.jpg)
Yapata wiki moja iliyopita, katika duka la vitabu la hapa Chuoni St. Olaf, ambamo daima kunakuwa na vitabu vingi ambavyo sijawahi kuviona, niliguswa kukiona kitabu cha Terry Eagleton, How to Read Literature, ambacho nilikuwa sijawahi hata kukisikia.
Terry Eagleton ni mwananadharia wa fasihi ambaye ni maarufu kabisa. Nilinunua vitabu vyake kadhaa na kuvisoma miaka ya 1980-86 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu Cha Wisconsin Madison. Nimeanza kusoma na kuvutiwa na How to Read Literature.
Juzi tarehe 14, wakati narudi kutoka Columbia Heights, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la vitabu la Half Price Books ambalo nimelitaja mara nyingi katika blogu hii. Nilinunua vitabu vitatu.
.jpg)
Kitabu kingine nilichonunua, Bluest Eye/Sula/Song of Solomon nacho kimejumlisha vitabu vitatu vya Toni Morrison. Ninahisi ninavyo vitabu hivi, ila sina hakika, kwani nina vitabu vingi sana. Toni Morrison ni mwandishi mmojawapo maarufu kabisa duniani. Alipata tuzo ya Nobel. Nina kitabu chake Playing in the Dark, ambacho kina fikra pevu kuhusu athari za utamaduni na fasihi ya wa-Marekani Weusi katika historia ya fasihi ya Marekani.
Kitabu cha tatu nilichonunua ni Great Expectations, cha Charles Dickens. Ninacho kitabu hiki, pamoja na vingine vya mwandishi huyu maarufu. Lakini hii haikunizuia kununua nakala nyingine. Labda, huko mbele ya safari, nitaweza kukijumlisha katika vitabu ambavyo nimekuwa nikitoa kwa vyuo, taasisi, na watu binafsi Tanzania.
No comments:
Post a Comment