Saturday, February 11, 2017

Ninamwazia Mwandishi Alexander Pushkin

Kwa wiki yapata mbili, nimekuwa nikimwazia sana Alexander Pushkin, mwandishi maarufu wa u-Rusi. Nimefahamu tangu ujana wangu kuwa wa-Rusi wanamwenzi kama baba wa fasihi ya u-Rusi. Miaka ya baadaye, nilikuja kufahamu kuwa Pushkin alikuwa na asili ya Afrika, na kwamba hata katika baadhi ya maandishi yake aliongelea suala hilo.

Nilisoma makala za profesa moja wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, nikafahamu zaidi suala hilo. Katika kufuatilia zaidi, niliguswa na mengi, hasa maelezo juu ya kipaji cha Pushkin cha ajabu katika matumizi ya lugha ya ki-Rusi na ubunifu wake, na pia jinsi alivyokufa. Aliuawa katika ugomvi akiwa na umri wa miaka 37 tu.


Siku kadhaa zilizopita, nilitoa mhadhara katika darasa la Nu Skool, kuhusu umuhimu wa Afrika na wa-Afrika katika historia ya ulimwengu. Kati ya watu maarufu wenye asili ya Afrika ambao niliwataja kwa mchango wao ni Antar bin Shaddad wa Saudi Arabia na Pushkin. Antar bin Shaddad ni mshairi aliyeishi kabla ya Mtume Muhammad, na ambaye tungo zake zinakumbukwa kama hazina isiyo kifani katika lugha ya ki-Arabu. Pushkin ni hivyo hivyo; wa-Rusi wanakiri kuwa umahiri wake katika kuimudu lugha yao hauna mfano.

Kutokana na hayo nimekuwa na hamu ya kumsoma Pushkin, nikakumbuka kuwa nilishanunua kitabu chake maarufu, Eugene Onegin, ambayo ni hadithi iliyoandikwa kishairi. Ninajiandaa kuisoma.

2 comments:

Maundu Mwingizi said...

Nitamsaka huyu. Ahsante kwa kumtambulisha kwangu.

Mbele said...

Ndugu Maundu Mwingizi

Nimeanza kusoma hiyo tafsiri ya Douglas Hofstadter ya "Eugene Onegin," na ninaona ni chemsha bongo, sio tu kwa upande wa lugha bali pia kwa jinsi inavyogusia mambo mengi, kama vile ya fasihi na falsafa. Kipaji cha Pushkin cha kuandika kwa ubunifu kinadhihirika katika tafsiri hii. Jambo moja ambalo tayari nimeshajiamulia ni kusoma tafsiri za wengine za "Eugene Onegin." Ninaamini kuwa kwa kusoma tafsiri mbali mbali, nitafaidi zaidi ladha ya "Eugene Onegin."