Monday, June 8, 2015

Nimerekebisha Kitabu Changu

Kwa zaidi ya wiki moja, nimekuwa nikikipitia kitabu changu cha Matengo Folktales kwa ajili ya kukiboresha. Rekebisho moja nililofanya ni kuongeza ukubwa wa herufi ili kitabu kisomeke kwa urahisi zaidi. Nilikuwa pia naangalia kama kuna kosa lolote katika uandishi wa maneno. Nimerekebisha dosari zilizoziona katika maneno yapata matano

Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena.

Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha nilijionea mwenyewe kuwa hapakuwa na kitabu nilichoona kinafaa kwa somo la fasihi simulizi kwa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu. Kuna usemi kuwa kama kitabu unachosoma huridhiki nacho, andika hicho kitabu unachokitaka.

Hali hiyo ya kukosekana kitabu kilichofaa katika ufundishaji wangu ilinihamasisha kutafakari masuala niliyokuwa nakumbaba nayo katika kuandika kitabu changu. Nilipania kuwa kiwe kinafaa kwa kufundishia. Miaka ilipita, nami nikawa natafiti, natafakari, na kuandika kiasi nilivyoweza. Wakati huo huo, nilikuwa nahangaika kuziboresha tafsiri za hadithi katika muswada. Shughuli hii ilinifundisha mengi kuhusu tafsiri, kama nilivyogusia katika makala iliyochapishwa katika jarida la Metamorphoses.

Historia ya kitabu hiki ni ndefu, na labda nitaweza kuiandika kiasi fulani siku za usoni. Ninakumbuka, kwa mfano, kwamba nilipokuwa nasomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, 1980-86, nilichukua somo la nadharia ya fasihi katika idara ya "Comparative Literature" lililofundishwa na Professor Keith Cohen. Kati ya nadharia tulizojifunza ni "Structuralism." Professor Cohen alitupa "homework" ya kuchambua hadithi yoyote kwa kutumia nadharia ya "Structuralism."

Nilitumia fursa hii kuichambua hadithi ya "The Tale of Two Women," ambayo imo katika Matengo Folktales. Mtu anayefahamu angalau kidogo nadharia ya "Structuralism" ataona athari zake, japo kidogo,  katika uchambuzi wangu.

Baada ya harakati za aina aina kwa miaka mingi, nilichapisha kitabu hiki mwaka 1999. Ndoto yangu ya kuandika kitabu cha kutumiwa katika ufundishaji wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haikutimia nilivyotarajia. Niliondoka Tanzania mwaka 1991, nikaja kufundisha katika idara ya ki-Ingereza Chuoni St. Olaf, huku  nikiwa bado naufanyia kazi mswada wangu. Kwa hivi kitabu kilichapishwa huku Marekani, na wanaokisoma ni wa-Marekani, kuanzia katika jamii hadi vyuoni, kama nilivyoelezea hapa na  hapa.

Masimulizi ni mengi, na kama nilivyogusia, labda nitafute wasaa miaka ijayo niandike kumbukumbu zangu za historia ya kitabu hiki.

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...


Ni busara na jambo jema ulilifanya kupitia maandishi yako na kuyaboresha. Niseme kuwa hilo ni jukumu ambalo sio waandishi wote hulifanya japo wengine waliyoandika ni yenye madhara sana kwa watu na amani ya ulimwengu.

Ulipomtaja Prof Keith Cohen, nilitaka kujua kazi zake na pengine maandishi yake. Nilipogoogle jina lake nilifadhaika kuona tuhuma juu yake na hatimaye barua kali ya kutaka board ya chuo imwachishe kazi kwa kwenda kinyume na kanuni za chuo hicho nakadhalika. Inasikitisha sana msomi kushutumiwa kwa yale ambayo Keith anadaiwa kuyafanya.

Jambo hilo limenifanya nitafakari na kukumbuka yale niliyopata kushuhudia chuoni, wakati Dr. mmoja maarufu alipojiwa na mkewe na kutaka kuzipiga katika faculty na mwanafunzi wa kike ambaye Dr. huyo alianzisha mahusiano na yeye. Ilikuwa kazi kwelikweli lakini mwishowe ni kama hayo yaliomkuta Keith.

Wasomi na maadili ya jamii ni jambo muhimu kujadiliwa kwa kina ili tujenge jamii ambayo haitojifunza wasemayo wasomi lakini wasome kwa vitendo vyao pia.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Sina namna ya kuelezea furaha na shukrani zangu kwa jinsi unavyofuatilia blogu yangu na kuchangia. Binafsi, ninauenzi mchango wako.

Nimefurahi kuona ulivyofuatilia taarifa za Profesa Cohen, niliyemtaja. Huu, kwa vigezo vyangu, ni uthibitisho wa kuelimika. Ishara ya kuelimika ni kuwa na dukuduku isiyoisha ya kutafuta elimu, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "intellectual curiosity."

Miaka ile alipotufundisha, Profesa Cohen alikuwa mwalimu wa kupigiwa mfano, sawa na wengine walionifundisha katika chuo kile maarufu. Profesa Cohen ndiye aliyenifungua akili katika mikondo mipya ya nadharia za fasihi.

Nimetoa mfano wa "Structuralism," kwa sababu nilikuwa naongelea kitu katika kitabu changu. Lakini alitufundisha pia nadharia kama za "Formalism" na "Semiotics." Nami, niliporejea tena kuendelea kufundisha Chuo Kikuu Dar, niliwafundisha hayo wanafunzi wa shahada ya uzamili, akina Hamza Njozi, Elias Songoyi na wenzao. Hao nimewataja kwa kuwa nao wanafundisha katika vyuo vikuu Tanzania.

Nimeandika hicho kidogo kuthibitisha mchango wa Profesa Cohen katika elimu yangu, kuniivisha vilivyo, nami nikatoa na ninaendelea kutoa mchango kwa wa-Tanzania na walimwengu.

Miaka ya baadaye sana. nilisikia habari za hayo mabaya. Mtu wa kwanza kuniambia alikuwa mama mmoja profesa katika idara ya "Comparative Literature" katika chuo kile kile cha Wisconsin-Madison, ambaye tulisoma kozi moja katika idara ile ile. Tulikuwa kwenye mkutano Chicago, akaniambia kuhusu kesi ya Profesa Cohen.

Nilisikitika, na bado nasikitika. Mtu anayetegemewa, kuheshimiwa na kupigiwa mfano katika jamii anapotumbukia katika kashfa, anatuweka wengi wetu njia panda. Tuliomfahamu na kumheshimu tunasikitika. Kisaikolojia, wanadamu wengi tunaingiwa na hofu, kwamba kama alianguka huyu, sembuse sisi. Yanaweza kutupata. Lakini, dunia ina mengi ya kujifunza. Wako pia wanadamu ambao, wakikuona unafanikiwa au umefanikiwa, hawakutakii mema, na ukianguka, wanafurahi.

Ndugu Khalfan Abdallah Salim umehitimisha ujumbe wako vizuri sana kwa kutukumbusha umuhimu wa kutafakari na kujadili. Napenda nichangie kwa kumnukuu Shakespeare, mwanatamthilia maarufu labda kuwazidi wote, na mchunguzi makini wa tabia za wanadamu. Katika tamthilia yake ya "Julius Caesar," mhusika mkuu mmojawapo aitwaye Antonio anasema:

"The evil that men do lives after them;
The good is oft interred with their bones..."

Natafsiri kwa ki-Swahili:

"Uovu wafanyao wanadamu hudumu baada ya kifo chao;
Wema wao aghalabu huzikwa pamoja na mifupa yao...."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...