Thursday, April 4, 2013

Mhadhara Katika Darasa la Wazee

Leo nilitoa mhadhara katika darasa la wazee, hapa Northfield. Somo wanalosomea ni "Folk and Fairy Tales."

 Hapa Northfield kuna masomo ambayo wazee husoma, yanayoendeshwa na taasisi iitwayo Cannon Valley Elder Collegium. Nimewahi kufundisha mara tatu darasa la wazee katika mfumo huo, na somo langu lilikuwa "The African Experience." Tulisoma na kujadili kitabu cha Things Fall Apart cha Chinua Achebe kama msingi wa kuongelea hali ya Afrika kabla na baada ya ukoloni, na hali ya leo ya ukoloni mamboleo.

 Nilivyoingia tu darasani leo, nilifurahi kuwaona wazee ambao walishasoma somo langu. Walikuwa yapata nusu ya darasa la leo.

 Nilichangia mawazo kuhusu somo hili la hadithi za fasihi simulizi, nikasimulia hadithi mbili za ki-Matengo ili kuthibitisha na kufafanua yale niliyosema kinadharia. Hadithi nilizosimulia ni "The Monster in the Rice Field" na "Nokamboka and the Baby Monster," ambazo zimo katika kitabu changu cha Matengo Folktales.

Tulikuwa na mazungumzo marefu, kuanzia saa saba na nusu mchana hadi saa tisa. Ilipendeza sana kuwaona wazee hao wakiimba nami wimbo wa ki-Matengo uliomo katika hadithi ya "The Monster in the Rice Field," wimbo unaorudiwa tena na tena. Ilivutia sana, na sote tulifurahi, tukazama katika kuichambua hadithi hii na ile ya "Nokamboka," ambazo zote zimejaa falsafa na masuali kuhusu maisha.

No comments: