Nimeona taarifa leo kuwa msikiti umechomwa moto huko Saudi Arabia. Ni msikiti wa dhehebu la Shia. Kwa wale wasiofahamu, wa-Islam, kama walivyo wa-Kristu, wana madhehebu mengi, kama vile Sunni, Shia, Ismailia, Ahmadiya na Tijanniya.
Habari ya msikiti kuchomwa moto imenikera, kama ninavyokerwa na habari za kuchomwa moto kanisa au nyumba nyingine ya ibada ya dini yoyote. Nimesema tena na tena kuwa ninaziheshimu dini zote, ninaiheshimu misahafu ya dini zote, na ninazihehimu nyumba za ibada za dini zote. Ninaamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya busara ambayo tunapaswa kuifuata.
Sawa na waumini wa dini zingine, nami nililelewa katika imani kwamba dini yangu ndiyo pekee dini ya kweli. Nilifundishwa kwamba nje ya dini yangu, nje ya u-Katoliki, hakuna wokovu. Ninajua kuwa wa-Islamu nao wanafundishwa hivyo hivyo, kuwa nje ya u-Islamu hakuna wokovu. Niliwahi kuwa mwanachama katika mtandao wa Radio Imaan, wa wa-Islam. Waliniambia kuwa mimi ni kafiri na kwamba nisiposilimu sitaingia ahera.
Hii ndio hali halisi. Binafsi nimeamua kujitungia mwelekeo nilioutaja hapa juu, ingawa ninajihesabu kama m-Katoliki. Katika hilo, simtumikii wala kumfuata binadamu. Natumia akili yangu na kufuata dhamiri yangu.
Kwa nini mtu uchome moto msikiti wowote, kanisa lolote, au nyumba ya ibada ya dini yoyote? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kwa msikiti wa Shia kwa vile tu wewe ni Sunni, au ni m-Kristu, au ni m-Hindu? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kanisa, kwa vile tu wewe si m-Kristu?
Kama hukemei, unaufumbia macho uozo ambao siku moja utakuja kusababisha nyumba ya ibada yako ichomwe moto. Usishangae ikitokea hivyo, wala usikasirike, kwani roho yako haina tofauti na ya yule atakayefanya uhalifu huo. Kilichopo ni kujitambua.
Tumelelewa na tunalelewa katika njia ya giza. Tuamke. Tuanze kujijengea mtazamo mpya wa kuheshimiana wanadamu wote, kila watu na imani yao, wenye dini na wasio na dini, na tuwalee watoto wetu katika njia hiyo.
Hayo ndio mawazo yaliyonijia niliposoma taarifa ya kuchomwa msikiti wa Shia kule Saudia. Ni mawazo yanayoendelea kunisonga na kuisumbua akili yangu. Kama unaona nimepotoka au ninapotosha, nawe ni muumini wa dini, kumbuka kuwa una wajibu wa kujitokeza, kukosoa, na kurekebisha. Ukiacha kufanya hivyo, kumbuka kuna jehenam au motoni, kama tunavyoita wa-Kristu. Na ukichangia, ukajiita "anonymous," unajisumbua na unajidanganya, kwani ingawa mimi sitakutambua, Mungu (Allah) anakuona na atakufichua siku ya kiyama. Kazi kwako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
6 comments:
Nimefurahi kuwa umelizungumzia hili. Lakini ili kuweka rekodi sawa huo msikiti haukuchomwa moto bali wakorofi wa ISIS walimpeleka mtu ambae alikuwa amejizongoresha mabomu na alipofika ndani akajiripua na kuuwa watu kama 20.
Lakini kitu cha kukumbukwa ni kuwa hawa wanaofanya hivi wanafanya ili kuiyumbisha serikali ya Saudia ambayo ndio mmoja wa adui wao.Wanaona tayari Saudia anapigana vita kule Yemen dhidi ya Houthi ambao ni mashia. Kwahiyo ISIS wameona wakiwaripua mashia ndani ya Saudi, itaongeza chuki dhidi ya Saudia. Kwa bahati mbaya hapa ni siasa ndio inayofanya kazi.Pia kumbuka kuwa ISIS wanapigana Syria na wale wanaomuunga mkono Raisi wa Syria ni mashia na serikali ya Iran. Kwahiyo wanataka kuendeleza uadui wao tu.Siku hizi watu wanatumia tofauti hizi za kidini zilizopo kwa manufaa yao ya kisiasa.
Ndugu Anonymous,
Shukrani kwa mchango wako kwenye suala hili la mlipuko msikitini. Papo hapo, napenda kurekebisha kauli yangu kuhusu wachangiaji "anonymous." Nimetambua kuwa yawezekana kuna watu wenye sababu za msingi za kutojitambulisha. Kwa hivi, ni bora kila mtu aamue mwenyewe, bila kipingamizi.
Nangojea kusikia maoni ya yeyote anayependa kuchangia.
yatia hamasa....lakini siku moja weusi yabidi warudie miungu yao...ndipo watalikomboa bara hili..
Ndugu Anonymous uliyeandika May 23, 2015 at 8:24, shukrani kwa ujumbe wako.
Yeyote anayezingatia ukweli, bila upendeleo, inambidi akiri kuwa wahenga wetu hawakuwahi kupigana kuhsiana na Imani zao za dini. Imani zao za dini hazikuwahi kuwa chanzo au kichocheo au kisingizio cha magomvi.
Huu upuuzi umekuja na hizi dini zilizotoka nje, kama vile u-Islam na u-Kristu. Tukubali hiyo hoja, bila kigugumizi. Tunaambiwa kuwa mpenda ukweli ni mtu wa Mungu.
Kuhusu kurudi kwenye imani za jadi, tatizo ninaloliona ni kuwa jamii zetu nyingi hazina kumbukumbu, kwani dini za kigeni zilifanya kila juhudi kuzifuta imani na ibada zile. Kwa mfano, ukinipa mtihani niandike ukurasa moja tu kuhusu imani za jadi za ukoo wangu au kijiji changu, nitafeli vibaya sana.
Tumekwama. Tumebaki tunanyoosheana vidole kuhusu eti Qur'an inasema hivi, eti Biblia inasema hivi, hadi povu linatutoka mdomoni, na mwisho ni kushikiana mapanga na kutoana roho.
Prof,. Naona umeamua kuvalia njuga hili swala hongera sana. Sikukatishi tamaa. Tatizo kubwa la kubwa la hizi dini kukosekana kwa hoja kuwa kila mwanadamu anauwezo wa kuelewa na kuchambua mambo kwa uwezo tofauti na uwelewa tofauti. Hizi dini hazikubali hizi tofauti. Haiwezekani na haitawezekana watu wote wakafikiri sawa. Lakini kwakuwa misingi ya hizi dini haijajengwa katiko hoja pingamizi, basi matatizo yataendelea. Prof. Ninawazo na ninaomba kama utakuwa nafasi unipe mawasiliano, niwasiliane nawe. Labda tunaweza kuokoa Jamii zetu.
Ndugu Anonymous uliyeandika May 24, 2015 at 6:53 AM, shukrani kwa ujumbe wako.
Ni wajibu wa msomi kutafuta ukweli bila kuchoka, kwa kutafiti, kusoma, kufikiri, kuchambua hoja, kukosoa na kujikosoa. Ni wajibu wa msomi kujitambua kuwa kile anachokijua, au kile anchodhani anakijua, ni hafifu na hivi lazima aendelee kutafuta elimu.
Kwa vigezo hivyo, mimi ni msomi, na usisite kunikosoa au kunielimisha kwa namna nyingine yoyote. Bila shaka, na wengine wa aina yangu wataelimika pia.
Naona umesema jambo la msingi sana, kwamba kila mtu ana kiwango chake cha kufahamu mambo.
Nami naamini kuwa Mungu atamhukumu kila mmoja kwa kiwango cha akili alizompa na namna alivyozitumia. Kwa hivyo, utaona ni kosa kwetu kubambikizana mambo kama vile tuna akili sawa.
Dini kwa ujumla zina tabia ya kubambikiza mambo na mara kwa mara ni kwa vitisho, badala ya kufundisha na kisha kumwachia kila mtu achambue mwenyewe kufuatana na uwezo wa akili yake. Kungekuwa na hali hiyo, watu wangeachwa huru hata kubadili dini. Lakini ninafahamu kuwa kuna watu ambao wanaishi kwa hofu ya kuhujumiwa uhai wao kwa vile tu wamebadili dini.
Post a Comment