Sunday, April 28, 2013

Hatimaye, Nimeonana na Mzee Patrick Hemingway

Nimerejea jioni kutoka Montana, ambako nilikwenda jana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtu maarufu sana. Ni yeye pekee ndiye bado hai kati ya watoto wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway.

Mwandishi Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 jirani na Chicago na kufariki 1961, ni maarufu duniani kote. Kwa miaka yapata kumi, nimevutiwa na jinsi alivyoandika kuhusu Afrika, kutokana na kutembelea na kuishi Afrika Mashariki, mwaka 1933-34, na mwaka 1953-54. Ninasoma na kufundisha maandishi ya Hemingway, kama nilivyoandika hapa, na hapa.

Kwa muda mrefu nilitaka niwasiliane na Mzee Patrick Hemingway, ambaye ni mtoto pekee wa Hemingway aliyebaki. Nilifahamu kuwa aliishi Tanzania miaka yapata 25. Moja ya shughuli alizofanya ni kufundisha katika chuo cha Mweka. Nilisoma sana maandishi yake na kusikiliza mazungumzo yake ambayo yako mtandaoni.

Nilijua kuwa huyu ni hazina kubwa kwa yeyote anayefuatilia maandishi na maisha ya Ernest Hemingway. Siku moja, miaka yapata miwili iliyopita, nilijipa moyo nikampigia simu. Nilifurahi jinsi alivyonifanyia ukarimu, tukaongea sana. Kuanzia hapo, nimeongea naye mara kwa mara.

Hatimaye, jana nilisafiri hadi Montana, ambako tumepata fursa ya kuongea kwa masaa mengi, jana na leo. Nimefurahi kwa namna ambayo siwezi hata kuelezea. Nategemea kuandika taarifa mbali mbali za ziara hii siku zijazo.

7 comments:

Anonymous said...

Nilidhani umekutana na mwandishi mwenyewe. Taaluma hairithishwi hivyo umechemsha na kutafuta sifa tu mkuu.

Mbele said...

Anonymous wa 30 April, 2013, 6:53, unajifanya unajua taratibu za taaluma, lakini napata picha wewe ni mbabaishaji.

Kwanza, ingekuwa vema iwapo ungejitambulisha ufahamike. Kwenye masuala ya taaluma ndivyo tunavyofanya.

Hayo uliyosema yanathibitisha kuwa wewe huna hata chembe ya ufahamu wa hiki unachoongelea. Mzee Patrick Hemingway anaheshimika duniani kwa maandishi yake yanayohusu uandishi wa baba yake. Ameandika utangulizi katika vitabu mbali mbali vya Ernest Hemingway na hivi kuwapa walimwengu mwanga kuhusu mambo mengi.

Patrick Hemingway amehariri maandishi mengi ya Ernest Hemingway, na pia ndio mmiliki wa urithi wote wa Ernest Hemingway, anayeratibu machapisho na matumizi na mapato yatokanayo na kazi za Ernest Hemingway.

Kila mtafiti anayehusika na masuala ya Ernest Hemingway anatambua kuwa Patrick Hemingway ni mtu wa pekee, mtu pekee aliyebaki, anayejua mengi yasiyojulikana kwa walimwengu.

Kwa msingi huo, fursa niliyopata ya kuwasiliana na Patrick Hemingway na kisha kukutana naye, ni bahati kubwa kwangu. Wewe anonymous zingatia hilo.

Mimi ni mtafiti. Kazi yangu ni kutafuta elimu muda wote. Ujinga ni kama ugonjwa. Natafuta elimu sawa na mgonjwa anayetafuta matibabu. Hii dhana yako kwamba natafuta sifa naiona ni ya mtu asiyeelewa maana ya elimu na taaluma.

Halafu, umethibitisha kuwa wewe ni kilaza wa kutupwa, pale unaposema kuwa ulidhani nimekutana na mwandishi mwenyewe. Huyu mwandishi Ernest Hemingway alishakufa miaka mingi iliyopita. Ningekutana naye vipi wakati huu?

Hata kwenye hii taarifa yangu fupi, nimesema kabisa kuwa Ernest Hemingway alishafariki.

Kati yako anonymous na mimi, ni nani aliyechemsha?

Anonymous said...

Prof achana nao hao, wajuaji wasiojijua. Ungekutana vipi na mwandishi mwenyewe wakati alishakufa zamani?

Hongera sana kwa juhudi zako usivunjwe moyo na watu ambao hata kukamata kalamu wakaandika abstract tu hawawezi.

Makengo said...

Binafsi naamini huyo jamaa hajui maana ya kukutana na mtu kama huyu, mtu ambaye kazi za baba yake na zakwake unazipenda. Binafsi nafahamu, nimekuwa nikisoma machapisho yako mbalimbali kwa muda mfupi tu, na nilitamani kuonana na wewe. Wakati mmoja nilifanikiwa kukuona ukiw ababati-manyara, nilifurahi sana na kutamani kuongea na wewe, lakini sikufanya hivyo kwani bado sikuwa tayari. Kwa hiyo nafahamu namna inavyokuwa unapotaka kukutana na mtu ambaye unamkubwali na unayethamini kazi zake. Watanzania wengi hatuthamni kazi za watu

mudhihiri njonjolo said...

Waswahili twasema 'mwana wa mhunzi asiposana huvuvia'.Heko Prof.

Mbele said...

Ndugu mudhihiri njonjolo,
Shukrani kwa kutembelea hapakwetu na kuweka ujumbe. Nakukaribisha wakati wowote, na nakutakia kila la heri.

mudhihiri njonjolo said...

Nimekaribia Prof,maarifa kiu yangu.
Sinong'onezwe na hofu,ibashiriyo uchungu.
Hino kazi ashirafu,impendezayo Mungu.
Matundaye maarufu,jaza mafungu mafungu.

Mudhihiri Njonjolo.
Mtwara-Mjini.