Tuesday, December 4, 2012

Nimekutana na Kobina Aidoo

Siku chache zilizopita, Kobina Aidoo kutoka Ghana alitembelea hapa Chuoni St Olaf kutoa mhadhara kama sehemu ya maazimisho ya Africa Weeks. Maazimisho hayo huandaliwa kila mwaka na jumuia ya wanafunzi iitwayo Karibu.

Sikuwa nimesikia jina la Kobina Aidoo, ila nilihudhuria mhadhara wake. Ni kijana mwenye kipaji anayeinukia katika nyanja za filamu na uanaharakati katika kuelimisha jamii.

Aliongelea suala la nani ni mw-Amerika Mweusi, akaleta changamoto nyingi zinazowakabili watu weusi wanaoishi hapa Marekani katika kujitambua na kujitambulisha. Baada ya kusema machache, alituonyesha DVD yake ambayo imajaa kauli na mitazamo ya watu weusi wanaoishi Marekani, wakiwa wametokea nchi mbali mbali za Afrika na bara la Marekani.

Ni mitazamo inayofikirisha na kuchangamsha akili. Inatupanua mawazo kuhusu utata wa suala hilo la nani ni m-Marekani Mweusi, na kwa ambaye hakufahamu, inashtua kuona migogoro baina ya waMarekani weusi wa asili na watu weusi ambao ni wahamiaji wa miaka ya karibuni nchini Marekani.

Katika picha hapo juu ninaonekana na Kobina, baada ya mhadhara wake. Tulipiga picha hii mara baada ya mimi kumkabidhi nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambayo anaonekana ameishika, na yeye akawa amenikabidhi nakala ya DVD yake.

7 comments:

Unknown said...

Nimevutiwa na jina la jumuiya iliyoandaa kongamano. Hilo jina ''Karibu'' nihili letu la kiswahili?

Mbele said...

Ndugu Ado Shaibu, shukrani kwa kutembelea hiki kijiwe changu na kuacha ujumbe. Hiki chuo ni cha wazungu, kwa maana kwamba wanaosoma na kufundisha hapa kwa ujumla ni wazungu. Kwa miaka yangu ya mwanzo 18 ya kufundisha hapa, profesa mw-Afrika nilikuwa mimi tu.

Kuna wanafunzi wachache kutoka Afrika, labda yapata 10. Miaka kama 10 iliyopita, msichana mmoja kutoka Kongo mashariki, ambaye familia yake walikuja hapa Minnesota kama wakimbizi, alijiunga kusoma katika chuo hiki.

Haikupita muda akaja na wazo la kuanzisha hiki kikundi aichokiita Karibu. Msichana huyu, kwa vile ni wa Kongo mashariki, ambako wanazungumza ki-Swahili, alichagua jina la Karibu akimaanisha kuwa ni kikundi cha kuwaleta watu pamoja. Ni jina zuri.

Lengo lilikuwa kuwaunganisha wa-Afrika na wapenzi wa Afrika, na wengine katika kuelimishana kuhusu utamaduni, siasa, na mambo mengine ya Afrika. Baadhi ya shughuli wanazofanya ni ngoma, maonesho ya mavazi, mihadhara, na filamu.

Kikundi hiki kilipata umaarufu tangu mwanzo hapa chuoni. Kinaelimisha na kuleta burdani za aina aina, hasa wakati huu wa Africa Weeks.

Kati ya faida zake ni kuwa wanafunzi wa ki-Marekani wanaokwenda Afrika kwa masomo hupenda kujihusisha na kikundi hicho, kabla ya kwenda Afrika au baada ya kurudi. Ni njia moja ya kuendeleza yale waliyoyaona na kujifunza Afrika.

Mara kwa mara kikundi cha Karibu kimenialika kuelezea utamaduni wa Afrika, kama vile kusimulia hadithi za Afrika na kuwashirikisha wasikilzaji katika kuzichambua. Mimi ni mtafiti na mwandishi katika taaluma hiyo, na daima niko tayari kutoa mchango wa aina hiyo.

Unknown said...

Nafurahi kusikia hivyo Prof.Mbele. Naunga mkono kila jitihada huko ughaibuni kuhusu kutangaza fahari ya Afrika.
Pia kuhusu mjadala wa nani ni Mmarekani Mweusi,mimi huwachukulia raia wote wa Marekani ambao wana asili ya Afrika(weusi) kuwa ndiyo Wamarekani Weusi. Sikuwahi kusikia wala kudhani hata siku moja kwamba kunaweza kuwepo mgawanyiko na ubaguzi baina ya wale walioenda Marekani zama za kale kupitia utumwa na wale walioenda miaka ya karibuni kama wahamiaji.

Mbele said...

Ndugu Ado, mahusiano baina ya wale weusi ambao wahenga wao walikuja kama watumwa na hao wa-Swahili waliofika miaka ya baadaye kutoka Afrika ni uhusiano wenye mengi.

Wa-Afrika wengi wanakuja na mawazo ya kujiona wao ni bora zaidi, mawazo ya kuwaona wa-Marekani weusi kuwa ni wavivu na wafujo, kadhalika. Na hao wa-Marekani weusi wengi wanayo mawazo potofu kuhusu wa-Swahili hao, kwamba wa-Swahili hao hawajastaarabika, kwamba wana maringo ya kijinga, na kwamba ni mbumbumbu wasiofahamu masuala ya ubaguzi Marekani, kwamba hawana shukrani kwa wa-Marekani weusi ambao walipambana na ubaguzi hadi kuikisha nchi katika hali ambayo wa-Swahili hao wameikuta na wanafaidi fursa zilizotokana na mapambano hayo.

Halafu kuna wa-Marekani weusi ambao wanaona aibu kuwa na asili ya ki-Afrika, kwa vile wameaminishwa kuwa Afrika ni bara la ovyo, dhiki, njaa, na magonjwa. Kwa hivi hawataki hata kuwazia kuwa walitoka huko, na wakimwona mw-Afrika wanaona "ni wale wale."

Hata hivi, kuna wa-Marekani weusi ambao wanajivunia asili yao ya u-Afrika, na utawakuta wanafanya kila juhudi kuifahamu zaidi Afrika, kutembelea Afrika, kujenga urafiki na wa-Afrika, na kadhalika. Utawakuta wanavaa mavazi ya ki-Afrika, au wamejipa majina ya ki-Afrika na wanajivunia, na majina hayo saa nyingine huwa ni ya ajabu kwetu wa-Swahili, lakini wao kwa vile hawazijui vizuri lugha zetu, wanadhani ni majina sahihi.

Na kuna pia wa-Swahili ambao wanafika hapa Marekani wakiwa wamejielimisha kiasi kuhusu historia ya nchi hii, na wanafahamu angalau kiasi mchango na harakati za wa-Marekani weusi. Waswahili hao wana tabia ya kuheshimu historia hiyo na sio kuwabeza wa-Marekani weusi, ambao ninafahamu kuwa wa-Bongo tunawaita pia wa-Nyamwezi.

Kuna maandishi mengi yaliyochapishwa kuhusu masuala hayo, na watafiti kama vile wanasoshiolojia, na kuna hata riwaya na tamthilia. Kwa mfano, tamthilia iitwayo "Dilemma of a Ghost," iliyoandikwa na mama Ama Ata Aidoo wa Ghana, inaelezea vizuri sana suala hilo.

Nimefurahi umegusia suala hilo, na nakumbuka niliandika kijimakala kwenye blogu yangu ya kiIngereza, ambacho unaweza kukisoma hapa.

Unknown said...

Nashukuru Professa kwa ufafanuzi wako. Nitajibidiisha kujifunza mengi uhusu eneo hili. Nitafurahi pia kujifunza kwa jicho la kifasihi. Nitajaribu kukitafuta ''Dilema of a Ghost'' kwenye maduka yetu ya vitabu. Nilikiona kwenye orodha ya vitabu vya kujibia somo la Literature in English kwa ngazi ya kidato cha nne. Lakini kuna changamoto fulani katika hili. Unaweza kutafuta vitabu kama Girls at War, Tales of Amadou Koumba, Sundiata kwenye maduka yetu ya vitabu usivipate. Cha kushangaza, vimo kwenye orodha ya vitabu vya kujibia somo la Literature in English

Anonymous said...

naomba nukunukuu professa hapo"unasema lakini wao kwavile hawazijui vizuri lughazetu,wanadhani ni majina sahihi" miminaona wanafanya vizuri hata kama hawajui lugha yetu vizuri kwani wao wanataka wajione kweli ni waafrika maana hata mimi huwa sielewi vizuri jina lako Mbele ila kwavile ni jina la kiafrika bado nalu nijinazuri maana haya Mbele lakini kikwenu natumai lina maana iliyo nzuri na inaeleweka hivyo hayo majina wanayoyataka nayo ni mazuri tu kwani hata majina ya kizungu mengine ukifsiriwa yanakuwa yana maana ya kawaida

Mbele said...

Ndugu Anonymous, umetoa mchango mzuri kwa kukumbushia changamoto na utata wa suala hilo la majina. Hata watafiti nao wamekuwa wakitafakari suala hilo na kuna makala zimechapishwa na zinaendelea kuchapishwa.

Kwa mfano kipengele kimojawapo kinachowashughulisha watafiti ni misingi inayotumiwa na jamii mbali mbali katika kuwapa watu majina. Katika tamaduni mbali mbali tunashuhudia jinsi wanavyofanya, na misingi yake. Ni somo pana.

Tukirudi kwetu sisi tuliozipokea dini za wageni, kama vile u-Islam na u-Kristo, inabidi tujiulize inakuwaje m-Matengo kuitwa Joseph au m-Zaramo kuitwa Abubakar. Je, majina ya ki-Kristo ni lazima yawe ya wazungu na wa-Yahudi? Na je, majina ya ki-Islam ni lazima yawe ya wa-Arabu?

Mada hii ya majina ni nzuri, yenye utajiri, na nashukuru kwa mchango wako.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...