Sunday, May 17, 2015

Tuziheshimu Dini Zote

Yeyote anayefuatilia blogu hii anafahamu kuwa ninahimiza tuziheshimu dini zote, tuiheshimu misahafu yote, tuheshimu haki na uhuru wa kila binadamu kuwemo katika dini yoyote anayoona inamfaa, haki na uhuru wa kubadili dini kufuatana na dhamiri yake, na yeyote asiye na dini anastahili heshima sawa na mwenye dini.

Tuzingatie tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo linataja uhuru wa kuabudu kama mmoja ya haki za binadamu. Naamini kuwa msimamo wangu, kama nilivyoueleza hapo juu, ndio njia sahihi inayotupasa kuifuata. Kufanya vingine ni kuendeleza matatizo, migogoro, na dhuluma, na hata umwagaji damu, mambo ambayo tumeyashuhudia kwa karne na karne.

Ninamshukuru Mungu kwa kunipa akili na utashi niweze kutafakari mambo na kuyafanyia maamuzi kwa namna ninayoamini inaendana na mategemeo yake. Simanini kwamba Mungu anataka wanadamu tuwe tunagombana, tunadharauliana, tunakandamizana, au tunapigana.

Mungu huyo huyo amenipa fursa ya kutembea katika nchi nyingi na kuonana na watu wa aina mbali mbali. Mwaka 1991, kwa mfano, nilikwenda India, nikaishi na watu wa dini tofauti na yangu. Nilipata bahati ya kutembezwa katika nyumba za ibada za dini ya Hindu, kama inavyoonekana pichani. Picha moja inanionyesha nikiwa nje ya nyumba ya ibada. Kuna sanamu nyingi, ambazo ni za miungu wa dini ya u-Hindu.

Ninapokuwa katika mazingira kama hayo, ninaonyesha heshima itakiwayo. Wenyeji wangu, wa-Hindu, walinikaribisha katika nyumba zao za ibada, nami nilifanya heshima kama wanavyofanya wao wenyewe. Sioni tatizo kufanya hivyo. Hapakuwa na tatizo kwa upande wao pia, ingawa mimi si muumini wa dini yao.

Miaka ya 1989-90 nilikwenda Lamu, Kenya, kufanya utafiti kuhusu tungo za zamani za ki-Swahili. Lamu ni mji mkongwe wa ki-Islam. Nilikaribishwa vizuri. Wazee kadhaa nami tulianzisha "kijiwe" chetu ambapo tulikuwa tunaongea na kupiga soga.

Siku moja, mzee mmojawapo alinifikisha kwenye nyumba ya Mwana Kupona, mtunzi wa utenzi maarufu wa Mwana Kupona, akanipitisha pia misikitini. Sikuwa nimeingia katika msikiti maisha yangu yote. Nilifuatana na yule mzee huku nikiwa na wasi wasi na uoga. Nilikuwa nimebeba kamera, na aliponikaribisha niingie msikitini, nilimwuliza kama ninaruhusiwa kuingia na kamera. Aliniambia kuwa hakuna tatizo lolote, nikaingia. Nilifanya ziara zangu misikitini kwa heshima zote.

Sioni kwa nini waumini wa dini mbali mbali tusiishi kwa kuheshimiana namna hii, kila mtu na imani yake. Mwenye mawazo tofauti aje hapa tumsikie. Blogu hii ni blogu huru kwa yeyote kutoa mawazo yake. Nami sitachoka kuitumia kuenezea mawazo na mitazamo yangu. Sipendezwi na jinsi watu wanavyoendekeza matatizo na uhasama duniani kwa kisingizio cha dini na misahafu. Nimepinga mambo hayo tangu zamani katika blogu hii.

No comments: