Showing posts with label utafiti. Show all posts
Showing posts with label utafiti. Show all posts

Wednesday, June 7, 2017

Umuhimu wa Kumpigia Mbuzi Gitaa

Katika jamii yetu wa-Tanzania, usemi kwamba usimpigie mbuzi gitaa unachukuliwa kuwa ni ukweli usiopingika, busara isiyo na walakini. Ni kile kinachojulikana kama busara ya kawaida, yaani "common sense," kwa ki-Ingereza. Lakini je, mtazamo huu ni sahihi? Hili ndilo suala ninalopenda kulijadili hapa, kwa mtazamo wangu kama msomi, mtafiti na mwalimu.

Napenda kutamka wazi kuwa kwa msomi au mwalimu au mtafiti, "common sense" ni kitu cha kujihadhari nacho. Kazi ya msomi, mwalimu au mtafiti si kuzingatia, kuafiki, au kuhalalisha "common sense," bali kuhoji na kudadisi "common sense." Ndivyo alivyofanya mwelimishaji maarufu Socrates. Kuna wengi wengine, kama vile Galileo. Jamii yote ilielewa kuwa jua linaizunguka dunia, kwani kila mtu alijionea mwenyewe. Ilikuwa ni "common sense." Lakini Galileo, akiendeleza mawazo ya Copernicus, alisema kuwa ni dunia ndio inayolizunguka jua. Jamii ya Galileo ilimtia matatani, kama vile jamii ya Socrates ilivyomtia matatani.

Turudi kwenye suala la kumpigia mbuzi gitaa. Ninapenda kusema kuwa ni wajibu wa msomi, mtafiti, au mwalimu kuhoji hii busara ya jamii kwamba kumpigia mbuzi gitaa ni kupoteza muda au ni ujinga. Msimamo huu wa jamii una walakini mkubwa. Ukipiga gitaa, inatoa sauti. Je, jamii inamaanisha kuwa mbuzi hana uwezo wa kutambua na kuguswa na sauti? Kama jamii inaamini hivyo, inakosea.

Sisi ambao tulikulia kijijini tukichunga mbuzi tunajua kuwa mbuzi wana milio yao ambayo wanatumia kuwasiliana. Hata wakati wa kuchunga, tulikuwa tunaweza kutambua mlio wa mbuzi mwenye dhiki. Tulikuwa tunawaita mbuzi kwa majina tuliyowapa au kwa kupiga mluzi. Kwa hivi, jamii inakosea iwapo inaamini kuwa mbuzi hawana uwezo wa kujieleza, kutambua au kuguswa na sauti.

Suala la kulitafakari ni sauti ipi ambayo mbuzi anaitambua na kuguswa nayo, na ipi hawezi kuitambua na kuguswa nayo. Kinachohitajika si hiyo "common sense" kwamba usimpigie mbuzi gitaa, bali utafiti. Tunatakiwa kumpigia mbuzi gitaa tena na tena, kwa mitindo mbali mbali.

Utafiti hauwekewi kikomo. Hata pale tunapodhani tumepata ufumbuzi wa suala, hatupigi marufuku utafiti zaidi wa suala hilo. Badala ya kuridhika na busara ya jamii kuwa tusimpigie mbuzi gitaa, mtafiti au msomi huwaza: kwa nini nisimpigie mbuzi gitaa? Itakuwaje nikimpigia mbuzi gitaa? Ngoja nimpigie mbuzi gitaa nione kitakachotokea. Huu ndio mtazamo wa mtafiti, msomi, na mwalimu. Hii duku duku ya kujua huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Msomi au mtafiti au mwalimu ni mtu anayetafuta elimu muda wote. Thomas Edison, mvumbuzi maarufu, alifanya majaribio ya kuvumbua na kuunda vitu akashindwa mara nyingi sana, lakini hatimaye alivumbua balbu ya umeme. Huu ndio moyo unaohitajika katika suala hili la kumpigia mbuzi gitaa. Tukitaka mfumo wa elimu wa kweli, inatubidi tujenge mtazamo na mwelekeo huu wa kutambua umuhimu kumpigia mbuzi gitaa.

Unapofanya utafiti kwa ajili ya kuchunguza suala fulani huwezi kujua matokeo yatakuwa yepi. Unaweza kupata matokeo ambayo hukutegemea. Katika majaribio yake ndani ya maabara, mwaka 1928 Alexander Fleming aliona kitu kimejitokeza kwenye kisahani kimojawapo alimoweka vitu vya kuvichunguza. Kitu hicho kilikuwa kimejitokeza bila yeye kutegemea, lakini ndicho kilikuja kubainika kuwa ni penicillin.

Kwa hivyo, mtu ukianza kumpigia mbuzi gitaa, ukawa anafuatilia kwa makini kila kinachotokea, huenda utajifunza mambo ambayo hakutegemea kuhusu tabia na hisia za mbuzi. Inawezekana ukipiga gitaa mara ya kwanza usione lolote likitokea. Lakini je, unajuaje kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ukimpigia mara kumi, au mara mia, au zaidi?

Kama unadhani ninatania, napenda tujikumbushe utafiti na uvumbuzi aliofanya Ivan Pavlov akitumia mbwa. Pavlov alifanya majaribio ambayo yalitoa mchango mkubwa katika taaluma ya saikolojia. Nashauri msomaji utafute taarifa za Pavlov na majaribio yake na uvumbuzi aliofanya. Huenda utakubaliana nami kuwa suala la kumpigia mbuzi gitaa si la kupuuzwa. Ni muhimu.

Sunday, May 22, 2016

Leo Nimemwandikia Mzee Patrick Hemingway

Leo nimemwandikia barua pepe Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Nilipiga naye picha inayoonekana hapa kushoto tarehe 27 Aprili, 2013, nyumbani pake mjini Craig, katika jimbo la Montana.

Nilifahamu habari zake kwa miaka mingi kabla ya kufahamiana naye na halafu tukakutana. Ni mzee mwenye maongezi ya kusisimua kuhusu baba yake Ernest Hemingway na waandishi wengine wa wakati wake. Pia ana kumbukumbu nyingi za Tanganyika, na kisha Tanzania, ambako aliishi kwa miaka yapata 25 kabla ya uhuru na baada ya uhuru, akiendesha kampuni ya utalii, na hatimaye akiwa mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mwika.

Tangu tulipoanza kufahamiana, ameguswa na ari yangu ya kutafiti maandishi, falsafa, na maisha ya Ernest Hemingway, na amevutiwa na msimamo wangu kuwa Ernest Hemingway ni mwandishi aliyetuenzi sana sisi watu wa Afrika Mashariki, na tunapaswa kujielimisha kuhusu mchango wake, na kisha kuutumia katika kujitangaza kama alivyotutangaza.

Hayo yamemfanya Mzee Patrick Hemingway awe tayari kunisaidia kwa dhati katika juhudi zangu za kujielimisha na kuuelimisha ulimwengu juu ya Ernest Hemingway. Miezi kadhaa iliyopita, nilivyomweleza kuwa napangia kutembelea hifadhi ya Ernest Hemingway katika John F. Kennedy Library, aliniambia kuwa nitakapokuwa tayari nimfahamishe ili anitambulishe kwa wahusika.

Nilipoongea naye tarehe 19 mwezi huu na kumtajia tarehe nilizopangia kwenda kwa shughuli hiyo, aliniagiza nimpelekee maelezo yangu kwa barua pepe, ili aweze kuandaa utambulisho huo. Aliniambia kuwa ninakwenda wakati mzuri, kwani kuna maonesho maalum juu ya Hemingway, ambayo yameanza siku chache zilizopita na yatadumu kwa miezi kadhaa.

Basi, leo nimemwandikia. Kilichobaki sasa ni kuandaa safari, nikajionee hiyo hifadhi kubwa kuliko zote duniani juu ya Ernest Hemingway. Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuitembelea hifadhi hiyo, lakini sitegemei kuwa itakuwa ni mara ya mwisho.

Wednesday, May 18, 2016

Muhula Unaisha; Umebaki Utafiti

Jana tumemaliza muhula wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nilikuwa ninafundisha "Folklore," Muslim Women Writers, na "First Year Writing." Kwa utaratibu wa chuo hiki, masomo matatu kwa muhula ndio kiwango cha juu kabisa. Hatufundishi zaidi ya masomo matatu. Kwa hivi, nilitegemea ningekuwa nimechoka, lakini sisikii uchovu. Alhamdulillah.

Kwa wiki nzima inayokuja, tutakuwa na mitihani. Baada ya hapo tutaanza likizo ndefu ya miezi mitatu na kidogo. Inaitwa likizo, lakini maprofesa tunaona ni wakati muafaka wa kufanya shughuli za kitaaluma kama utafiti na uandishi.

Nami nimeamua kwenda Boston kwa siku chache kufanya utafiti juu ya Ernest Hemingway katika maktaba ya John F. Kennedy. Humo kuna hifadhi kubwa kuliko zote duniani ya vitabu, miswada, picha na  kumbukumbu zingine zinazomhusu Hemingway. Ingawa nimefika Boston mara kadhaa, sijawahi kwenda katika maktaba hiyo maarufu.

Nina bahati kuwa ninafahamiana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway ambaye bado yuko hai. Yeye ndiye mmiliki wa haki zote za urithi wa Hemingway. Nilipomwambia kwa mara ya kwanza kwamba napangia kwenda kufanya utafiti katika maktaba ya John F. Kennedy,  aliniambia nimfahamishe ni lini ili anitambulishe kwa wahusika. Wiki chache zilizopita, katika maongezi yetu, nilimwambia tena kuwa napangia kwenda kwenye maktaba ile, alikumbushia kuwa nimweleze ni muda upi nitakwenda ili awafahamishe.

Ninashukuru sana kwa hilo, kwani katika kusoma taarifa za maktaba ile, nimefahamu kuwa kuna masherti yanayohusu kuitumia hifadhi ya Ernest Hemingway. Mtu hukurupuki tu ukafika pale na kufanya utafiti. Kuna baadhi ya kumbukumbu ambazo zimefungiwa. Mtafiti unahitaji kibali maalum kuweza kuzifanyia utafiti. Sherti nichukue hatua hima.

Wednesday, December 30, 2015

Nimekutana na Mdau wa Miaka Mingi

Leo nimekutana na mdau wangu wa miaka mingi, Dr. Barbara Poole Galyen, ambaye anaishi California. Kwa siku chache hizi za Krismasi na Mwaka Mpya, yuko hapa Minnesota kwa ndugu zake. Kwa kupitia facebook tuliwasiliana na leo nilikwenda mjini Lakeville alikofikia.

Dr. Galyen na mimi tulifahamiana mwaka 1995, wakati nilipokuwa natafiti masimulizi ya jadi na tamaduni mkoani Mwanza. Utafiti huo ambao nilifanya tangu mwaka 1993 hadi 1996 uligharamiwa na shirika la Earthwatch. Dr. Galyen alikuwa mmoja wa watu kutoka nchi mbali mbali waliokuwa wanakuja Tanzania kushiriki utafiti wangu. Yeye alikuja wakati wa utafiti kisiwani Ukerewe.

Kwa kauli yake mwenyewe, huu ulikuwa mwanzo na msingi wa yeye kuipenda Afrika, hadi akaenda kufanya kazi Kenya katika United States International University, ambapo nilimtembelea mwaka 1997. Hatimaye alianzisha kampuni ya ushauri kuhusu masuala tamaduni ulimwenguni. Shughuli hizi, ambazo zinafanana na zangu, zimempa fursa ya kuzunguka sehemu mbali mbali za dunia na kujenga mtandao wa kimataifa wa washiriki.

Leo imekuwa furaha kubwa kuonana tena baada ya miaka mingi, kubadilishana mawazo na kupiga michapo. Nilimchukulia nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambamo nimegusia mambo yaliyotokana na utafiti wangu wa Earthwatch.

Dr. Galyen mwenyewe katika ukurasa wake wa facebook, ameandika kuhusu kukutana kwetu leo:

I enjoyed a wonderful visit with Dr. Joseph Mbele who was the one who originally introduced me to Africa in 1995 on an "Earthwatch" adventure. I give him credit for changing my life completely after I moved to Kenya as a result of our fascinating studies on a remote island in Lake Victoria, TZ. Born in Tanzania, Dr. Mbele is currently a professor at St. Olaf College in MN where he continues to work on special projects around the world! He's inspiring me again to get more involved in heart-felt projects globally.

Monday, December 28, 2015

Kitabu Juu ya Charles Dickens

Siku chache zilizopita, niliingia katika gereji yangu ambayo imefurika vitabu. Katika kufukua fukua, nilikiona kitabu Dickens, kilichotungwa na Peter Ackroyd. Sikumbuki nilikinunua lini na wapi, ila niliamua kukichukua, kwa lengo la kukipitia angalau juu juu. Nina vitabu kadhaa vilivyotungwa na Dickens. Baadhi nimevisoma na baadhi sijavisoma.

Dickens ni kati ya waandishi ambao watu wa rika langu tuliwasoma miaka ya ujana wetu Tanzania, tukawapenda sana. Kutokana na mvuto huu, nimeandika juu ya Dickens mara kadhaa katika blogu hii. Mifano ni hapa, na hapa. Kwa hivyo, nilivyokigundua kitabu cha Dickens katika gereji,  nilifurahi, nikakichukua hima.

Nilikuwa nafahamu jina la mwandishi Peter Ackroyd, ingawa sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu chake chochote. Katika kupitia taarifa kwenye jalada la kitabu chake cha Dickens, nimeona orodha ya vitabu alivyoandika na umaarufu wake. Kwa mfano, amejijengea heshima kubwa kwa kuandika vitabu vya historia na wasifu wa waandishi kama William Shakespeare na William Blake .

Kitabu cha Dickens ni wasifu wa Dickens, maelezo kuhusu maisha yake na maandishi yake, pamoja na maelezo kuhusu jamii alimoishi na kuandika. Ni kitabu kilichosheheni uchambuzi wa maandishi ya Dickens, sambamba na uchambuzi wa uhusiano baina ya maandishi hayo na jamii. Ni matunda ya utafiti wa kina na mpana. Dickens ni hazina kubwa, kitabu chenye kurasa 1195.

Nimekuwa nikikipitia kwa mshangao juu ya juhudi na umakini uliotumika katika utafiti na uandishi wake. Ninafahamu kuwa wenzetu wa nchi kama za Ulaya na Marekani wana jadi ya kufanya utafiti wa kina na kuandika kwa umakini kuhusu waandishi wao maarufu. Kwa mfano, kuna vitabu vya aina hiyo juu ya William Shakespeare, Johann Wolfgang von Goethe, Henrik Ibsen, Leo Tolstoy, Mark Twain, Ernest Hemingway, na William Faulkner.

Tukijifananisha na hao wenzetu, sisi wa-Tanzania tumefanya utafiti gani na tumeandika nini juu ya waandishi wetu maarufu kama Mgeni bin Faqihi na Shaaban Robert? Hakuna chochote ambacho tumefanya kinachoweza kufananishwa na majuzuu makubwa aliyoandika Michael Reynolds juu ya Ernest Hemingway, achilia mbali majuzuu waliyoandika wengine juu ya huyu huyu Charles Dickens. Labda, kwa kutafakari hayo tutagundua na kukiri kuwa tuna njia ndefu mbele yetu.

Saturday, September 12, 2015

Wazo Kuhusu Kuchagua Kiongozi

Tunavyoelekea kwenye uchaguzi, mwezi ujao, nchini Tanzania, tunaona malumbano yanashamiri. Tunataka kujua nani anafaa kuwa kiongozi. Napenda kuchangia kifupi malumbano haya. Mchango wangu unasimama katika taaluma na utafiti.

Suala la uongozi linaingia moja kwa moja katika utafiti juu ya akili na saikolojia. Miaka yetu hii, watafiti wamekuwa wakituambia kuwa kuna aina nyingi za akili. Kuna maandishi mengi juu ya suala hilo, ambalo kwa ki-Ingereza linajulikana kama "multiple intelligence" au "multiple intelligences."

Kwa mujibu wa utafiti huo, uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Ni akili inayomfanya mtu awe na mvuto kwa watu kwa haiba na mwenendo wake, uwezo wa kuunganisha watu, uwezo wa kuwafanya wafuate njia fulani kwa kutumia ushawishi, si vinginevyo. Mtu mwenye "emotional intelligence" kubwa ndiye anayefaa kuwa kiongozi.

Katika malumbano yanayoendelea miongoni mwa wa-Tanzania wakati huu wa kuelekea uchaguzi, sijaona dhana hii ya "emotional intelligence" ikitajwa. Sijaona kigezo hiki kikitajwa. Watu wanaongelea vitu kama uchapa kazi kama kigezo, lakini si "emotional intelligence." Watu wanaongelea uwezo wa kutoa hotuba ndefu, au uwezo wa kutembea kwa ukakamavu. Lakini hawaongelei "emotional intelligence."

Kwani kutoa hotuba ndefu ndio nini? Mtu unaweza kuongea kwa masaa lakini ukawa unasema umbea na upupu. Mtu mwingine anaweza kuongea kifupi, lakini akawa anatoa hoja thabiti.

Kwani nguvu za mwili na kifua kama cha mpiga ndondi ndio nini? Inahusiana vipi na uongozi? Lakini hivyo ndivyo vigezo vinavyoshabikiwa katika malumbano ya wa-Tanzania.

Hii haishangazi. Tanzania ni nchi ya watu wasio na utamaduni wa kusoma vitabu vya kuelimisha. Watanzania ni wavivu kutafuta elimu. Ndivyo walivyo, na ndivyo wanavyojiandaa kwa uchaguzi.

Monday, June 8, 2015

Nimerekebisha Kitabu Changu

Kwa zaidi ya wiki moja, nimekuwa nikikipitia kitabu changu cha Matengo Folktales kwa ajili ya kukiboresha. Rekebisho moja nililofanya ni kuongeza ukubwa wa herufi ili kitabu kisomeke kwa urahisi zaidi. Nilikuwa pia naangalia kama kuna kosa lolote katika uandishi wa maneno. Nimerekebisha dosari zilizoziona katika maneno yapata matano

Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena.

Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha nilijionea mwenyewe kuwa hapakuwa na kitabu nilichoona kinafaa kwa somo la fasihi simulizi kwa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu. Kuna usemi kuwa kama kitabu unachosoma huridhiki nacho, andika hicho kitabu unachokitaka.

Hali hiyo ya kukosekana kitabu kilichofaa katika ufundishaji wangu ilinihamasisha kutafakari masuala niliyokuwa nakumbaba nayo katika kuandika kitabu changu. Nilipania kuwa kiwe kinafaa kwa kufundishia. Miaka ilipita, nami nikawa natafiti, natafakari, na kuandika kiasi nilivyoweza. Wakati huo huo, nilikuwa nahangaika kuziboresha tafsiri za hadithi katika muswada. Shughuli hii ilinifundisha mengi kuhusu tafsiri, kama nilivyogusia katika makala iliyochapishwa katika jarida la Metamorphoses.

Historia ya kitabu hiki ni ndefu, na labda nitaweza kuiandika kiasi fulani siku za usoni. Ninakumbuka, kwa mfano, kwamba nilipokuwa nasomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, 1980-86, nilichukua somo la nadharia ya fasihi katika idara ya "Comparative Literature" lililofundishwa na Professor Keith Cohen. Kati ya nadharia tulizojifunza ni "Structuralism." Professor Cohen alitupa "homework" ya kuchambua hadithi yoyote kwa kutumia nadharia ya "Structuralism."

