Monday, December 17, 2012
Hongera JWTZ Kwa Kufungua Maktaba
Nimevutiwa sana na taarifa juzi kuwa Rais Kikwete, Amiri Jeshi wa Tanzania, amefungua maktaba ya kisasa kwenye chuo cha mafunzo cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Monduli. Ni habari njema kabisa.
Mimi ni mdau mkubwa wa maktaba na katika blogu hii ninaziongelea mara kwa mara. Mifano ni maktaba za Tanga, Dar es Salaam, Songea, Lushoto, Moshi, Iringa, na Southdale.
Kwa miaka mingi sijawahi kusikia rais au kiongozi mwingine wa kitaifa Tanzania akifungua maktaba, ukiachilia mbali tarehe 9 Desemba, 1967, ambapo Mwalimu Nyerere alifungua Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam.
Pita katika maktaba yoyote Tanzania, utaona kuwa maktaba ni kitu ambacho wa-Tanzania hawakithamini sana, isipokuwa labda wanafunzi. Na hao wanafunzi wanaonekana maktabani endapo wamebanwa sana na mwalimu au wanakabiliwa na mitihani.
Wakaazi wa Tanga, kwa mfano, wamekuwa na bahati ya kuwa na maktaba tangu mwaka 1958, kabla ya Uhuru. Ingebidi wawe juu kabisa kitaifa kwenye suala la elimu. Lakini wapi, ukiingia katika maktaba ile, hutawaona. Je, unadhani kuwa ukimwuliza mkaazi wa Arusha au Songea akuonyeshe maktaba iko wapi, ataweza kukuambia? Jaribu uone.
Tanzania tumezoea kusikia kuhusu ufunguzi wa baa, sio maktaba. Kama unafungua baa maarufu, unaweza kabisa kumleta waziri akawa mgeni rasmi. Kutokana na utamaduni huo, kitendo cha JWTZ cha kufungua maktaba ya kisasa ni cha pekee. Ni kitendo kinacholeta matumaini kuwa labda tutashtuka na kuelewa umuhimu wa maktaba. Natoa pongezi kwa JWTZ.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment