina dada wenzake.
Ningekuwa na uwezo, ningebadili mioyo ya wa-Tanzania, wawe kama hao wa-Marekani, wenye kupenda kusoma. Ningehamasisha ujenzi wa maktaba zaidi. Kwa mji kama Dar es Salaam, ningependa ziwepo maktaba Sinza, Kinondoni, Buguruni, Kigamboni, Kawe, Kimara, Ukonga na sehemu zingine. Ingekuwa ni Marekani, mji wa ukubwa wa Dar es Salaam ungekuwa na maktaba nyingi. Lakini, miaka hamsini na zaidi tangu tupate uhuru, maktaba ni hiyo hiyo moja. Si jambo la kujivunia.
No comments:
Post a Comment