Saturday, January 14, 2017

Kitabu cha Uchambuzi wa "Hamlet"

Mwandishi maarufu Ernest Hemingway alisema, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Vyovyote unavyotaka kuitafsiri kauli hii ya Hemingway, ukweli ni kuwa kusoma kitabu kizuri ni mithili ya kuongea na rafiki wa kweli.

Baada ya kusoma Hamlet, kama nilivyoelezea katika blogu hii, nimeamua kusoma kitabu cha insha juu ya Hamlet, kinachoitwa Hamlet, ambacho kimehaririwa na Susanne L. Wofford. Ni kitabu cha insha ambazo zinaongelea nadharia za fasihi, na zinaichambua Hamlet kwa kutumia hizo nadharia tofauti.

Nadharia hizo ni "Feminist Criticism," "Psychoanalytic Criticism," "Deconstruction," "Marxist Criticism," na "The New Historicism." Lakini, pamoja na maelezo ya kina ya nadharia hizo, na uchambuzi mbali mbali wa Hamlet, kitabu hiki kina pia tamthilia yote ya Hamlet, toleo la The Riverside Shakespeare. Pia kitabu hiki kina maelezo ya maisha ya Shakespeare na mazingira ya kihistoria alimokulia, na historia ya uchambuzi wa tamthilia hiyo.

Ingawa nina vitabu vingine vya nadharia za fasihi, sio tu hizi zilizomo katika kitabu hiki, bali pia zingine, kama vile "Post-colonial criticism," "Structuralism," na "Post-structuralism," ninafurahia sana kusoma kitabu hiki. Kwa upande moja, ni muhimu kutambua kwamba hata kama unadhani unalifahamu jambo fulani katika taaluma, ni vizuri kuendelea kusoma mitazamo mbali mbali juu ya jambo hilo, au maelezo tofauti, kwani hata kama mtazamo ni ule ule, kila mwandishi ana namna yake ya kuuelezea.

Kwa hivyo, tukichukulia nadharia kama "Feminist Criticism" inavyoelezwa katika kitabu hiki, tunaona kuwa kuna misisitizo au mielekeo tofauti baina ya wachambuzi wa Marekani, Uingereza, na Ufaransa. Jambo hilo nilianza kulifahamu miaka ya 1980-86 nilipokuwa ninasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, hasa katika idara ya "Comparative Literature."

Ningetamani kuwa na ufahamu mkubwa wa ki-Swahili kiasi cha kuweza kuelezea kila kitu bila kutumia maneno ya ki-Ingereza. Dosari hii si jambo la kujivunia, nami sijasita kutamka hivyo katika blogu hii. Hata hivyo, ninavyofaidi kusoma vitabu vya ki-Ingereza, ninawasikitikia wale ambao hawajui lugha hii ambayo ndio lugha muhimu kuliko zote katika mawasiliano duniani.

No comments: