Pembeni mwa Kanisa kuna nyumba za mapadri na masista, na pia ofisi. Hata Abate/Askofu mstaafu anaishi hapa. Nilienda Peramiho ili kumwona, kwani sijawahi kumwona tangu mwaka 1970, nilipomaliza kidato cha nne katika Seminari ya Likonde, ambapo alikuwa mwalimu wangu wa Historia na ki-Ingereza. Niliambiwa amesafiri. Nje ya makazi yake nilipiga picha inayoonekana hapa kushoto, kwa kuvutiwa na sanamu ya Mtakatifu Benedikt. Maaskofu, mapadri, masista, na mabruda walioleta dini ya Katoliki Peramiho ni wa shirika la Mtakatifu Benedikt. Pamoja na dini, walijishughulisha na masuala ya afya, elimu, na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Hapo kushoto naonekana ndani ya Kanisa. Kwa vile nililiona kanisa hili kwa mara ya kwanza nilipokuwa kijana mdogo, kuwepo tena hapa mahali kulinifanya nikumbuke miaka ya zamani.
Hapo hapo kwenye eneo la Kanisa Kuu niliona kijipango kinachoonekana kushoto, kikiwa na sanamu ya Bikira Maria. Kijipango cha aina hii tunakiita groto. Kwetu wa-Katoliki, groto ni sehemu ya ibada. Ingawa sio kanisani, huwezi kuwepo mahala hapo halafu ukawa unasogoa na marafiki zako au unatafuna njugu. Basi hapo niliona ni muhimu nipige picha pia, iwe kumbukumbu yangu.
6 comments:
Nimefurahi kweli leo nimejikuta nipo nawe hakika nyumbani ni nyumbani...Ahsante kwa kutupeleka KUPERAMIHU LELU
Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe. Napenda nikiri kuwa nilipokuwa nasafiri kutoka Songea hadi Peramiho nilikuwa nakuwazia sana, hasa nilipopita kwenye mji wako wa Ruhuwiko.
Halafu, jana, wakati naandika makala hii, nilikuwa nakuwazia muda wote, nikijua kuwa utaguswa na habari na picha hizi za Kuperamihu.
Yaani..na ndhani uliiona nyumba yetu pale Ruhuwiko..ni kweli nimeguswa sana ..Ahsante tena na tena..
Kama iko karibu na barabara, huenda niliiona, ila tu ni kwamba siifahamu. Dada zangu wawili wana nyumba zao hapo, na huenda watafahamu nyumba yako ilipo. Ni bahati mbaya kwamba ule mwaka jana, tulipokuwa wote Songea, tulipishana bila kuonana, ingawa tulijitahidi.
asante kwa kunikumbusha kwetu
ASANTE
Post a Comment