Wa-Swahili husema, milima haikutani bali binadamu hukutana. Hayo yalinipata mjini Karatu mwaka 2008 nilipokutana na mzee ambaye anaonekana nami pichani.
Siku hiyo ilikuwa siku ya mnada mjini Karatu, siku ambayo hutokea mara moja kwa mwezi. Katika umati mkubwa wa watu, yeye na mimi tulijikuta uso kwa uso. Yeye alinitambua mara moja, akauliza: "Profesa Mbele?" Nilimwambia ndio mimi. Tulifurahi sana, tukaanza michapo.
Mzee huyu nilimfahamu mwaka 1996 wakati nafanya utafiti wa masimulizi ya jadi kuhusu shujaa wa wa-Iraqw aitwaye Saygilo Magena. Utafiti huu ulinipeleka kwenye miji na vijijini kama vile Mbulu, Mamaisara, na Karatu.
Kati ya watu walionisaidia sana ni huyu mzee ambaye jina lake ni John Qamlali. Baada ya kufahamiana kule Mbulu, tulikutana tena mjini Arusha, tukaongea sana. Anajua sana habari za wa-Iraqw na ameshawasaidia watafiti wengine wa mataifa mbali mbali. Ninazo kanda za maongezi yetu.
Kukutana tena mwaka 2008, miaka zaidi ya kumi tangu tulipokutana mara ya kwanza, ilikuwa ni ajabu na pia jambo la kushukuru.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
Naam Profesa Mbele. Nionavyo mimi, kuna maprofesa wenye shahada zinazotambulika, mathalani hiyo ya kwako, na wapo maprofesa ambao hawana vyeti lakini wana maarifa mengi na adimu kwenye vichwa vyao. Nadhani Mzee huyu anaingia kwenye kundi hilo la pili. Hivyo, hapo mlikutana maprofesa wawili. Hongera sana kwa habari hii.
Ndugu Simba Deo, shukrani kwa ujumbe. Mimi nilitambua miaka mingi sana iliyopita kwamba kupata digrii au madigirii vyuo vikuu haimaanishi kuwa mtu unajua kila kitu.
Baada ya kugundua hilo, msimamo wangu umekuwa kwamba mtu ana ujuzi au elimu fulani ambayo sina. Kila mtu anaweza kunifundisha kitu.
Mimi ni mtafiti, na katika utafiti wangu wa masimulizi ya jadi, lugha, na utamaduni, nimekuwa nikiwatafuta wazee vijijini na mijini, na hata vijana pia. Wao nawahesabu kama waalimu wangu.
Nimefanya utafiti sehemu za vijijini kama vile Ukerewe, Bariadi, Mbulu, Shinyanga, na mwambao wa Kenya. Nimefundishwa mengi na wazee, na baadhi ya hao wazee hawajasoma shuleni.
Watafiti maarufu wa masomo kama yangu utawakuta wamefanya utafiti kwa wazee hao ninaosemea, na ndio chanzo cha hao watafiti kuandika vitabu na makala nzito na kuwa maarufu.
Mimi mwenyewe nimeshafanya mahojiano na wazee kama Haji Gora Haji wa Zanzibar, ambaye hakwenda shule zaidi ya madrasa ya kiIslam alipokuwa mdogo. Lakini ni bingwa wa hali ya juu katika masuala ya fasihi, lugha na utamaduni wa Visiwani.
Au tuje pale Chuo Kikuu Dar es Salaam. Kwa miaka mingi alikuwepo pale Mzee Pera Ridhiwani (marehemu sasa) akinukuu miswada ya zamani ya kiSwahili, ambayo imo katika hati ya kiArabu. Nilizoeana na mzee huyu, akanisaidia sana. Ingawa hakusoma chuo kikuu chochote, ni bingwa katika fani zake kiasi ambacho sijakutana na profesa mwenye madigirii ambaye anamfikia.
Ningeweza kuendelea kuandika sana, kwani nimekutana na wazee wengi mno katika mikoa mbali mbali ya Tanzania na pia, kama ninavyosema, mwambao wa Kenya. Maprofesa wa vyuoni tunaponea kwao.
Siwezi kukudanganya, kama nina umaarufu wowote katika taaluma zangu, wazee hao wamechangia kwa kiasi kikubwa. Ni lazima kuwaenzi na kuwashukuru.
Ndio maana mimi huwa nachukizwa sana na tabia ya baadhi ya watu kujivunia usomi au madigirii. Kwa mtazamo wangu, mbwembwe hizo ni dalili ya kutoelimika.
Naam. Nakubaliana nawe Profesa. Pengine ingefaa kuanzisha utafiti kuhusu watu/wazee wa aina hii hasa katika eneo letu la Afrika ya Mashariki. Kwa kueleza maisha na michango ya watu kama hawa katika benki jumla ya ujuzi wa watu, huenda itatusaidia kuelewa kwamba elimu ni zaidi sana ya vyeti -- elimu ni hasa namna gani mtu anatumia maarifa aliyo nayo kuleta mabadiliko chanya katika harakati za mtu kuyamiliki mazingira yake.
Pengine, mpango huo utatusaidia kuthamini watu kwa vile walivyo na si kwa nini hasa wanacho.
Nakupongeza sana kwa jitihada unazofanya kuleta mabadiliko chanya katika maisha yetu.
Asante
Hongera Sana Simba Deo kwa maoni yako! Elimu iliyobora zaidi Ni ile ya mtu kujitambua,na kuweza kuyamiliki mazingira yake,na kuweza kuishi vyema na binadamu wenzake!Wazee wetu wengi waliishi hapa duniani na kufa,bila ya kutuachia sehemu kubwa ya hazina ya ujuzi walionao.
Kuna sababu mbalimbali zilizochangia Hali hiyo kutokea,ikiwa Ni Pamoja na mwingiliano wa tamaduni za wageni,hasa Wazungu.Kimsingi,Wazungu walichangia kwa kiwango kikubwa kudororesha uwezo wetu wa asili,na hivyo tukawa tegemezi kwao.(Indigenous knowledge).
Hata hivyo,ukifuatilia Sana,hasa katika nchi zilizoendelea,wenzetu hao wanawatambua Sana wenzao waliofanya makubwa,na huwa wanawatunuku shahada za heshima,kinyume na huku kwetu!
Nini kifanyike kwa sasa? Wataalamu wetu wa Sasa wazishawishi mamlaka zilizopo zianze kuwatambua Hawa Wazee wetu wenye taaluma za Hali za juu,ili waenziwe ipasavyo.Pia wataalamu wetu wa kisasa watusaidie kuandaa namna Bora ya kuandaa data base ya kila mmoja wa Hawa wataalamu wetu wa jadi,ili wasiondoke na taaluma zao.Pia kuwepo na hati miliki ya ujuzi wa kila mmoja wao.
Post a Comment