Sunday, May 24, 2015

Angalizo kwa Wenye Vyama: Tanzania ni Yetu Wote

Mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Natoa angalizo kwa wa-Tanzania wenye vyama, hasa CCM, wazingatie kuwa Tanzania ni yetu wote. Naitaja CCM namna hii kwa sababu ni chama tawala, chenye wajibu wa kuongoza njia na kuwa mfano kwa wengine.

Wa-Tanzania wenye vyama wakumbuke kuwa wao ni wachache kwa kufananisha na idadi ya wa-Tanzania kwa ujumla. Wafanye siasa zao, ila wasisahau jambo hilo. Nasema hivyo kwa sababu wana tabia ya kujiona kuwa wao ndio Tanzania, na Tanzania ni wao.

Kinachonikera zaidi ni fujo. Wa-Tanzania wenye vyama wana tabia ya kuleta fujo na kuhujumu amani, hasa kinapokaribia kipindi cha uchaguzi. Ni aibu sana kwamba, kutokana na fujo za wa-Tanzania wenye vyama, tumefikia mahali sasa ambapo watu wanasali na kufanya ibada kuombea amani. Hii ni fedheha ambayo tumeletewa na wa-Tanzania wenye vyama.

Ni sahihi kumwomba Mungu atupate mvua ya kutosha kwa mazao yetu. Ni sahihi kumwomba atuepushe na majanga kama vile matetemeko ya ardhi. Ni sahihi kumwomba atupe uzima siku hadi siku tuweze kujenga nchi yetu na kutimiza majukumu yetu mengine.

Lakini kuombea amani kwa kuwa inatishiwa na utovu wa nidhamu unaofanywa na wa-Tanzania wenye vyama ni jambo lisilokubalika. Kuombea amani kwa sababu ya utovu wa busara wa watu hao ambao wanadhani nchi hii ni yao peke yao, wanaodhani wana haki ya kujifanyia watakalo katika nchi hii, ni jambo lisilokubalika. Hili si suala la kuombea amani. Ni suala la kupambana na hao wahujumu wa amani.

Inashangaza kwamba hata Ikulu imeshindwa kutambua hilo. Haijawahi kutokea Ikulu ikawaita wa-Tanzania wasio na vyama kwa mazungumzo na mashauriano. Ikulu imekuwa tayari kuwaita wenye vyama na kuongea nao, lakini sio sisi tusio na vyama, ambao ndio wengi zaidi na ni mfano wa kuigwa.

Wa-Tanzania wenye vyama wazingatie kuwa sisi tusio na vyama hatujawahi na hatuna mpango wa kuhujumu amani ya Tanzania kama wanavyofanya wao. Tumetunza heshima ya Tanzania wakati wao wanaihujumu. Wajifunze kutoka kwetu ili wote tudumishe amani na tuipe nchi yetu heshima inayostahili.

2 comments:

babumbwa said...

Huwa nawashangaa sana watu wa dini mbalimbali wanaokusanya waumini wao ili kuombea amani badala ya kuwakemea kwa nguvu zao zote hao wenye vyama wanao hatarisha amani!

Mbele said...

Ndugu babumbwa,
Ninakukumbuka kama mchangiaji wa blogu hii. Narufahi umerejea tena na kuchangia kama ulivyochangia hapo juu.
Wa-tanzania wenye vyama wamezoea kusahau kuwa sisi pia tuko na tuna akili pia. Mimi mwenyewe hutoa mawangu yangu mitandaoni, na imewahi kutokea kuwa nadhaniwa kuwa ni mwanachama wa chama cha siasa, hasa CHADEMA. Hivi mtu hawezi kufikiri hadi awemo katika chama cha siasa?
Mimi naongea kama raia nisiye na chama. Nina mawazo yangu tofauti na yale ambayo huchukuliwa kama "common sense." Ninaihoji "common sense." Ninajaribu kufungua milango ya fikra mpya katika masuala haya ya siasa na mengine. Ninajaribu kuhamasisha kile kiitwacho "thinking outside the bok," kwa ki-Ingereza. Tayari nimechapisha kitabu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii, chenye mwelekeo huo. Katika kurasa za blogu hii upande wa juu kulia, kuna picha yangu, na chini ya picha kitabu hiki kimetajwa. Mtu akibonjeza kile kisanduku cha rangi ya chungwa atatua mahali kinapopatikana kitabu.