Thursday, June 11, 2015

Kesi ya Raif Badawi: Mwanablogu wa Saudi Arabia

Raif Badawi ni mwanablogu wa Saudi Arabia ambaye anafahamika sana duniani kutokana na kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na viboko 1000. Alihukumiwa kwa kile kilichoitwa kuitukana dini ya u-Islam. Amekaa gerezani miaka miwili na tayari alishapigwa viboko 50 nje ya msikiti mjini Jeddah. Adhabu hiyo si nyepesi; inaweza kusababisha kifo.

Watu wengi duniani wanalaani hukumu hiyo. Wengi hawaoni ni kwa vipi Raif Badawi ameutukana u-Islam. Wengi wamechukizwa na hukumu hiyo kwa kuwa ni hujuma dhidi ya uhuru wa kutoa mawazo.

 Mawazo ya Raif Badawi yaliyosababisha hukumu dhidi yake ni ya kawaida sana kwa vigezo vyetu wa-Tanzania na wengine duniani. Lakini wahusika nchini Saudi Arabia wameendelea kusisitiza kuwa Raif Badawi anastahili hukumu hiyo. Kuna tetesi kuwa huenda akashtakiwa upya ili apewe hukumu kali zaidi, kukatwa kichwa, hukumu ambayo hutekelezwa sana Saudi Arabia.

Kesi ya Raif Badawi imeibua masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia. Kuna mengi yanayoongelewa. Kwa mfano, ni marufuku Saudi Arabia kutoa mawazo yanayopingana na yale ya watawala na viongozi wa dini. Ni marufuku kwa watu wasio wa-Islam kujenga nyumba za ibada zao, kama vile makanisa, katika ardhi ya Saudi Arabia. Ni marufuku kuhubiri dini tofauti na u-Islam. Ni marufuku kwa wanawake kuendesha gari. Ni marufuku kwa wanawake kusafiri bila kibali cha mume au ndugu wa kiume.

Kuna kampeni kubwa sehemu mbali mbali duniani kulaani hukumu dhidi ya Raif Badawi. Sisi wanablogu wa Tanzania tunasimama wapi? Ni vema kukumbushana kuwa ukiona mwenzako ananyolewa, wewe tia maji.

5 comments:

Marko Mwipopo said...

Je, mheshimiwa profesa Mbele, hivi inajulikana wazi alitukanaje dini ya u-islamu? Maana naona kama adhabu ni kubwa mno. Tena ni mtu anayeishi ndani ya nchi yake kiasi kwamba hajainyooshea kidole nchi ya ugenini. Na kwa wastani ni kama anapigwa viboko visivyopungua viwili ndani ya muda wa siku 3. Inasikitisha sana. Hapa kuna mawili: Nchi kama Saud Arabia wanaona kama hawajatenda kosa kutoa adhabu hiyo sababu sheria zao zinatokana na msaafu, ambao kimsingi ndio unawakingia kifua. Maana hata kanisani au msikitini, kasisi au shekhe akisema kitu katika mahubiri utamsikiliza tu sababu dini haijadiliwi kwa bahati mbaya. Lakini jambo la pili ni lile linalotofautiana kidogo katika baadhi ya nchi zingine. Jambo hili ni ukiukwaji wa mambo yaliyoainishwa katika katiba za nchi husika. Mfano, askari anaweza kukupiga ukaumia hadi ukafa, na saa zingine asifanywe kitu. Kuna wakati pia hata viongozi wakuu wa nchi wamenukuliwa wakisema wananchi "wapigwe tu". Hizi zote ni shida kubwa sana duniani.

Nikirejea kwa huyo bwana wa Saudi Arabia, nadhani kuna haja ya kutia saini au namna fulani ya watu wa dunia nzima kuoneshwa na kutokukubaliana na kitendo cha serikali hiyo ya nchi yake.

Mbele said...

Ndugu Marko Mwipopo,

Shukrani kwa ujumbe wako. Ukipitia linki niliyoleta yenye nukuu kutoka kwenye blogu ya Raif Badawi, utaona kama ukosoaji wake na masuali yake ni matusi dhidi ya u-Islamu au la. Baadhi ya maandishi yake yametafsiriwa kwa ki-Jerumani na kuchapishwa kitabu. Bahati mbaya wengi hatujui ki-Jerumani. Lakini ukisoma taarifa mbali mbali, utaona kuwa uhuru wa kutoa mawazo umefinywa sana nchini Saudi Arabia, kwa kiwango ambacho si cha kawaida.

Ingawa hakuna nchi duniani yenye uhuru kamili, kila wakati kunakuwa na nchi ambayo inaonekana imevuka mpaka na inakemewa na walimwengu kwa ujumla. Mifano iko mingi. Kuna wakati dunia, pamoja na mapungufu yake, ilikuwa inamkemea Adolf Hitler. Kuna wakati dunia, pamoja na mapungufu yake, ilikuwa inaukekemea ukaburu wa Afrika Kusini. Upepo wa dunia unavuma kuelekea kwa yule ambaye anaonekana kuongoza kwa ubaya. Leo, hukumu dhidi ya mwanablogu Raif Badawi inaushtua ulimwengu na upepo unaelekea Saudi Arabia.

Binafsi, daima nimekuwa mtetezi wa uhuru wa waandishi. Kwa mfano, wakati serikali ya Tanzania ilipokipiga marufuku kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai, nilipinga hatua hii ya serikali, nikawa natetea haki na uhuru wa Hamza Njozi kufanya utafiti na kuandika kama alivyoandika. Nilisema kwamba kama serikali haikupendezwa na ailyoandika, iandike kitabu kuelezea mtazamo na fikra zake. Kama polisi hawakupenda alichoandika Njozi, waandike kitabu chao. Kama yeyote mwingine hakuridhishwa au alichukizwa na kitabu cha Njozi, aandike kitabu chake.

Ukisoma kitabu alichoandika Njozi baada ya hicho cha Mwembechai, utaona amenitaja na kunishukuru kwa kutetea haki yake ya kuandika. Ndio msimamo wangu juu ya huyu mwanablogu Raif Badawi, sawa na nilivyopinga na ninaendelelea kupinga kufungiwa kwa gazeti la "Mwanahalisi" nchini Tanzania.

Mfuko said...

Mzee Mbele Tanzania pia juzijuzi Raisi katia saini sheria mpya inayoitwa sheria ya makosa ya mtandao, imelalamikia na wadau mbali mbali wa mitandao kama wamiliki wa blogs,kwa kutoshirikishwa vyakutosha kwenye utengenezwaji wa sheria hiyo kwa kutoa mawazo yao,hivyo inaonekana ni sheria yenye manufaa Zaidi kwa serikali kuliko wananchi.

Mbele said...

Ndugu Mfuko,

Shukrani kwa kukumbushia suala hilo.

SELF HELP BOOKS PUBLISHERS LTD said...

Nchi zinazoshikilia sharia kali za dini mfano wa Saudiarabia, zinajidanganya tu na ni jambo la wakati tu, waitazame Ulaya au tuseme nchi za Magharibi, karne nyingi zilizopita mambo yalikuwa hivyo hivyo, wanafikra huru na wagunduzi kama kina Gallileo, Copernicus na wengineo walifanyiwa hivyo hivyo na watawala wa kidini, maandiko yao kupigwa marufuku kabisa na hata wengine kuuwawa. Lakini polepole kadiri binadamu walivyozidi kupanuka uelewa na kwa kuwa binadamu ni kiumbe chenye kuutafuta ukweli na uhuru daima pasipokujali unamuwekea vikwazo kiasi gani sasa hivi wahanga walewale waliopigwa marufuku na kuuwawa fikra zao ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kisasa na wala hazipingani na dini kama ilivyokuwa imedhaniwa na watawala wa wakati huo. Hivyo Badawi na wengi ambao leo hii wanauwawa kutokana na fikra zao huru, na wala siyo kuitusi dini kama wanavyosingiziwa miaka kadhaa ijayo watakuja kukumbukwa kishujaa kama kina Galileo wanavyokumbukwa leo hii.