Sunday, February 19, 2017

Utungo wa Pushkin, "Eugene Onegin," Ni Mtihani

Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nilikuwa ninajiandaa kusoma Eugene Onegin, utungo maarufu wa Alexander Pushkin. Nilianza hima, na sasa ninaendelea.

Nilifahamu tangu zamani kuwa Pushkin alikuwa ameandika tungo zingine pia. Nilifahamu kuwa Eugene Onegin ndio utungo wake maarufu kuliko zingine. Nilifahamu kuwa utungo huo ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kishairi.

Nilidhani kuwa ningesoma Eugene Onegin bila matatizo, kama ninavyosoma kazi za waandishi wengi. Baada ya kuanza kuusoma, na ninavyoendelea kusoma, ninajikuta kama vile niko katika mtihani. Eugene Onegin si rahisi kama nilivyodhani.

Pushkin ameusuka utungo wake kwa umahiri mkubwa, akitumia mbinu mbali mbali za kisanii, na pia taarifa za wasanii wa mataifa mbali mbali, kuanzia zama za kale, hadi zama zake. Humo kuna majina ya watunzi wa mataifa mbali mbali, kama vile Theocritus, Juvenal, Ovid, Racine, Chateaubriand, Lord Byron, pamoja na waandishi na waigizaji kadha wa kadha wa u-Rusi, wa wakati wa Pushkin na kabla yake, ambao hata mimi sikuwa ninawafahamu.

Kwa kufuatilia dondoo, dokezo, na maelezo yaliyomo, ninajifunza mambo mengi mapya. Mtindo huu wa Pushkin unanikumbusha ushairi wa Derek Walcott. Kusoma mashairi yake ni chemsha bongo. Unajikuta ukipelekwa sehemu nyingi katika historia, ikiwemo historia ya fasihi, sanaa, na falsafa.

Tafsiri ya Eugene Onegin ninayosoma ni ya Hofstadter. Katika kupambana na tafsiri yake, nimefikia uamuzi kuwa nikimaliza kusoma tafsiri, nisome tafsiri nyingine angalau moja ya mtu tofauti. Lakini ukweli utabaki kuwa ingekuwa bora zaidi kama ningekuwa ninakifahamu ki-Rusi, nikajisomea mwenyewe alichoandika Pushkin. Kama taaluma inavyotufundisha, hakuna tafsiri ambayo inaweza kuwa sawa na utungo unaotafsiriwa.

Mtu unaweza kujiuliza: Kwa nini ninajipitisha katika mtihani huu wa kusoma Eugene Onegin, badala ya kusoma vitabu rahisi? Jibu langu ni kuwa chemsha bongo ni muhimu kwa afya ya ubongo, kama vile mazoezi ya viungo yalivyo muhimu kwa afya ya binadamu. Utungo kama Eugene Onegin, kwa jinsi ulivyosheheni utajiri wa fikra na kumbukumbu za aina mbali mbali, ni njia bora ya kutajirisha akili. Nitajisikia mwenye furaha nitakapoweza kusema nimeusoma na kuutafakari kwa makini utungo huu mashuhuri wa Pushkin.

No comments: