Sunday, May 3, 2015

Vitabu Nilivyonunua Karibuni

Napenda kuendelea na jadi yangu ya kuvitaja vitabu nilivyoongeza katika maktaba yangu katika siku chache zilizopita.

Kitabu kimoja ni The Poetic Edda: Stories of the Norse Gods and Heroes, kilichotafsiriwa na Jackson Crowford. The Poetic Edda ni kitabu maarufu sana ambacho nimekisikia kwa miaka mingi. Ni mkusanyo wa hadithi na mashairi ya mapokeo juu ya miungu na mashujaa wa Iceland.

Nimeamua kujipatia nakala wakati huu ambapo nimekuwa nafundisha utungo maarufu wa Finland uitwao Kalevala. Kwa pembeni nimekuwa nayapitia pia mashairi ya mapokeo ya Finland yaliyokusanya na Elias Lonnrot katika kitabu kiitwacho Kanteletar. Nina hamu ya kuona kama The Poetic Edda inahusiana na hizo tungo zingine, kwa kuzingatia kuwa zote ni za Ulaya ya kaskazini.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Village by the Sea, cha Anita Desai wa India. Nilipangia kukifundisha muhula huu katika kozi yangu ya Post-colonial Literature, lakini tumeishiwa muda. Nimeshafundisha riwaya kadhaa za Anita Desai. Ni mwandishi bora sana. Ndio maana nikaamua kukiweka kitabu chake cha The Village by the Sea katika orodha ya muhula huu.

Kitabu kingine nilichonunua ni Monkfish Moon. Ni mkusanyo wa hadithi fupi za Romesh Gunesekera wa Sri Lanka, ambaye riwaya yake ya Reef nimeifundisha. Gunesekera ni mwandishi hodari sana. Nilikijumlisha kitabu chake cha Monkfish Moon katika orodha yangu ya Post colonial Literature. Lakini, muda umeshindikana.

Kitabu kingine nilichonunua, yapata wiki moja iliyopita, ni See Now Then cha Jamaica Kincaid wa Antigua, Carribean. Niliwahi kuhudhuria mhadhara wake katika Chuo Kikuu cha Minnesota.

Kitabu kingine nilichonunua, ambacho nimekipata leo, ni The Gunny Sack, cha Moyez Vassanji. Moyez Vassanji alizaliwa Kenya lakini alikulia Dar es Salaam. Ni mwandishi maarufu ambaye anaishi Canada. Kati ya vitabu vyake vinavyovuma sana ni Uhuru Street na The Book of Secrets., ambacho niliwahi kukifundisha katika semina ya waalimu Chuo cha Colorado. Kinavutia sana kwa ustadi uliotumika katika kukiandika. Kitabu chake kingine, Amriika, nilikinunua miezi mingi iliyopita ila sijakisoma bado.

1 comment:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Hakuna utajiri unaodumu milele kama vitabu.Huwa nina falsafa moja: Kwanini kuwatumikisha watu wakati kuna watumwa wazuri wenye kutii na kuelewa mambo kama vitabu? Kama u mpenzi wa ushairi basi kitabu changu cha Souls on Sale kikitoka lazima nikutumie kimoja. Huwa napenda msisitizo na kutambua kwako umuhimu wa vitabu. Kwangu mimi bila vitabu nisingekuwa hapa nilipo na nilivyo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...