Nilienda na wanafunzi wawili, ambao walikuwa miongoni mwa wanafunzi niliowapeleka Tanzania mwezi Januari mwaka huu, kwa kozi niliyoiita "Hemingway in East Africa." Katika msafara wetu, alikuwepo pia baba mzazi wa mwanafunzi mmojawapo, ambaye alitupa usafiri wa ndege yake, na rubani wake.
Katika picha hapa kushoto, tunaonekana wote, na mwenyeji wetu, Mzee Patrick Hemingway na mkewe Carol, wakati wa chakula cha jioni. Kutoka kulia kwenda kushoto hapo mezani ni mwanafunzi Jimmy, Mzee Patrick Hemingway, Bwana Cooper (mwenye ndege), rubani, mwanafunzi Clay, Mama Carol, na mimi.
Tulienda kupata chakula cha jioni siku tuliyowasili Montana, yaani tarehe 27. Ilikuwa ni baada ya masaa kadhaa ya kuongea na Mzee Patrick Hemingway, akajibu masuali yangu kuhusu baba yake Ernest Hemingway na maandishi yake yahusuyo Afrika. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya mimi kuandaa safari hii ya kwenda kumwona.
Mazungumzo yetu yalikuwa marefu, na ilifikia wakati niliona nihitimishe, ili kutomchosha sana Mzee wetu. Lakini Mzee Hemingway ni mwongeaji sana. Pamoja na uzee wake, ana kumbukumbu nzuri sana ya mambo na anapenda kusimulia michapo ya miaka ile ya zamani, ikiwemo ile inayomhususu Ernest Hemingway.
Ziara yetu ilikuwa ya mafanikio makubwa sana. Sote tunakubaliana hivyo, akiwemo Mzee Patrick Hemingway mwenyewe, kama alivyonieleza leo kwenye simu. Leo nimepata barua kutoka kwa mzee mwenye ndege, na kati ya mambo aliyoandika ni "It was a truly remarkable, memorable, and thought provoking weekend."
No comments:
Post a Comment