Friday, February 3, 2017

Miaka 50 ya Azimio la Arusha

Tarehe 5 Februari, mwaka huu, itakuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 50 tangu "Azimio la Arusha" litangazwe, tarehe 5 Februari, 1967. Watu wa rika langu na wale wa umri mkubwa zaidi wanakumbuka jinsi "Azimio la Arusha" lilivyotangazwa na kupokelewa nchini. Wanakumbuka msisimko wa furaha na matumaini ulioigubika nchi kutokana na Azimio hilo.

Azma ya kuondoa unyonyaji, kuweka njia kuu za uchumi katika mikono ya wakulima na wafanyakazi, kujenga usawa, kuhakikisha kila mtu mwenye uwezo anafanya kazi na anapata malipo halali ya kazi yake, na kujenga nchi yenye kujitegemea, yote hayo yaliisisimua nchi nzima.

"Azimio la Arusha" lilielezea kuwa tumekosea kwa imani yetu kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo. Lilitufundisha kuwa msingi wa maendeleo ni watu wenyewe, sio pesa. Na huo ni ukweli hata katika mazingira ya leo. Msingi wa maendeleo ni watu kutumia nguvu yao, akili, maarifa, ubunifu, na uthubutu, bila kutetereka. Maendeleo yanatokana na watu, ni maamuzi ya watu wenyewe, kujipangia malengo, wala hayaletwi kutoka nje.

Leo wa-Tanzania wamepotea njia. Wanaamini kuwa serikali itawaletea maendeleo, au rais atawaletea maendeleo. Wanaamini kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo. Wakati wa serikali ya awamu ya nne, palikuwa na mpango ulioitwa "mabilioni ya Kikwete" ambao ulikuwa ni mpango wa kuwagawia watu pesa za miradi. Vile vile, katika kampeni za urais za mwaka 2015, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli, aliahidi kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Imani imejengeka kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo.

Lakini, kwa kuzingatia kuwa watu ndio msingi wa maendeleo, "Azimio la Arusha" lilituelekeza katika kutambua umuhimu wa kuwekeza katika watu, kwa njia ya elimu, maarifa, uhuru wa kutoa mawazo, na demokrasia. Huu ulihesabiwa kama msingi muhimu wa maendeleo. Maendeleo yanategemea watu walioelimika, wenye kufikiri, kuhoji mambo, na kutoa mawazo. Kwa ajili hiyo, "Azimio la Arusha" lilifuatiwa na matamko mengine, yaliyofafanua dhana hizi, kama vile "Elimu ya Kujitegemea."

Kwa maneno mengine "Azimio la Arusha" liliona mbali likaweka msingi ambao leo unawafanya watu makini ulimwenguni waongelee kile kinachoitwa "knowledge economy" kwa ki-Ingereza. Wa-Tanzania hatuna habari hiyo; tunasubiri mabilioni ya Kikwete au milioni 50 za Magufuli.

Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa "Azimio la Arusha," hakuchoka kuendelea kufafanua maana na malengo ya "Azimio la Arusha." Kwa mfano, dhana ya kuwa msingi na lengo la maendeleo ni watu aliifafanua katika kitabu cha "Binadamu na Maendeleo." Dhana ya demokrasia iliendelea kufafanuliwa katika "Mwongozo wa TANU," ambao ulisisitiza kuwa uongozi si unyapara. Kiongozi alitakiwa awe sambamba na watu katika kujadili masuala na kutoa maamuzi.

Hayo yote ni ishara ya namna Mwalimu Nyerere alivyojali dhana ya kwamba watu ndio msingi wa maendeleo. Ninaposema hivi, ninakumbuka jinsi dhana hii inavyofanana na ile ya Mao Tse-tung, ambayo kwa ki-Ingereza ilitafsiriwa kama "mass line," na pia ninakumbuka dhana ya Kim il Sung iliyoitwa "the juche idea."

Kuna mengi ya kutafakari juu ya "Azimio la Arusha." Kwa mtazamo wangu, ukiachilia mbali kupatikana kwa Uhuru na Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, hakuna jambo jingine la muhimu lililowahi kutokea katika miaka yetu hii kama "Azimio la Arusha." Uhuru, Muungano, na "Azimio la Arusha" ndio mambo muhimu kuliko yote.

Kwa hivyo, haipendezi kushuhudia namna siku hizi za kuelekea siku ya kumbukumbu ya miaka 50 ya "Azimio la Arusha" zinavyopita kama vile ni siku za kawaida tu. Ilitakiwa kuwe na msisimko mkubwa nchi nzima kwa mikutano, warsha, na hotuba za kutathmini nafasi na maana ya "Azimio la Arusha" katika Taifa letu na ulimwenguni.

No comments: