Monday, December 28, 2015

Kitabu Juu ya Charles Dickens

Siku chache zilizopita, niliingia katika gereji yangu ambayo imefurika vitabu. Katika kufukua fukua, nilikiona kitabu Dickens, kilichotungwa na Peter Ackroyd. Sikumbuki nilikinunua lini na wapi, ila niliamua kukichukua, kwa lengo la kukipitia angalau juu juu. Nina vitabu kadhaa vilivyotungwa na Dickens. Baadhi nimevisoma na baadhi sijavisoma.

Dickens ni kati ya waandishi ambao watu wa rika langu tuliwasoma miaka ya ujana wetu Tanzania, tukawapenda sana. Kutokana na mvuto huu, nimeandika juu ya Dickens mara kadhaa katika blogu hii. Mifano ni hapa, na hapa. Kwa hivyo, nilivyokigundua kitabu cha Dickens katika gereji,  nilifurahi, nikakichukua hima.

Nilikuwa nafahamu jina la mwandishi Peter Ackroyd, ingawa sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu chake chochote. Katika kupitia taarifa kwenye jalada la kitabu chake cha Dickens, nimeona orodha ya vitabu alivyoandika na umaarufu wake. Kwa mfano, amejijengea heshima kubwa kwa kuandika vitabu vya historia na wasifu wa waandishi kama William Shakespeare na William Blake .

Kitabu cha Dickens ni wasifu wa Dickens, maelezo kuhusu maisha yake na maandishi yake, pamoja na maelezo kuhusu jamii alimoishi na kuandika. Ni kitabu kilichosheheni uchambuzi wa maandishi ya Dickens, sambamba na uchambuzi wa uhusiano baina ya maandishi hayo na jamii. Ni matunda ya utafiti wa kina na mpana. Dickens ni hazina kubwa, kitabu chenye kurasa 1195.

Nimekuwa nikikipitia kwa mshangao juu ya juhudi na umakini uliotumika katika utafiti na uandishi wake. Ninafahamu kuwa wenzetu wa nchi kama za Ulaya na Marekani wana jadi ya kufanya utafiti wa kina na kuandika kwa umakini kuhusu waandishi wao maarufu. Kwa mfano, kuna vitabu vya aina hiyo juu ya William Shakespeare, Johann Wolfgang von Goethe, Henrik Ibsen, Leo Tolstoy, Mark Twain, Ernest Hemingway, na William Faulkner.

Tukijifananisha na hao wenzetu, sisi wa-Tanzania tumefanya utafiti gani na tumeandika nini juu ya waandishi wetu maarufu kama Mgeni bin Faqihi na Shaaban Robert? Hakuna chochote ambacho tumefanya kinachoweza kufananishwa na majuzuu makubwa aliyoandika Michael Reynolds juu ya Ernest Hemingway, achilia mbali majuzuu waliyoandika wengine juu ya huyu huyu Charles Dickens. Labda, kwa kutafakari hayo tutagundua na kukiri kuwa tuna njia ndefu mbele yetu.

No comments: