Monday, May 4, 2015

Kuiheshimu Misahafu ya Dini Zote

Pichani hapa kushoto ninaonekana nimeshika nakala yangu ya Bhagavad Gita, msahafu wa dini ya Hindu. Ingawa mimi ni m-Kristu (m-Katoliki), ninaamini kwa dhati kuwa ni wajibu kuiheshimu misahafu ya dini zote.

Kwa mfano, ninayo Qur'an. Siku moja nilimwuliza kijana mmoja mu-Islam kuhusu heshima itakiwayo kwa Qur'an. Kuna baadhi ya mambo niliyajua, lakini kijana aliniambia jambo la ziada. Alisema kwamba pasiwekwe chchote juu ya Qur'an.

Basi, daima ninakumbuka na ninazingatia hilo. Ingawa ofisi yangu imefurika vitabu, na  mezani pangu panakuwa pamefurika vitabu, na Qur'an yangu iko hapa hapa mezani muda wote, siwezi kuweka kitabu, karatasi, au kitu chochote juu yake. Nafanya hivi kwa kufuata dhamiri yangu, si kwa kuogopa labda atafika mtu ofisini akute hali nyingine.

Ninaamini kuwa kama dini yoyote inajinadi kuwa ni dini ya amani, ni lazima idhihirishe jambo hilo kwa kuziheshimu dini zingine. Ni lazima iwaheshimu waumini wa dini zingine, na misahafu yao. Kufanya kinyume ni kuhatarisha amani. Amani inajumlisha pia amani ya akilini na moyoni.

Amani haijengwi kwa kuwadharau wengine. Haijengwi kwa kudharau imani za wengine. Inasikitisha kuona jinsi baadhi ya watu nchini Tanzania wanavyozibeza dini za wenzao, wanavyoibeza misahafu ya wenzao, katika malumbano ambayo hayajengi amani bali yanaweka misingi ya kuhujumu amani.

Wa-Kristu tunawajibika kufanya kila juhudi kufuata agizo la Yesu la kumpenda Mungu kwa uwezo wetu wote, akili yetu yote, roho yetu yote, na kwa moyo wetu wote. Tunawajibika pia kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe. Katika mafundisho yake, inadhihirika pia kuwa Yesu alituasa kuwapenda hata maadui zetu. Wa-Kristu tunakatazwa kulipiza kisasi.

Kwa kuwa fundisho la msingi la u-Kristu ni hilo, ambalo linathibitisha kuwa ni dini ya amani, kwa nini nisifanye juhudi ya kuwaelewa wanadamu, kuzielewa tamaduni zao, na kuzielewa dini zao? Mtu asishangae akinikuta ninasoma Bhagavad Gita, Qur'an, au msahafu mwingine, sambamba na Biblia yangu. 

12 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele nakubaliana nawe kuwa ni muhimu kuheshimu misahafu na imani za watu wengine. Ila kuna sharti. Kama nao wanaheshimu misahafu na imani za wengine. Hili la kutoweka kitu chochote juu ya Quran ni ushirikina na kutojua maana ya Quran hasa ikizingatiwa kuwa Quran ni kitabu sawa na vingine. Pili Quran ni ujumbe na si kitabu. Kama kutoweka juu ya Quran kitu chochote ni shurti mbona mahafidh au watu waliohifadhi Quran wanachanganyikana na wengine hasa kwenye madala dala? Je kati ya hafidh na kitabu cha Quran ujumbe uko wapi na upi upewe heshima? Niliwahi kujadili mada hii na vijana wa chuo cha Kiislam cha Al-Haramain ambacho sasa ni chuo kikuu na tukahitimisha kuwa kuitukuza Quran (kitabu) inaweza ima kuwa shirk au ujinga wa kuabudia vitu vionekanavyo. Isitoshe, mtume Muhammad (SAW) hakuacha kitabu kinachoitwa Quran zaidi ya kuiacha kwenye vifua na nyoyo za waumini. Waandishi wa Quran tuliyo nayo walifanya hivyo baada ya kufa Muhammad. Hivyo, kwanza hatujui ni kwanini Muhammad hakuamrishwa na Allah iandikwe Quran. Pili, tutajuaje kama waliongeza au kupunguza mambo hasa ikizingatiwa kuwa master mwenyewe aliyeshushiwa ujumbe alikuwa kishatoweka. Na tatu nadhani Muhammad hakutaka uvivu wa kutohifadhi Quran ndiyo maana hakuamuru iandikwe. Kwa leo nakuchangia hilo.

Mbele said...

Ndugu Mhango
Shukrani kwa mchango wako. Unasisimua akili. Hili ni jambo ninalolitamani na kulienzi. Tuna wajibu kuyatafakari na kuyajadili masuala ya dini sawa na masuala mengine yoyote, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Masuali yako yanatubidi sisi tunaojiita waumini wa dini tuyatafakari kwa kina. Kwa mfano, kuhusu tofauti baina ya ujumbe alioshusha Mungu na maandiko yaliyoandikwa na wanadamu miaka mingi baadaye ni suala muhimu kulitafakari. Tunajionea wenyewe jinsi watu wanavyong'ang'ania maneno ya misahafu kikasuku, badala ya kutofautisha "the letter and the spirit of Scripture."

Ninategemea watu watajitokeza kuongelea masuali uliyoibua, ambayo nayaona ni ya msingi sana.

Khalfan Abdallah Salim said...

Mhango,

Nitoe mchango wangu kama ifuatavyo juu ya mawazo ambayo sio sahihi ya Bwana Mhando:
Mhando anadai:
1. Kutoweka kitu juu ya Qu'ran ni Ushirikina na kuwa Qur'an ni sawa na vitabu vingine. Maoni yangu ni kuwa, lazima ujue ushirikina ni nini kabla ya kudai kuwa tendo au jambo fulani ni Ushirikina. Katika Uislamu, Ushirikina ni dhambi kubwa na ni kitendo cha kuabudu mola asiyekuwa mmoja tena asiyekuwa Mwenyezi mungu au Allah. Ni kuamini kuwa mola anayepaswa kuabudiwa amezaliwa, amezaa au anafanana na kitu fulani hapa duniani.Suala la kutoweka kitu juu ya Qur'an si suala linaoingia katika maana hiyo niliyoitaja ila tu iwapo mtu atafanya mungu wake kuwa ni hicho kitabu badala ya yule aliyenena katika kicho kitabu (Mwenyezi Mungu). Hakuna anayejua Uislamu anayeweza kuabudu Qur'an, waislamu waujuao Uislamu hawafanyi hivyo kamwe.

Qur'an si kitabu kama kitabu kingine, yataka ukisome na ukijue kitabu hiki ili uweze kujua tofauti yake na vitabu vingine si tu ambavyo wanaandika wasomi bali hata misahafu mingine. Tofauti ni kubwa sana, nakushauri usome kitabu hiki ili upate jampo kwa ufupi tofauti ya Qur'an na vitabu vingine: The Sources of the Qur'an: A Critical Review of the Authorship Theories (by Hamza Mustafa Njozi). Ikiwa lengo lako ni kuwa Qur'an ina cover na kurasa kwa hiyo ni sawa na vitabu vingine,nadhani ufahamu wa dhana ya kitabu itakuwa haifahamiki vyema. Prof. Mbele anaweza andaa mada ya kitabu ni nini, aina za viatbu n.k ili watu wafaidike.
Katika kuonesha kuwa hiki si kitabu kama vingine, ni kuwa kitabu hiki kina miiko yake, moja wapo ni kuwa hakiwekwi kitu juu yake, wala hakiwekwi sakafuni wala bafuni wala hakisomwi ila asomaye hupata thawabu kwa kila herufi aisomayo, wala hakishikwi na mtu aliye na janaba au mwanamke akiwa katika hedhi au anatokwa na damu ya uzazi.Soma " Etiquette with the Quran by Imam Nawawi."

Ama juu ya kutowekwa juu yake kitu kingine, Mola anasema juu ya maneno yake " ...Kalimatullah hiya al ulya..." Maana yake "... Maneno ya Mungu (Qur'an) yapo juu (ya maneno ya viumbe)." Moja ya tafsiri ya maneno hayo ni kuwa Qur'an iwe juu ya vitabu vingine, au wewe unaelewaje maana ya maneno hayo?

2. "Kama kutoweka juu ya Quran kitu chochote ni shurti mbona mahafidh au watu waliohifadhi Quran wanachanganyikana na wengine hasa kwenye madala dala? Je kati ya hafidh na kitabu cha Quran ujumbe uko wapi na upi upewe heshima? " Maswali mazuri, La kwanza jawabu lake ni kuwa kuchanganyikana si sawa na kuwa juu ya mwengine. Swali la Pili,kwa ufupi, ujumbe upo katika Qur'an na upo kwa hafidh na ujumbe utabaki na hishima yake ile ile hata kama hafidh ni mtu muovu, ujumbe atakaosoma kutoka katika Qur'an, heshima yake ni ile ile na ujumbe utakaosomwa na mcha mungu.
3. "Niliwahi kujadili mada hii na vijana wa chuo cha Kiislam cha Al-Haramain ambacho sasa ni chuo kikuu na tukahitimisha kuwa kuitukuza Quran (kitabu) inaweza ima kuwa shirk au ujinga wa kuabudia vitu vionekanavyo." Kwa hayo niliyobainisha hapo juu, ni wazi hitimisho lenu halikuwa sahihi na ni la kirahisi mno.

Itaendelea..

Khalfan Abdallah Salim said...


Endelea..

4. "Isitoshe, mtume Muhammad (SAW) hakuacha kitabu kinachoitwa Quran zaidi ya kuiacha kwenye vifua na nyoyo za waumini. Waandishi wa Quran tuliyo nayo walifanya hivyo baada ya kufa Muhammad." Madai yako ni ya ajabu kwa wenye elimu juu ya jambo hilo, Qur'an imeitwa hivyo na Mwenyezi Mungu, neno Kitabu limetumika mara kadhaa katika Qu'ran. Soma Qur'an sura ya 1 aya ya 2 inasema 'Hiki ni 'Kitabu' kisicho na shaka ndani yake', kitabu hicho si tu kilikuwa katika nyoyo au vifua bali mpaka katika maandishi, nashauri usome kitabu hiki vizuri kufahamu juu ya jambo hilo:An Introduction to the Sciences of the Qur'aan by Abu Ammar.
5. "Hivyo, kwanza hatujui ni kwanini Muhammad hakuamrishwa na Allah iandikwe Quran. Pili, tutajuaje kama waliongeza au kupunguza mambo hasa ikizingatiwa kuwa master mwenyewe aliyeshushiwa ujumbe alikuwa kishatoweka." Nadhani ukishasoma hizo rejea nilizokupa utapata mwangaza na elimu ya kutambua kuwa uliyoyasema si tu ni dhana bali ni aina moja wapo ya upotoshaji.

Mimi nafarijika sana kuwa Prof. Mbele anatuhimiza tusome vitabu sana na maranyingi katika hii blog yake na tuvielewe na tuelimike. Ni vyema tukasoma,tukiwa na fikra huru bila ya kasumba ili tupate mawazo mapya!

Nimalizie na nukuu hii kutoka katika Qur'an "Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayo yatenda. Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hii inasadikisha yaliyo tangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote.Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile. Basi angalia jinsi ulivyo kuwa mwisho wa madhaalimu hao.Na miongoni mwao wapo wanao iamini, na miongoni mwao wapo wasio iamini. Na Mola wako Mlezi anawajua vyema mafisadi.Na wakikukanusha wewe, sema: Mimi nina a'mali yangu, na nyinyi mna a'mali yenu. Nyinyi hamna jukumu kwa niyatendayo, wala mimi sina jukumu kwa myatendayo." Surat Yunus: aya ya 35 -41. Nukuu hii maneno yake si mepesi,yataka mazingatio na umakini.

Niwieni radhi kwa maandishi marefu. Ahsante kwa sasa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Bwana Khalfan Abdallah Salim shukrani kwa mchango wako japo sikubaliani na uchambuzi wako. Mie naitwa Mhango si Mhando. Naomba nitoe maelezo mafupi kuhusiana na Shirk ambayo ni kumfananisha Mungu na kitu chochote. Hiyo ni dhana ya kwanza. Dhana ya pili ni kuabudia kitu kingine zaidi ya Allah. Nadhani kama si kuepuka au tuseme kukwepa baadhi ya dhana nilizojenga ungeelewa nilichomaanisha kuwa ni shirk. Nilijenga hoja madhubuti kuwa a) Kati ya hafidh na Quran huo ujumbe unaoamriwa usiwekewe kitu juu ya content yake yaani kitabu, uko wapi? Nilitegemea swali hili kuu lingejibiwa. Kwani tunaona mahafidh wakisongamana na watu kwenye dala dala. Na sijui hao hafidh wa kike kwenye mikao yao mingine hawawekewi kitu kingine juu? Nadhani kudai kuwa Qurana haipaswi kuwekewa kitu juu yake ni kuitukuza zaidi ya binadamu ambaye imeshushwa kuja kumtumikia na si kuitimikia. Kwa taarifa yako ni kwamba wakati misahafu ikisafirishwa toka Uchina inakochapishwa na kwingineko, makontena kwa makontena hukaliana jambo ambalo ni kuweka kitu juu yake. Na kwa hali ilivyo si rahisi kutoweka kitu juu yake hasa ikizingatiwa kuwa hata watu wanaoapa kwa kutumia Quran wengine huweka mkono juu yake.
b) Kwanini Mtume Muhammad (SAW) hakuacha hiki kitabu kinachoitwa Quran? Jibu lake limo kwenye mchango wangu wa awali. Sijui kama kuna msomi wa Quran na dini mwenye ujuzi kuliko Master mwenyewe. Unapoongelea kitabu kutajwa kwenye Quran haimaanishi Quran yenyewe bali ujumbe. Maana hata hiyo Biblia imetajwa na wale wanaoitumia kuitwa Ahl al-Kitab yaani watu waliopewa ujumbe ambao kwa lugha rahisi huitwa kitab. Kimsingi "Kitab kisicho na shaka ndani yake" haimaanisha volume bali ujumbe. Kwa lugha rahisi ni ujumbe usio na shaka ndani yake.
Nisisitize kuwa kwa wanaoamini Kalimatullah hiya al ulya..." Maana yake "... Maneno ya Mungu (Qur'an) yapo juu (ya maneno ya viumbe)." Kalimatullah ni pamoja na binadamu aliwaumba kwa upendeleo mkubwa. Sijui nao utawaweka kundi gani. Nadhani una haja ya kuzamia zaidi uje maana ya kauli hii hasa ikizingatiwa kuwa Kalimatullah imo vifuani mwa mahafidh na hata kwenye CDs siku hizi. Nadhani kama utakubaliana nami kuwa kadri teknolojia inavyokua, kuna siku hii Quran in the form of book/volume kuna siku itafinywa na kuwa kwenye CDs au USB sticks. Je nazo hazitawekewa kitu juu? Nadhani dhana ya kutoweka kitu juu ya Quran ni ya kizamani wakati wa uhaba na ukosefu wa teknolojia.
Kwa kumalizia naomba nikupe faida nyingine kuwa Quran si kazi mpya wala kitu kipya kilichoshushwa kam wengi wanavyodhani.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Quran ni mkusanyiko wa vitabu vilivyomo kwenye Biblia kama vile Zaburi, Injili na Torati na nyongeza ya sura alizoongeza Muhammad. Kilichotofauti ni kwamba baada ya vitabu hivi ambayo vilishaandikwa kwenye Biblia hivyo kutokuwa na ulazima wa kuviandika upya, vimeandikwa kishairi tofauti na prose ya kwenye Biblia.
Hakuna jipya ambalo Biblia hakulitaja na Quran ikakariri kuanzia Adam na wengine ambao kilichofanyika ni kubadili majina yao na ku-sound ya kiarabu mfano, Yohana anaitwa Yahya, Yesu, Issa, Maria, Mariam, Eve, Hawa na wengine wengi. Kuna jipya hapa kama tutaamua kutumia akili bila imani?
Nimalizie kwa kushukuru kupendekeza mdaharo kuhusiana na suala hili. Pia nishauri kuwa usihukumu kuwa watu hawajaisoma Quran bila kujua backgrounds zao. Umenikumbusha ugomvi uliwahi kutokea baina yangu na wanafunzi wangu wa Al Haramain nilipojitambulisha kwao kama Sayyidna Nkwazi Mhango (RA)Radhiallahu 'anhu yaani Allah awe na radhi nami. Walishangaa kuona natumia kitu walichodhani ni exclusive venue ya masahaba au marafiki wa mtume. Waliamua kugomea vipindi vyangu vya fasihi ya kiingereza hadi nilipowapa darasa kwa kuuliza ni nani alikuwa radhi mimi niumbwe kama siyo Mungu? Baada ya hapo wengi wa wanafunzi wangu walianza kutumia title hii ili kuondoa dhana ya ubaguzi kuwa marafiki wa mtume walikuwa waarabu tu wakati Quran inasema kuwa marafiki wa kweli wa mtume ni wale waliomwamini bila kumuona wala kumsikia. Hivyo, kinachogomba kwa wengi ni mazoea na mafunzo ya kidini yasiyo na critical thinking. Kwa watu wasiofikiri kibubusa kila kitu kinaweza kuwa deconstructed. Bahati mbaya mimi ni deconstructionist karibu wa kila kitu ikiwamo dhana nzima ya kuletawa dini za kimamboleo na kutufarakanisha, kututenganisha kiasi cha baadhi ya ndugu zetu kujihisi wana udugu zaidi na co-religionists wao kuliko hata ndugu zao wa damu. Kuna haja ya kuelewa kwanza kabla ya kuamini maana kuamini ni kujiridhisha na jambo ambalo hulijui kana kwamba unalijua. Je unalijua? Dhana hizi nimezijadili kwenye kitabu miswada yangu ya Africa reunite or Perish ambayo Insh'Allah na Deconstructing education: Taking on the dominant western grand narrative (Hiki ni cha kisomi-academic book) ikitoka huenda utasoma na kuelewa.
Hata kwenye vitabu vyangu vya Saa Ya Ukombozi na Nyuma ya Pazia nimegusia imani za kibubusa na mfarakano na hasara tunayopata waafrika kama jamii ya watu ambapo tusipokengeuka tutabakia kwenye ukale na ujinga huku wenzetu wakipaa na kuendelea kututawala na kutunyonya kama wanyama.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim na Ndugu Mhango,

Haya ndio aina ya mambo ninayopenda kuyaona katika blogu yangu.

Nataka blogu yangu iwe na ibaki kuwa ni uwanja ambao ni huru kwa mawazo, maoni, na mitazamo kuwekwa na kujadiliwa kwa hoja, bila vitisho au kupigwa marufuku kama inavyofanyika katika hizo zinazoitwa dini.

Tuendelee na mjadala.

Anonymous said...

Nashukuru sana Ndugu Mhango na Ndugu Khalfan hay ndio majadiliano ninayoyapenda pia. Ndugu Mbele nashukuru pia.
Tukifikiri namna hii watanzania tutakuwa watu wa maana sana, kuliko kuwa washabiki wa imani za kigeni kama nilivyowahi kusema hapo awali.
Mkae salama.

Mbele said...

Ndugu Anonymous wa May 7, 2015 6:28 PM, ni kweli, tukijifunza na kujizoeza kutumia akili badala ya jazba na mihemko, tutakuwa tumefikia ustaarabu wa kupigiwa mfano.

Bado njia ni ndefu, lakini hatua ndogo ndogo tunaweza kupiga, kama huu mjadala wa kistaarabu ambao tumeuona katika ukurasa huu. Tutafika.

Khalfan Abdallah Salim said...


NN Mhango,

Pole kwa kukosea jina lako. Juu ya swali lako ulilotegemea kujibiwa, na kwa kuwa umeupanua mjadala wake kujumuisha Kitabu, Watu, Cd, flash na makontena, swali linalojitokeza hapo ni je vipi iwapo Qur'an ipo katika vitu hivyo? Mimi nilikujibu juu ya kitabu tu. Sasa nitoe maoni yangu juu ya watu nakadhalika.

Suala na kuihifadhi kifuani, au katika CD, flash, Kontena nakadhalika hizo ni hali tofauti na hali ya kitabu, japo upo mfanano katika tofauti zao. Kwa tofauti zao, hata namna ya kuheshimu hutofautiana. Hali kadhalika tunaona vitu vikiwa katika hifadhi tofauti, huhifadhiwa tofauti. Usisahu, kuwa lisilo na budi hufanywa!

Mada ni kuheshimu misahafu yawengine, na kutoweka kitu juu ya Kitabu cha Qur'an ni katika kuheshimu kitabu hicho. Kufanya hivyo sio ushirikina hii ndio hoja yangu katika kupinga hoja yako ya awali kuwa "Kutoweka kitu juu ya Qu'ran ni Ushirikina." Kwangu mimi, hamna dalili yenye ushawishi, unaposema hivyo bali ni kutofahamu mambo na kuyachanganya au kujichanganya.

Pili, unadai kuwa "Quran ni mkusanyiko wa vitabu vilivyomo kwenye Biblia kama vile Zaburi, Injili na Torati na nyongeza ya sura alizoongeza Muhammad. Kilichotofauti ni kwamba baada ya vitabu hivi ambayo vilishaandikwa kwenye Biblia hivyo kutokuwa na ulazima wa kuviandika upya, vimeandikwa kishairi tofauti na prose ya kwenye Biblia." Hilo ni dai kongwe sana kwa wale wasioikubali Qur'an, hata Maqureish wa maka wakidhani hivyo na kusema hivyo japo kuwa maneno ni tofauti.

Dr. M.Amir Ali, amejibu hoja yako aliposema "The mere existence of similarities between any two books is insufficient to prove that one must have been copied from the other.Both could have drawn information from a third common source, thus accounting for some similarities between them. Could the Qur’an have been copied from the Bible if they exhibit serious creedal differences? Regarding doctrines such as the concepts of God and prophethood, sin and forgiveness, the Qur’an differs significantly with the Bible. Even in the case of narration common to both scriptures, vital discrepancies can be observed. For example, the Qur’an, unlike the Bible:

— does not blame women for the mistake committed by Adam and Eve (peace be upon them) in disobeying God in the Garden of Eden. (Compare Genesis 3:12-17 with Q.91:7-8 and 2:35-37);
- mentions that the eventual dwelling of Adam and Eve on Earth was already part of God’s plan even before He created them (Q.2:30), and not a sort of punishment (Genesis 3:17-19).

The Qur’an also mentions a good amount of historical information about which the Bible is completely silent. From which portion of the Bible were the following copied?

-The stories of the people of ‘Ad and Thamud, and their Prophets, Hud (p) and Saleh (p).
-The dialogue between Prophet Noah (p) and his son before the flood (Q.11:42-43).
-The dialogue between Abraham (p) and his father (Q.6:74), as well as between he and a king (Q.2:258), and between he and his people (Q.22:70-102; 29:16-18; 37:83-98; 21:57).
-The mention of the city of Iram (Q.89:7).
-The Pharaoh of the Exodus having drowned, with his body preserved as a sign for people of future generations (Q.10:90-92)."

Mifano ipo mingi sana, yenye kuonesha tofauti kubwa iliyopo baina ya Qur'an na Bible n.k.

Itaendelea.





Khalfan Abdallah Salim said...


Tatu, unasema "Umenikumbusha ugomvi uliwahi kutokea baina yangu na wanafunzi wangu wa Al Haramain nilipojitambulisha kwao kama Sayyidna Nkwazi Mhango (RA)Radhiallahu 'anhu yaani Allah awe na radhi nami.Walishangaa kuona natumia kitu walichodhani ni exclusive venue ya masahaba au marafiki wa mtume.Waliamua kugomea vipindi vyangu vya fasihi ya kiingereza hadi nilipowapa darasa kwa kuuliza ni nani alikuwa radhi mimi niumbwe kama siyo Mungu?" Ukiona neno limetumika mahala ujue limesadifu matumizi yake. Je unajua kwa nini masahaba wanaitwa hivyo? Unaonaje hivi ukimsikia rafiki rako asiye na mwana akajiita "Baba Juma Bakari" iwapo mtu mlevi, mzinzi na mshirikina unayemjua akijiita " Mtakatifu Juma Bakari" Nadhani kuna haja ya deconstructionist wa mambo ya maana na yale unayojua historia yake.

Kwangu mimi, kujiita hivyo ni kukosa uungwana, japo ni hiyari yako. Masahaba huitwa hivyo wala hawajajiita wao hivyo, wewe unajiita mwenyewe! Kufanya hivyo kuna maana gani, kama deconstructionist?

Ni hayo tu kwa sasa.


Siraji Haji said...

Joseph Mbele kwa upande huu wa Dini nimekuelewa msimamo wako ila kule kwenye siasa sikuelewi tusiuhamishie ule mjadala huku ili tusivuruge maudhui haya asante,SIRAJI HAJI

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...