Walimu Tunduru walia na mazingira duni ya kazi
CHANZO: Blogu ya Maendeleo ni Vita
MAZINGIRA duni ya
kufanyia kazi yaliyopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma yanatajwa kuwa ni
miongoni mwa sababu zinazosababisha wilaya hiyo kuwa duni katika elimu ya
msingi na sekondari.
Hayo yamesemwa na
baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo katika mahojiano
maalum ya kutambua kwanini wilaya hiyo inakuwa ya mwisho kitaaluma katika
wilaya zote za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea vijijini,Songea manispaa,Nyasa,Mbinga,Namtumbo
na Tunduru.
Teresphol Ngonyani ni
mwalimu wa sekondari ya Frankweston anazitaja sababu za wilaya hiyo kuwa ya
mwisho kuwa ni pamoja na maslahi duni ya walimu wanaoishi na kufanya kazi
katika mazingira magumu kama ya wilaya ya Tunduru hivyo walimu wamepoteza moyo
wa kufanyakazi.
“Kama moyo wa mwalimu
umekufa kufanyakazi hata serikali ingeleta wakaguzi kumi kila siku mwalimu
hawezi kutoa elimu bora badala yake atatoa bora elimu na matokeo yake ndo
tumeanza kuyaona kwa kuwa madhara ya walimu kugoma hayaonekani kwa urahisi kama
ilivyo kwa madaktari kwa kuwa watu watakufa lakini walimu sasa wanatengeneza
taifa la wajinga jambo ambalo ni hatari sana’’,alisisitiza.
Neema Mwakila mwalimu
wa sekondari Frankweston aliitaja sababu
nyingine ambazo inaifanya wilaya ya Tunduru kuwa ya mwisho kitaaluma ni idadi
kubwa ya wanafunzi kusomea katika chumba kimoja cha darasa ambapo hivi sasa
kuna shule chumba kimoja kinakuwa na wanafunzi karibu 100 hali ambayo
inasababisha ugumu katika tendo la ufundishaji na kujifunza.
Ally Chilowa mwalimu
kutoka shule ya sekondari Mgomba anasema kutokana na mazingira duni ya kusomea
yamesababisha wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari baadhi yao hupokelewa
wakiwa hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu na kwamba wanafunzi wengi wanaosoma
wana matatizo makubwa ya kusoma,kuandika na kuhesabu.
Edmund Ndunguru
anasema mitihani yote ambayo inafanywa hivi sasa kuanzia shule za msingi na
sekondari ni ya kiini macho kwa kuwa wizara inashusha wastani na kuonekana
mambo ya kisiasa kwa kuwa wanafunzi
wanaofanya vibaya wanaongezewa alama ili waonekane wamepata alama nzuri,lakini
katika hali halisi katika shule za msingi utafiti ukifanyika kuna idadi kubwa
ya wanafunzi ambao hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu.
“Walimu kuanzia shule
za msingi na sekondari katika nchi nzima nina uhakika wataalamu wangekwenda
kufanya utafiti kwa kila darasa watakuta idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajui
kusoma,kuandika na kuhesabu hali hiyo inatokana na walimu kufa moyo wa
kufundisha kwa kuwa serikali imeshindwa
kumjali mwalimu kuanzia nyumba
wanazoishi na maslahi yao’’,alisema mwalimu Teresphol Ngonyani.
Mwalimu wa shule ya
msingi Mbarikiwa kata ya Ligunga tarafa ya Matemanga Ally Rashid kutokana na
ubovu wa nyumba anayoishi ambayo inaweza kuanguka wakati wowote ameamua
kuandika kwenye mlango “tatizo namba moja
ni nyumba’’ hivyo serikali inatakiwa kushughulikia matatizo hayo kabla bomu
la elimu halijalipuka anasema mwalimu huyo.
Terephol Ngonyani
mwalimu wa sekondari ya FrankWeston ametaka serikali iache utani na walimu kwa
kuhakikisha inatekeleza madai yote ya
walimu ambayo yanachangia kushusha kwa elimu.
Mwalimu Ally Chilowa anasema Serikali ijitahidi kuboresha maisha ya wananchi wake ili waweze
kusomesha watoto wao hasa katika wilaya ya Tunduru ambayo wakazi wake wengi ni
masikini wanashindwa hata kulipa ada na michango mbalimbali inayotakiwa
shuleni.
Mwalimu Edmund
Ndunguru anaishauri serikali iboreshe mfumo mzima wa ajira ya mwalimu, ili mwalimu
awe na mwajiri mmoja badala ya hali ambayo ipo hivi sasa mwalimu anawaajiri
zaidi ya watatu, anadai kuwa mwalimu ndiyo mtumishi wa umma ambaye ana hali
mbaya ya maisha matokeo yake mwalimu anadharaulika katika jamii kutokana na
maisha duni yanayosababisha kuwa na madeni mengi
“Mwalimu anayemlipa
mshahara ni mwajiri mwingine,anayefanya naye mkataba wa kazi ni mwajiri
mwingine na anayefuatilia utendaji kazi wake ni mwajiri mwingine,hivyo mfumo
mzima wa elimu ufanyiwe marekebisho ili kufikia malengo ya millennia ambayo
yanategemea sana elimu bora kwa watu wote’’,alisema.
Mwalimu Ally Chilowa
anasema serikali inahusika moja kwa moja
na kutoa fungu la pekee kwa
walimu wanaoshi katika mazingira magumu ikiwemo wilaya ya Tunduru kwa kuwa
waliahidi kutoa fungu ili walimu walimu wanaoishi katika mazingira magumu waweze
kuishi maisha bora ambayo yatasababisha walimu kutoa elimu bora.
Kaimu Afisa elimu
wilayani Tunduru Flavian Nchimbi amekiri miundombinu hafifu ya vyumba vya
madarasa,nyumba za walimu na madawati ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia
kuporomoka kwa elimu katika wilaya hiyo.
Hata hivyo mkuu wa
wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amekiri mazingira duni katika wilaya hiyo
yanachangia elimu duni na kwamba hivi sasa serikali inajitahidi kuboresha
mazingira bora ya kufundishia kuanzia ujenzi wa vyumba vya madarasa,nyumba za
walimu na kuongeza idadi ya walimu.
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru ina jumla ya shule za msingi 145
kati ya hizo shule za serikali ni 144 na shule moja ni ya shirika la kidini
ambapo shule za sekondari katika wilaya nzima zipo 23 kati ya hizo shule 21 ni
za serikali na mbili ni seminari za shirika la kidini.
albano.midelo@gmail.com
1 comment:
Kabla hatujaenda mbali, naomba nikumbushie kuwa hii Tunduru inayozungumziwa ina utajiri wa madini ya mbali mbali, ambayo hao wanaoitwa wawekezaji wanafaidika nayo, wakati wenyeji wa Tunduru wanasota hata walimu wanakosa nyumba.
Kuhusu utajiri wa Tunduru katika madini, kuna taarifa nyingi mtandaoni, kwa mfano soma hapa.
Post a Comment