Monday, January 2, 2017

Mazungumzo na Wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus

Leo mchana nilikuwa Mount Olivet Conference & Retreat Center katika maongezi na wanafunzi wa chuo cha Gustavus Adolphus wanaokwenda Tanzania kimasomo. Profesa Barbara Zust, alikuwa amenialika, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Wanafunzi wengi wa programu hii wanasomea uuguzi, na lengo la kwenda Tanzania ni kujifunza namna masuala ya afya na matibabu yalivyo katika mazingira tofauti na ya Marekani, kwa maana ya utamaduni tofauti. Kwa lengo hilo, wanafunzi husoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Kwa hivyo, hiyo jana, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, niliwakuta wanafunzi wamesoma kitabu hiki na wamejizatiti kwa masuali ambayo yalinithibitishia kuwa ni wanafunzi makini wenye duku duku ya kujua mambo. Tulikuwa na mazungumzo ya kina yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili. Mwanafunzi mmoja, msichana, aliniambia kuwa yeye na mama yake walisoma kitabu changu pamoja. Taarifa hii imanigusa. Ni kama vile mzazi ametafuta namna ya kushiriki yale ambayo binti yake atayapitia atakapokuwa ugenini Tanzania.

Hiyo leo, nilipoanza kuongea na wanafunzi hao, niliwapongeza kwa uamuzi wao wa kwenda katika programu hii, ambayo itawapanua mtazamo na fikra, na hivyo kuwaandaa kukabiliana na dunia ya utandawazi wa leo. Baada ya mazungumzo yetu, tuliagana tukiwa tumefurahi, kama inavyoonekana pichani. Anayeonekana kulia kwangu kule nyuma kabisa ni Profesa Zust. Mbele yangu ni Mchungaji Todd Mattson.

Kwa taarifa zaidi kuhusu safari ya hao wanafunzi, fuatilia blogu yao With One Voice Tanzania

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...