Leo napenda kuongelea habari ya simba wa Tsavo. Ni habari iliyokuwa inatusisimua sana tulipokuwa shuleni, baina ya darasa la tano na la nane.
Kulikuwa na kitabu, Simba wa Tsavo, ambacho kilichapishwa mwaka 1966. Ni tafsiri ya kitabu cha J.H. Patterson kilichoitwa The Man Eaters of Tsavo.
Kitabu hiki kilielezea matukio ya kutisha wakati ujenzi wa daraja la reli kwenye mto Tsavo, nchini Kenya, miaka mia na kitu iliyopita. Kilielezea namna simba walivyokuwa wakiwavizia, kuwadaka na kuwaua wafanya kazi kwenye eneo la hili daraja wakawaua watu zaidi ya mia, hadi, hatimaye, Patterson alipofanikiwa kuwaua, mwezi Desemba 1898. Hiyo ndio habari tuliyosoma tukiwa shuleni, miaka hiyo ya sitini na kitu.
Lakini, kwa miaka hii ya karibuni, yapata miaka kumi, nimekutana na taarifa nyingine nyingi kuhusu simba wa Tsavo. Je, unajua wale simba waliishia wapi?
Katika kusoma habari za mwandishi Ernest Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 eneo la jirani na Chicago, nimegundua kuwa alipokuwa mtoto alipelekwa na baba yake katika hifadhi ya Field Museum of Natural History mjini Chicago. Hapo alipata kuziona maiti za wanyama mbali mbali kutoka Afrika ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kitaalam ili zionekane kama vile ni wanyama hai.
Kati ya wanyama hao ni wale simba wa Tsavo, ambao picha yao inaonekana hapa juu. Habari hii ilinishtua sana, kwani sikujua kabisa kuwa simba wa Tsavo wamehifadhiwa na kwamba wako Chicago. Hiyo ni faida ya wazi ya kusoma vitabu, kwamba mtu unagundua mambo ambayo hukuyajua.
Pamoja na kuangalia wanyama hao waliohifadhiwa, mtoto Hemingway alisoma kitabu cha The Man Eaters of Tsavo. Hayo yote yalichangia katika kumjengea Hemingway mapenzi makubwa aliyokuwa nayo juu ya Afrika kwa maisha yake yote.
Mwaka 1933, Hemingway na mke wake Pauline walifunga safari wakitokea Ulaya, wakaja Afrika Mashariki. Walishuka meli Mombasa, wakapanda treni kuelekea Nairobi. Walipita Tsavo, wakaenda hadi Machakos, kisha Tanganyika. Kuhusu safari yake ya Tanganyika, Hemingway aliandika kitabu maarufu kiitwacho Green Hills of Africa, ambacho ni kimoja ya vitabu vyake ambavyo nimevisoma na kuwafundisha wanafunzi.
Saturday, December 8, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Kweli kusoma vitabu kuna faida sana na kama wengi wangeiga mfano wako basi mengi wangeyafahamu. Ahsante kwa kutokuwa mchoyo was habari hii
Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe. Kuna mengi yanayosikitisha. Kwa mfano, nimemtaja huyu mwandishi Hemingway. Aliishi na kutembelea sehemu nyingi hapa duniani, kama vile Hispania, u-Faransa, Cuba na kwake Marekani.
Wenzetu sehemu kama Cuba wamehifadhi nyumba yake vizuri kabisa, na hata baa alipokuwa anakunywa ulabu imehifadhiwa. Na vyote hivyo ni vivutio vikubwa vya utalii. U-Faransa na Hispania ni hivyo hivyo. Sehemu alizoishi hapa Marekani ni hivyo hivyo, kama vile nyumba zake za Oak Park (karibu na Chicago), Key West (Florida), na kadhalika.
Sisi Bongo ni wazembe wa kutupwa. Hemingway alitembelea sehemu nyingi za nchi yetu, akaandika juu yake. Lakini kwa vile hakuna utamaduni wa kusoma vitabu, hatujui. Tungeweza na sisi kuvutia watalii wengi sana iwapo tungesoma na kugundua sehemu hizo na kuzitangaza. Lakini sisi ni sifuri kabisa, tena zile sifuri tulizokuwa tunachorewa na walimu shule ya msingi, zikiwa na masikio. Ndio sifuri zetu hizo.
Kwa masikitiko na hamu ya kuona tunabadilika, nimeandika haya katika insha mojawapo katika kitabu changu cha CHANGAMOTO. Insha hiyo inaitwa "Vitabu na Utalii."
Lakini baada ya kuandika, nilikumbuka kuwa nimekosea stepu, kwani kwa kuandika kitabu, huwezi kuwafikia wa-Bongo. Hawatakisoma.
Tungeweza hata kufunguka macho kwa kuangalia yaliyotokea Botswana, baada ya mwandishi Alexander McCall Smith kuandika kitabu kiitwacho "The No. 1 Ladies' Detective Agency."
Kitabu hiki kimepata umaarufu wa ajabu, sehemu kama huku Marekani, na karibu kila mtu anayeongelea uandishi wa kiAfrika atakutajia. Kitabu kimetengenezwa filamu yake, ambayo nayo ni kivutio kikubwa. Kutokana na hayo, Botswana imepanda chati katika uwanja wa utalii.
Lakini sisi Bongo ni uvivu, majungu, ushirikina, na wabunge kuchapa usingizi wakati wa vikao. Yaani Bongo tambarare kweli :-)
Post a Comment