Wednesday, September 5, 2012

Nilizuru Nyumba za Ibada za wa-Hindu, India

Mwaka 1991 nilipata fursa ya kwenda India, kwa utafiti wa mwezi moja. Nilifikia katika taasisi ya American Studies Research Center, ambayo ilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Osmania, mjini Hyderabad. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishi na wa-Hindi.

Siku moja, Afande Rana, mstaafu wa jeshi la India, alinichukua kwa piki piki yake, tukazunguka maeneo kadhaa ya Hyderabad. Alinipitisha katika nyumba kadhaa za ibada za wa-Hindu, kama inavyoonekana katika ukurasa huu.
 




Hapa kushoto tunaonekana mbele ya nyumba mojawapo ya ibada, tukiwa tumevaa vilemba.


Kwa bahati nzuri, ninasoma misahafu na maandishi mengine ya u-Hindu. Ninafahamu kiasi cha kuridhisha kuhusu historia ya dini hii, imani yake. Ni dini yenye miungu wengi, baadhi wanafahamika kwa kila muumini na kuabudiwa, na wengine hawafahamiki na kila muumini. Baadhi ya miungu hao wanachorwa wakiwa na umbo la wanyama. Kwa mfano mungu aitwaye Ganesha anawakilishwa na tembo, na mungu aitwaye Hanuman anawakilishwa na umbo la tumbili. Ndio maana hapa kwenye picha kushoto, ninaziangalia sanamu kwa uchaji.
 Hapa tuko mlangoni pa nyumba ya ibada. Tunapiga kengele, kabla ya kuingia. Sikuelewa maana yake, lakini nimesoma hivi karibuni kuwa huu ni utaratibu wa kuwafahamisha miungu kuwa umekaribia kuingia hapo.
Hapo kushoto naonekana nikitoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Mhusika wa nyumba hii anaonekana akitabasamu, ingawa alijua kuwa mimi si m-Hindu. Ni ishara kuwa watu wa dini mbali mbali tunaweza kuheshimiana na kupendana bila tatizo.
Hapa naonekana nimekaa kwa heshima kabisa ndani ya nyumba ya ibada. Sikumbuki kama nilikuwa ninasali, au kama nilisali vipi, au labda nilikuwa nimegubikwa na mshangao kuwemo katika nyumba hii ya ibada ya dini ambayo sio yangu. Katika mazingira kama haya, mtu unaogopa kukiuka utaratibu, kwa hivi nadhani nilikuwa na woga fulani.
Hapa ninaonekana nikiendelea kutoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Kwa kufanya hivyo, siamini kama nilikiuka imani yangu ya Katoliki. Niliwahi kukaribishwa misikitini katika mji wa Lamu. Niliingia kwa heshima zote, na bado mimi ni m-Katoliki. Nashukuru kupata fursa ya kuona nyumba hizo za ibada na hivi kujiongezea ufahamu kuhusu dini hizo. Kwa mtazamo wangu, hii ni njia moja ya kujenga maelewano na kuheshimiana miongoni mwa watu wa dini mbali mbali.

2 comments:

Anonymous said...

hicho ndicho ninachokupendea profesa wangu kwani,maana kunawengine kuingia msikitini wakati akiwa mkiristo au kuingia kanisani wakati akiwa muislam wanaona kama muhali maana mimi nilitoka ktk ukristo nikaingia kwenye uislam hakuna nilichokiona kimebadirika kwenye kiwiliwili changu au kwenye akili zangu kwahiyo watu tatizo lao wanajikwaza au akiliyao wanaiweka upande mmoja kiasi kwamba labda kama vile kusikiliza imani ya mtu mwingine ni muhali.Binafsi bado vilevile ninaamini IBADA zetu za kale kupitia mizimu yetu kwamaana ninafanya matambiko kila mwaka ya mizimu yetu hivyo ninajisikia kuwa huru sikwaziki asante sana profesa kwa uelimishaji mzuri sana ubarikiwe KAZOBA KA NYAMUHANGA AKWEBEMBELE.....

Mbele said...

Ndugu Kazoba ka Nyamuhanga Akwebembele, shukrani kwa ujumbe wako na mawaidha yako murua. Ni kweli usemavyo, tuko ambao hatujawahi hata kuwazia kuingia katika nyumba za ibada za dini tofauti na zetu.

Kwa upande wa Tanzania, nilichoona ni kuwa sisi wa-Kristu tunaogopa hata kuusogelea msikiti. Sijui wa-Islam wana hisia zipi kuhusu kulisogelea kanisa au kuingia ndani.

Woga wangu ulitoweka nilipotembelea Lamu, pwani ya Kenya. Lamu ni mji unaofahamika kuwa ngome ya u-Islam tangu zamani sana, na una misikiti ya kale maarufu.

Wazee pale Lamu walinikaribisha, na siku moja nilitembezwa katika baadhi ya misikiti, hadi kuingia ndani na kuelezwa mambo ya misikitini.

Sitasahu ukarimu huu na elimu, na jinsi nilivyotolewa woga. Lakini, katika kurejea tena Tanzania, nilirudia utamaduni ule ule tuliozoea, maana sielewi wa-Islam wa Tanzania na wa-Katoliki wenzangu watajisikiaje nikisema naenda msikitini.

Ninachoweza kusema tu ni kuwa inabidi tubadilike, na hili somo ninaliona katika ujumbe wako. Shukrani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...