Thursday, January 19, 2017

Nimejipatia Vitabu Vingine vya Bure

Jana niliandika katika blogu hii kuhusu vitabu nilivyovipata jana hiyo hiyo. Nilisema kuwa nilivipata hapa chuoni St. Olaf. Leo nilipita tena hapo, nikaviona vitabu vingi vya soshiolojia, na vichache vya taaluma zingine.

Nilichukua vitatu. Kimoja ni Who Speaks for Islam?: What a Billon Muslims Really Think, kilichoandikwa na John L. Esposito na Dalia Mogahed. Ni matokeo ya utafiti uliofanywa miongoni mwa wa-Islam kutoka nchi nyingi, ili kubaini mitazamo yao juu ya masuala kadhaa, kama vile mahusiano baina ya nchi za ki-Islamu na mataifa ya Magharibi, wanawake katika jamii za ki-Islam, na jihad.

Kitabu kingine ni Student Learning Abroad: What Our Students Are Learning, What They're Not And What We Can Do About It. kilichohaririwa na Michael Vande Berg, R. Michael Paige, and Kris Hemming Lou. Nimekisikia kitabu hiki kwa miaka miwili au mitatu, na nilitaka kukinunua. Imekuwa kama muujiza kuwa nimeiona nakala, nikajuchukulia. Kutokana na nilivyofahamu, kitabu hiki ni muhimu sana kwa watu kama mimi ambao tunajishughulisha na programu za kupeleka wanafunzi nchi za nje.

Katika vyuo vingi vya Marekani kuna programu za kupeleka wanafunzi nchi za nje kwa masomo ambayo huweza kuwa ya muda mfupi, kama mwezi moja, muda mrefu kiasi, kama miezi sita, na pia muda mrefu zaidi, kama mwaka moja. Fikra zilizopo ni kuwa fursa hizo huwapa wanafunzi upeo mpana wa ulimwengu na tamaduni tofauti, na kwa hivyo huwaandaa kuweza kuumudu ulimwengu ambao una mwingiliano mkubwa wa tamaduni.

Kitabu hiki chenye insha nyingi kinajadili mtazamo huo ili kuona kama una mashiko au la. Kwangu mimi ambaye daima nimeamini kuwa programu za kupeleka wanafunzi nchi za nje zina manufaa sana, kitabu hiki ninahisi kitanifungua macho nione mambo ambayo sikuyafahamu.

Kitabu cha tatu nilichojipatia ni riwaya, On the Hills of God, iliyotungwa na Ibrahim Fawal. Huyu ni m-Marekani mwenye asili ya Palestina, mzaliwa wa Ramallah. Sikuwa ninamfahamu, ila nimeona maelezo juu yake katika kitabu hiki. Ni msomi anayefundisha masomo ya filamu na fasihi. Hii ni riwaya ya kwanza ya mwandishi huyu, na inaanzia na tukio la kuporwa kwa ardhi ya wa-Palestina kulikofanywa na wa-Zionisti mwaka 1947, Kutokana na upekee wa suala la harakati za wa-Palestina, nitafanya juu chini niisome riwaya hii.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...