Juzi nilileta ujumbe kuwa nimepata fursa ya kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye bado hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Kwangu kama mtafiti na mwalimu, tukio hili ni la kukumbukwa daima. Hapa napenda tu kuongelea mipango ya safari ilivyokuwa.
Nilipokuwa Tanzania mwezi Januari na wanafunzi nikiwafundisha kozi kuhusu Ernest Hemingway, niliwaambia wanafunzi kuwa mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway nina mawasiliano naye kwa simu, na kwamba ni mzee wa miaka 85. Niliwaambia pia kuwa ninapangia kwenda kuonana naye. Mwanafunzi mmoja ambaye amekuwa akirekodi kozi yangu na habari zinazohusika alisema atapenda tutanguzane kwenye hiyo safari. Mwanafunzi mwingine alisema kuwa ana hakika kuwa baba yake atatupeleka kwa ndege yake.
Baada ya kurejea Marekani, tuliendelea na mipango yetu. Niliwasiliana kwa karibu na Mzee Hemingway na huyu kijana wa mwenye ndege aliwasiliana na baba yake, tukakubaliana tufanye safari tarehe 27 wikiendi iliyopita.
Mzee mwenye ndege alikuja kutoka kwao Ohio na rubani wake, nasi tukajumuika nao katika uwanja mdogo wa Lakeville, inavyoonekana pichani kushoto. Kulia kabisa ni mzee mwenye ndege. Kijana wake ni huyu aliyevaa kaptula. Kijana huyu na huyu mwenzake mrefu kabisa ndio wale walifika Tanzania kwenye kozi yangu.
Mzee huyu ni msomi na msomaji wa vitabu. Ni msomaji makini wa mwandishi Hemingway. Wakati nilipokuwa nafundisha kozi yangu kule Tanzania, alitafuta silabasi kutoka chuoni kwangu akafuatilia kozi nzima.
Mzee Hemingway alikuwa ametushauri tukatue uwanja wa Great Falls, Montana. Safari ilichukua yapata masaa matatu, baada ya kutua kwenye mji wa Bismarck, Dakota ya Kaskazini, kwa ajili ya kupata mafuta ya ndege. Hali ya hewa ilikuwa nzuri njia nzima.
Baada ya kufika Great Falls, tulichukua gari tukaenda kwenye mji mdogo wa Craig, ambako Mzee Hemingway alisema angekuwepo.
Tulipata msisimko mkubwa tulipomwona anatungoja nje ya nyumba yake. Nilimwomba hapo hapo tupige picha, kabla hatujaingia ndani kwa mazungumzo, ambayo nitaelezea baadaye. Nimeandika ujumbe huu kwa lengo la kujitunzia kumbukumbu. Mengine ya msingi, yale tuliyojifunza kutoka kwa Mzee Hemingway, yatakuja siku za usoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment