Monday, January 30, 2017

Kitabu Nilichonunua Leo: "The Highly Paid Expert"

Leo nilikwenda Minneapolis na wakati wa kurudi, nilipita Mall of America, kuangalia vitabu katika duka la Barnes & Noble. Nilitaka hasa kuona kama kuna vitabu vipya juu ya mwandishi Ernest Hemingway.

Niliangalia scheme vinapowekwa vitabu vya fasihi, nikakuta kitabu kipya juu ya Ernest Hemingway, Everybody Behaves Badly: The Backstory to 'The Sun Also Rises.' kilichoandikwa na Lesley M.M. Blume. Kwa kuwa nimezama sana katika uandishi wa Hemingway, maisha na falsafa yake, na kwa kuwa nimeshasoma The Sun Also Rises, nilitamani kukinunua kitabu hiki, ambacho, kwa maelezo niliyoyaona, kinazungumzia yaliyo nyuma ya pazia.

Sikuwa na hela za kutosha, kwa hivyo nikaamua kuangalia vitabu vingine. Nilitumia muda zaidi katika sehemu ya "Business/Management." Huwa ninapenda sana kununua na kusoma vitabu vya taaluma hii, kwani vinanifundisha mengi kuhusu mambo ya ujasiriamali na biashara. Taaluma hii inanisaidia katika kuendesha shughuli za kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants.

Hatimaye, nilikiona kitabu kilichonivutia kwa namna ya pekee, The Highly Paid Expert, kilichoandikwa na Debbie Allen.  Kwa mujibu maelezo nyuma ya kitabu, huyu mwandishi ni mtaalam maarufu katika mambo ya biashara na ujasiriamali. Niliangalia ndani, nikaona mada anazoongelea ni za kuelimisha kabisa, kama vile matumizi ya tekinolojia za mawasiliano na mitandao.

Niliona anatoa ushauri wa kusisimua. Kwa mfano, anasema kuwa ni lazima mtu unayetaka mafanikio katika shughuli zako, uwasaidie wengine kufanikiwa. Unavyowasaidia wengine wafanikiwe, unajijengea mtandao wenye manufaa kwako pia. Ubinafsi na uchoyo wa maarifa haukuletei mafanikio. Kitabu hiki kinavutia kwa jinsi mwandishi anavyothibitisha mawazo yake, ambayo kijuu juu yanaonekana kama ya mtu anayeota ndoto.

Kwa bahati niliweza kuimudu gharama ya kitabu hiki, nikakinunua na kuondoka zangu, kwani nilikuwa sina hela iliyosalia. Sijutii kununua vitabu. Vitabu vinavyoelimisha ni mtaji, kwani hakuna mtaji muhimu zaidi ya elimu. Kwa wajasiriamali, wafanya biashara, watoa huduma, na kwa kila mtu, elimu ni tegemeo na nguzo muhimu. Ulazima wa kununua vitabu ni sawa na ilivyo lazima kwa mkulima kununua pembejeo.

No comments: