
Leo, baada ya wiki nyingi kidogo, nimeona nirejee tena kwenye mada ambayo nimekuwa nikiiandikia tena na tena
katika blogu hii. Ni juu ya vitabu ninavyojipatia, iwe ni kwa kununua, au kwa namna nyingine.
Leo asubuhi, kama kawaida, nilienda
chuoni St. Olaf kufundisha. Nilipoingia katika jengo la maktaba, ambamo pia ni makao ya idara yangu ya ki-Ingereza, nilipita kwenye meza ambapo huwekwa vitabu na makabrasha kwa ajili ya yeyote anayehitaji. Niliona meza imejaa vitabu kuliko siku nyingine yoyote iliyopita, nikaamua kuviangalia.
Niliona kuwa vyote vilikuwa vitabu vya taaluma, hasa masuala ya wanawake na jinsia. Niliamua kujichukulia vitatu, baada ya kuangalia ndani na kuona maelezo ya vitabu hivi. Kitabu kimojawapo ni
Sex & Power, kilichotungwa na Susan Estrich. Niliona maelezo kuwa mwandishi alikuwa profesa wa sheria katika
Chuo Kikuu cha Harvard na baadaye profesa wa sheria katika
Chuo Kikuu cha California ya Kusini. Ameandika vitabu kadhaa na makala mbali mbali. Alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa
Harvard Law Review. Huenda msomaji wa taarifa hii utakumbuka kuwa hiki ni cheo ambacho Barack Obama aliwahi kushika. Kutokana na mada ya kitabu, na orodha ya sura zake niliona kuwa kitabu hiki kitanielimisha sana kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii.
Kitabu cha pili kilichonivutia kwa namna ya pekee ni
Globalization: The Making of World Society, ambacho kimetungwa na Frank J. Lechner. Kama tunavyofahamu, mada ya utandawazi inavuma sana miongoni mwa wanataaluma, wanasiasa, na jamii kwa ujumla. Hata hivi, mitazamo kuhusu nini maana ya utandawazi, chimbuko lake, faida na hasara zake, ni masuala ambayo yanajadiliwa na yamegubikwa na utata.
Mimi mwenyewe, kwa miaka kadhaa, nimetafakari suala la utandawazi, nikilihusisha na tofauti za tamaduni. Nimewahi hata kuendesha warsha kadhaa, nchini Tanzania, katika miji ya
Arusha, Dar es Salaam, na
Tanga. Kwa hivi, nilipokiona kitabu cha
Globalization: The Making of World Society, nilikuwa na hamu ya kukisoma. Hiki kitaongeza idadi ya
vitabu vyangu kuhusu utandawazi.
Kitabu cha tatu,
Behind the Veil in Arabia: Women in Oman, kilichoandikwa na Unni Wikan, kilinivutia pengine zaidi ya hivi vingine. Nilipoona jina la kitabu hiki, nilikumbuka mara majina ya vitabu vingine, kama vile
Beyond the Veil, cha Fatima Mernissi wa Morocco. Suala la wanawake katika nchi za ki-Arabu limeshika nafasi ya pekee kichwani mwangu kutokana na kozi niliyoanzisha na ninaifundisha,
"Muslim Women Writers."
Simaanishi, na mtu asidhani, kwamba wa-Arabu wote ni wa-Islam, bali kuna suala la jinsi utamaduni unavyoingiliana na dini kiasi kwamba pamoja na tofauti za dini, kuna mambo kama mila, desturi, na lugha, ambayo yanawaungamisha wa-Arabu.
Katika kufundisha kozi ya
"Muslim Women Writers" imedhihirika kuwa vazi kama hijab ni suala la utamaduni zaidi kuliko dini.
Qur'an inasema wanawake wajisitiri na wainamishe macho, lakini haisemi wavae nini. Hili ni suala la kila utamaduni, na ndio maana mavazi ya wanawake wa ki-Islam katika tamaduni mbali mbali yanahitilafiana.
Maktaba yangu imetajirika leo kwa kuongezewa vitabu hivi muhimu. Ni raha iliyoje kujipatia hazina kubwa namna hii bila gharama yoyote kwa upande wangu.