Nilitumia fursa hii kuichambua hadithi ya "The Tale of Two Women," ambayo imo katika Matengo Folktales. Mtu anayefahamu angalau kidogo nadharia ya "Structuralism" ataona athari zake, japo kidogo,  katika uchambuzi wangu.

Baada ya harakati za aina aina kwa miaka mingi, nilichapisha kitabu hiki mwaka 1999. Ndoto yangu ya kuandika kitabu cha kutumiwa katika ufundishaji wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haikutimia nilivyotarajia. Niliondoka Tanzania mwaka 1991, nikaja kufundisha katika idara ya ki-Ingereza Chuoni St. Olaf, huku  nikiwa bado naufanyia kazi mswada wangu. Kwa hivi kitabu kilichapishwa huku Marekani, na wanaokisoma ni wa-Marekani, kuanzia katika jamii hadi vyuoni, kama nilivyoelezea hapa na  hapa.

Masimulizi ni mengi, na kama nilivyogusia, labda nitafute wasaa miaka ijayo niandike kumbukumbu zangu za historia ya kitabu hiki.

Saturday, March 21, 2015

Leo Nimehojiwa na "African Global Roots"

Nimerejea mchana huu kutoka Minneapolis, kwenye mahojiano na African Global Roots (AGR). Wiki mbili hivi zilizopita, Ndugu Petros Haile, mkurugenzi wa AGR alikuwa ameniomba tufanye mahojiano hayo.

Ndugu Haile nami tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Nimewahi kushiriki katika program zake kwa kupeleka vitabu vyangu. Vile vile, alivyovyofahamu kuwa nimepeleka wanafunzi Tanzania kwenye kozi ya Hemingway, aliniomba niandike makala, ambayo aliichapisha.

Kwa mahojiano ya leo, Ndugu Haile alitaka tuongelee kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho alishakisoma miaka iliyopita. Alitamani, kwa kutumia mawasiliano ya AGR kusambaza ujumbe katika jamii ya wa-Afrika hapa Marekani na ulimwenguni na kwa watu wengine, kuhusu umuhimu wa kuyaelewa masuala ninayoongelea katika kitabu changu.

Kwa kuwa nilijua kuwa Ndugu Haile alitaka kunihoji kuhusu dhughuli zangu za kuelimisha umma, nilichukua pia nakala ya kitabu changu cha Matengo Folktales, ambacho ni ushahidi wa namna ninavyojitahidi kujifunza kutokana na masimulizi ya jadi ya mababu na mabibi zetu wa Afrika, na namna ninavyotumia hazina hii kuuelimisha ulimwengu kuhusu mchango wa wahenga wetu katika dunia.

Mahojiano yalikuwa mazuri. Ndugu Haile alitunga masuali muhimu kutokana na yaliyomo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na pia aliniuliza masuali kuhusu utafiti wangu ulioniwezesha kuandika kitabu cha Matengo Folktales.

 Mahojiano haya tumefanyia katika kituo cha Afric Tempo, kinachomilikiwa na Ndugu Malick wa Senegal. Leo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika mahali hapo, ambapo pana mgahawa, stoo, na studio ya kurekodia programu za televisheni.

Sitaandika zaidi kwa leo. Nangojea hadi mahojiano yatakapopatikana mtandaoni, ndipo niwaeleze walimwengu. Inafurahisha sana kuweza kukutana na kushirikiana na watu kama Malick na Petros, wenye kupenda kujitolea kwa hali na mali ili kujenga maelewano katika jamii. Jambo moja tuliloongelea leo na kukubaliana ni kuwa tunaamini kuwa Mungu ametuweka duniani kwa madhumuni kama hayo.


Tuesday, December 25, 2012

Milima Haikutani

Wa-Swahili husema, milima haikutani bali binadamu hukutana. Hayo yalinipata mjini Karatu mwaka 2008 nilipokutana na mzee ambaye anaonekana nami pichani.

Siku hiyo ilikuwa siku ya mnada mjini Karatu, siku ambayo hutokea mara moja kwa mwezi. Katika umati mkubwa wa watu, yeye na mimi tulijikuta uso kwa uso. Yeye alinitambua mara moja, akauliza: "Profesa Mbele?" Nilimwambia ndio mimi. Tulifurahi sana, tukaanza michapo.

Mzee huyu nilimfahamu mwaka 1996 wakati nafanya utafiti wa masimulizi ya jadi kuhusu shujaa wa wa-Iraqw aitwaye Saygilo Magena. Utafiti huu ulinipeleka kwenye miji na vijijini kama vile Mbulu, Mamaisara, na Karatu.

Kati ya watu walionisaidia sana ni huyu mzee ambaye jina lake ni John Qamlali. Baada ya kufahamiana kule Mbulu, tulikutana tena mjini Arusha, tukaongea sana. Anajua sana habari za wa-Iraqw na ameshawasaidia watafiti wengine wa mataifa mbali mbali. Ninazo kanda za maongezi yetu.

Kukutana tena mwaka 2008, miaka zaidi ya kumi tangu tulipokutana mara ya kwanza, ilikuwa ni ajabu na pia jambo la kushukuru.

Tuesday, May 31, 2011

Safari ya Bajaji: Lushoto Hadi Irente

Agosti 6, mwaka jana, nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Irente. Nilishawahi kusafiri hadi Irente miaka michache kabla, nikitumia teksi. Lakini mwaka jana niligundua kuwa ningeweza kusafiri kwa bajaji. Bajaji yenyewe ndio hii inayoonekana katika picha, na dreva wake. Bajai hii ilikuwa maarufu mjini Lushoto.

Niliziona bajaji kwa mara ya kwanza nilipokuwa India, mwezi Aprili mwaka 1991. Wakati huo hapakuwa na bajaji Tanzania. Lakini kidogo kidogo, miaka iliyofuatia, bajaji zilianza kuonekana, na leo zimejaa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Sasa zinaonekana hata kwenye miji midogo kama Lushoto. Ndio mambo ya ulimwengu katika utandawazi wa leo.

Safari ilikuwa murua. Bajaji ilikula milima na kukwepa mifereji na mashimo kama mchezo. Tulipofika Irente, nilianza kuwatafuta vijana wawili mapacha ambao niliwafahamu miaka iliyotangulia, wakati nafanya utafiti kuhusu masimulizi juu ya Osale Otango na Paulo Hamisi. Osale Otango na Paulo Hamisi ni maarufu katika historia ya miaka ya hamsini na kitu, walipokuwa wakisakwa na serikali ya wa-Ingereza kwa ujambazi. Walikuwa wakizunguka na kujificha maeneo hayo ya Irente.

Kwa bahati nzuri siku hiyo, hao mapacha walikuwa kijiji cha jirani wakati bajaji yangu ilipofika hapo. Tulifurahi kukutana, tukapandisha njia hadi nyumbani kwao.

Nilipiga picha hii wakati tunateremka kutoka kanisani. Hao marafiki zangu wametangulia. Bajaji ilikuwa imepaki kwenye nyumba zinazoonekana kule ng'ambo. Upande wa kulia, kule ukingoni, ndipo penye mwamba ambapo watalii na wageni wengine hufika kuangalia mandhari ya sehemu hizo na sehemu za mbali. Panaitwa Irente Viewpoint. Kuna picha nyingi za mahali hapo mtandaoni. Ni mahali maarufu kiasi kwamba kama hujafika hapo, inakuwa kama vile hujafika Lushoto.

Hapa ninaonekana nikiwa na hao marafiki zangu mapacha. Kule nyuma yetu ni miamba ambayo nayo imepigwa picha sana na watalii na wageni wanaofika hapa Irente. Kuna miteremko ya kutisha maeneo hayo. Hata mimi ambaye natoka sehemu za milimani, Umatengo, kwenye milima na miteremko, ninatishika na miteremko ya Irente.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...