Sunday, January 22, 2017

Maandamano Makubwa Dhidi ya Rais Trump

Jana hapa Marekani yamefanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Donald Trump, ambaye aliapishwa juzi. Maandamano haya yaliyoandaliwa na kukusudiwa kwa wanawake, yanasemekana kuwa makubwa kuliko yote yaliyowahi kufanyika katika historia ya Marekani kwa siku moja. Maandamano haya yamefana sana, kwa mahudhurio na hotuba mbali mbali, na yametoa ujumbe wa wazi kuwa serikali ya Rais Trump isitegemee kuwa itatekeleza ajenda yake bila vipingamizi.

Marekani ni nchi inayoheshimu uhuru wa watu kujieleza. Katiba inalinda uhuru huo. Ndio maana maandamano ya kumpinga Rais Trump yalifanyika nchi nzima bila kipingamizi. Polisi walikuwepo kwa ajili ya kulinda amani, si kuzuia maandamano, wala kuwakamata wahutubiaji waliokuwa wanamrarua Rais Trump. Polisi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa waandamanaji wanayo mazingira muafaka na fursa kamili ya kutekeleza haki yao ya kuandamana na kuelezea mawazo yao.

Ninajua kuna wengine walioshiriki maandamano ya jana ambao si wa-Marekani. Kuna wakimbizi na wahamiaji kutoka nchi mbali mbali ambao walishiriki. Hapa Marekani, huhitaji kuwa raia ili kushiriki maandamano. Mimi sikushiriki, kwa sababu zangu binafsi.

Kwa kuwa mimi si raia wa Marekani, na sijawahi kuwazia kuwa raia, sioni kama nina haki au sababu ya kujihusisha na siasa za ndani za Marekani. Sipigi kura wakati wa uchaguzi wa viongozi. Kwa nini nijihusishe na maamuzi ya hao viongozi? Kama maamuzi yataiathiri nchi yangu, hapo nitaona nina wajibu wa kuisemea nchi yangu. Ninatambua wajibu wangu wa kuitetea nchi yangu popote nilipo.

Ingekuwa maandamano yanahusu masuala ya Tanzania ningeshiriki, kwa sababu Tanzania ni nchi yangu. Serikali ya Tanzania ikifanya mambo yasiyokubalika, halafu wa-Tanzania au marafiki wa Tanzania wakaandaa maandamano ya kupinga au kulaani, ni haki yangu kushiriki. Kule Uingereza, mwaka 2015, wa-Tanzania waliandamana kupinga mwenendo wa uchaguzi Zanzibar. Maandamano kama yale ni haki yangu kushiriki.

Huu utamaduni wa Marekani na nchi kama Uingereza unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Baada ya maandamano haya ya kihistoria ya jana dhidi yake, Rais Trump ametuma ujumbe: "Peaceful protests are a hallmark of our democracy. Even if I don't always agree, I recognize the rights of people to express their views." Tafsiri kwa ki-Swahili ni, "Maandamano ya upinzani ya amani ni kielelezo thabiti cha demokrasia yetu. Hata kama mara nyingine sikubaliani na wahusika, ninatambua haki ya watu kuelezea mawazo yao."

No comments: