Saturday, May 23, 2015

Leo Nimenunua Kitabu: "Jesus: Prophet of Islam"

Leo nilikwenda Minneapolis kwenye mkutano mdogo wa watu wanne ambao tulifanyia katika jengo la maduka na biashara mbali mbali liitwalo Somali Mall. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jingo hili. Nilipata fursa ya kuingia katika duka la vitabu liitwalo Akmal Bookstore, ambalo limejaa vitabu vya ki-Islam katika ki-Arabu na ki-Somali.

Niliuliza iwapo kuna vitabu vya ki-Ingereza, nikaonyeshwa. Niliviona vingi vilivyonivutia, nikanunua kimoja, Jesus: Prophet of Islam, kilichoandikwa na Muhammad 'Ata' ur-Rahim na Ahmad Thomson.

Nimefahamu kwa miaka mingi kuwa katika u-Islam, Yesu anatambulika kama mtume maarufu, ila sio mwana wa Mungu, kama tunavyomwona sisi wa-Kristu. Sioni tatizo, wala sikosi usingizi kwa sababu hiyo. Ninachozingatia ni waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kila mtu na imani yake. Tukumbuke kwamba dini zinatofautiana, na kuna dini ambazo hamzimjui Yesu kabisa, iwe ni kama mtume au mwana wa Mungu.

Mara yangu ya kwanza kuelewa namna wa-Islam wanavyomwona Yesu ni wakati nilipokuwa nafundisha somo la "Epic" kwa wanafunzi wa uzamili (M.A.) katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1986-88. Kati ya maandishi ya kitaaluma niliyoyaongelea darasani ni insha maarufu ya Alan Dundes, "The Hero Pattern and the Life of Jesus."

Ulipofika muda wa kuandaa tasnifu, mwanafunzi mojawapo, Hamza Njozi, aliniambia kuwa angepnda kuandika kuhusu masimulizi juu ya Yesu (Issa) katika Qur'an. Niliona ni mada murua. Alifanya utafiti na uchambuzi mzuri akamaliza tasnifu yake. Katika kumwelekeza kwa miezi yote ya utafiti na uandishi wa tasnifu, nami niliweza kufahamu msimamo wa Qur'an juu ya Yesu (Issa).

Hii leo, nilipokiona kitabu cha Jesus: Prophet of Islam, nilikumbuka yote hayo, nikakinunua bila kusita. Nangojea kwa hamu kukisoma.

15 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Ninacho kitabu hicho na nimekisoma miaka mingi iliyopita baada ya kupewa na rafiki yangu M-kristo, Mlokole. Sijui kwa nini alinipa mimi. Lakini ninalokumbuka siku moja nilikuwa na mazungumzo ya imani zetu na rafiki yangu mwingine, M-kristo Mkatoliki. Alitusikiliza mazungumzo yetu, kisha baadaye nilipokuwa mimi na yeye alinipa kitabu hicho.

Jambo lililowazi katika kitabu hicho, ni kuwa mafundisho ya Mtume huyu yalivyokuwa na yaleo wanayofunzwa wakristo juu ya Mungu ni tofauti sana.

Ningelipenda kila mkristo some kitabu hicho na iwapo waandishi wamekosea, wakikosoe kwa kujibu hoja za mwandishi ikibidi.

Nilipojadiliana baadaye na rafiki yangu mkatoliki juu ya maudhui ya kitabu hicho, hakuwafikiana na mwandishi lakini hakuweza kujibu hoja zilizomo. Nilifahamu baadaye kuwa, lengo la mwenzangu ilikuwa kubishana tu na si lazima kwa misingi ya hoja na kufikiri kwa makini.

Nikupongeze kuwa umepata kitabu kizuri kuhusu Mtume Issa/Yesu reheme nyingi za Mola ziwe juu yake.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdalla Salim,
Shukrani kwa mchango wako. Kabla ya yote, napenda kukushukuru pia kwa namna unavyojitokeza na kushiriki mijadala katika hii blogu yangu.
Wewe, na mimi, na wengine wanaojitolea muda wao kueleza mawazo yao, mitazamo, mawaidha, hisia na kadhalika, wanafanya kazi muhimu kwa jamii, kuamsha fikra, kuibua masuali, kupanua akili, na kadhalika. Ninaamini kuwa haya ni matumizi sahihi ya akili alizotupa Muumba. Kwa hilo nasema Allah (Mungu) akubariki.

Nadhani tunapaswa kuwa na moyo huu wa kuwa tayari kuwasikiliza wenzetu, kusoma wanayoandika, na kuendelea kuheshimiana, hata kama hatukubaliani nao. Binafsi, sijiwekei mipaka kuhusu vitabu ninavyosoma.
Mimi ni m-Katoliki, lakini nina vitabu vya dini mbali mbali, kama vile u-Islam na u-Hindu, na huwa ninajaribu kuvisoma. Ninasoma pia vitabu vinavyohoji au kupinga dini. Ninavyo vitabu vilivyopigwa marufuku.
Hicho kitabu cha "Jesus: Prophet of Islam," nimefurahi kukiona na kukinunua. Nimeanza tu kukisoma, na nimeona katika utangulizi kinasema sisi wa-Kristu tumepotosha habari ya Yesu. Inaonekana kitabu hiki kimetoa ushahidi thabiti wa hoja hiyo. Siku chache zilizopita, niliona katika duka la vitabu la hapa chuoni petu kitabu kiitwacho "How Jesus Became God," ambacho kimeandikwa na Bart D. Ehrman. Nilikipitia humo humo dukani nikaona kinajenga hoja hiyo. Nitakinunua nikisome.

Ninapenda kuongeza kuwa hiki chuo ninapofundisha kilianzishwa na wa-Luteri, na bado kinajitambulisha kama chuo cha ki-Luteri. Lakini kwenye duka la vitabu unakuta vitabu vya dini mbali mbali na hata vya wapinga dini. Madarasani, mwanafunzi anaweza kujifunza masomo ya dini mbali mbali, kama vile u-Islam na u-Hindu.
Wakristu hatuna haki miliki juu ya Yesu. Yesu anatambuliwa na dini zingine pia, kama vile u-Islam na Bahai. Wote wanamfahamu Yesu kwa namna yao.
Wa-Islam nao hawana haki miliki juu ya Muhammad. Nimesoma kuwa Mtume huyu anatambulika katika dini ya Bahai pia. Nao wanamwelewa kwa namna yao. Na nimmewahi kusoma kuwa hata miongoni mwa madhehebu ya wa-Islam, kuna tafsiri tofauti. Kwa mfano, kuna wale ambao kwao ni marufuku kuchora picha ya Muhammad, na kwa wengine kuchora picha za Muhammad imekuwa ni jadi tangu zamani.
Binafi nataka pawe na uhuru wa kufanya utafiti, hata kama ni kuhusu hao mitume, na kuandika vitabu, hata kama vinapingana na mafundisho yanayoruhusiwa. Pasiwe na vitisho, wala shinikizo. Naamini pia kuwa ni wajibu wetu kusoma bila mipaka.

NN Mhango said...

Japo sijabahatika kusoma kitabu hiki, title yake ina utata. Kwanza sijui aliyekiandika ni nani na mwenye imani ipi. Pili, kama tutakumbuka vizuri maneno ya Yesu ni kwamba hakuja kwa ajili ya kaumu yoyote isipokuwa nyumba ya Israel. Hata wanaojiita wakristo Yesu hawajui kwani alipoondoka aliacha wanafunzi ingawa wale waliowachukia waliwapachika jina la Ukristo jambo ambalo ni utata mtupu. Pia Yesu si mtume kwa Waislamu kama tutazingatia maneno haya kwenye Matayo 15:24 "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli" Hapa sijui kama watu wa nyumba ya Ismael (Waislamu wapo au ndugu zangu wakristo wa aina zote). Kuonyesha kuwa Yesu hakuwa na utata kwenye matamshi yake, nyumba ya Israel au Yakobo au Mwenda usiku inajulikana kuwa ni koo kumi na mbili zilizotajwa kwenye biblia. Hapa hakuna waislamu wala wakristo. Kwa ufupi ni kwamba watu wa imani nyingi wamejitahidi kumdandia Yesu ili kuhalalisha imani zao. Hata ukiangalia watu wanaoitwa au kuniita maaskofu, hawakidhi vigezo vya Yesu hata kidogo. Kama waislamu watamkiri Yeusu kuwa mtume wao basi watapaswa kumpa talaka Muhammad maana Yesu alisema kuwa yeye ndiye njia kweli na uzima pekee Yohana 14:6. Kuna ushahidi mwingie kuwa Yesu hakuwa na lolote na yeyote isipokuwa wana wa Israel ambao nao bahati mbaya walimkana kutokana na aina yao ya maisha. Shehe Khalfan nilipojibu hoja zako kwenye andiko la kaka Mbele lililopita nilidhani lau ungerejea kukubaliana au kupingana nazo. Hata hivyo, ujumbe ulifika barabara. Nakushukuu kwa michango yako isiyo na jazba. Uendelee hivyo.
Namshukuru kaka mwalimu mwenzangu kaka Mbele kuleta mijadala tekenyeshi za sisimushi kila apatapo fursa ya kuandika. Uendelee hivyo kadhalika.

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani kwa mchango wako wa kusisimua akili. Umenichekesha uliposema wa-Kristu na wa-Islam tunadandia jina la Yesu ili kuhalalisha imani zetu. Huwa napendaga kusikia fikra za kusisimua akili namna hii.

Napingana na wale ambao wakisikia hoja za namna hii, wanapandisha jazba na kutafuta mapanga ili wazitoe roho za watu. Sitachukua upanga hata siku moja kwa misingi kama hiyo. Kama sina hoja ya kujibu hoja, ninapendelea kukiri hivyo.

Hiki kitabu cha "Jesus: Prophet of Islam," kimeandikwa na Muhammad 'Ata' ur-Rahim na Ahmad Thomson. Ninavyokiona kimejenga hoja madhubuti. Si ubabaishaji, bali ni matokeo ya utafiti wa miaka mingi, hasa katika British Library.

Lakini kuna pia waandishi wa-Kristu ambao wanahoji mafundisho mbali mbali ya Kanisa. Wanafanya utafiti bila kipingamizi. Kwangu ni jambo la kujivunia kwamba wa-Kristu hatuwawindi wanaoandika vitabu dhidi ya mafundisho ya dini yetu na kuwakata shingo. Miaka ya zamani, tulikuwa tunawakamata na kuwasulubisha, lakini tumepiga hatua mbele. Tunafahamu kuwa mwenye hukumu ya haki ni Mungu.

NN Mhango said...

Kaka Mbele, kwanza nafurahi kuwa nimekuchekesha maana kicheko ni dawa. Pili nimefurahi kuwa umegundua kuwa hoja zangu licha ya kusisimua akili zina mashiko.
Ngoja nikuchomolee machache kwenye kitabu change cha AFRICA REUNITE OR PERISH uone nisivyocheza na mambo haya. Soma halafu unipe uoni wako.

Those profiteering and depending on abusing Africa said that we worship unseen and dead things as if their deities are alive. If their deities were alive why haven’t they shown it by at least coming once? Anything that is not subject to biological rules is dead arguably. All Gods may be regarded so due to the fact that they don’t share common patterns and rules of living like living ones. This is why all Gods and gods have always spoken through living human beings not through animals or anything if we put myths and folkloric tales and the likes aside. I know this argument can be seen misconstrued–as it has always been the behaviour of pro-God believers and thinkers –with vitriol and other intimidations. Again, if we face it, is there any power under the Sun that can prove the living existence of its God or god without depending on belief but not understanding based on naked truth? Sometimes, those who defend faiths tend to bombard us with blurry arguments and myths so as to be cowered and buy into unrealistic things such as their versions of God as opposed to our version of the same. Why can’t it be agreed that nobody knows what is ahead of her or him as far our perception is concerned with all these many limits especially when it comes to future things? Why should we depend on belief instead of naked and pure understanding of God’s existence and messages? How can you be sure if at all believing is being sure of what you are not sure of as if you are sure of? Ask yourself. Am I sure of what I believe in? The good answer is to the negative. Why don’t we agree to differ that we know our faiths and we don’t know theirs the same they don’t know our faiths but they know theirs especially in making money and colonizing others? Is it possible for the creature who doesn’t know all parts of his or her body, environment and universe able to know God who is so much gargantuan that cannot be accommodated by our weak brains? Then why do we pretend to know God while we know nothing that we make something wantonly for the thirsty of fooling and controlling others? Your God is your God and my God is my God just it is your wife and being. I think this is why Africans did not bother proselytizing others knowing that faith and religions are person issues that do not need conversion or propagations. Another thing that differentiates African religions and neo-religion is the fact that Africans did not complexify their religions in order to threated, dupe or attract others.

Mbele said...

Ndugu Mhango
Nimeufurahia mwelekeo wa hoja zako na pia hoja zenyewe. Kazi ya uandishi wa aina yoyote inaumiza kichwa na inahitaji ustahimilivu katika kusahihisha na kusahihisha tena na tena ili iwe bora zaidi na zaidi. Daima napenda kurejea mfano wa mwandishi Ernest Hemingway, ambaye alipata tuzo ya Nobel kwa uandishi wake. Alikuwa anarekebisha maandishi yake mara nyingi sana ili kuyaondolea kila dosari na kuyanyoosha kwa kila hali ilivyowezekana. Sembuse sisi?
Kwa hivi sitagusia hilo, bali napenda tu kuongelea hoja zako. Masuali unayouliza yana mantiki nzuri. Mambo ya dini ni mambo ya imani. Sioni kama inawezekana kuyathibitisha kisayansi.
Mimi mwenyewe ni muumini wa dini. Ni m-Katoliki. Ninafahamu fika kwamba waumini wa dini mbali mbali wanaamini kuwa kuna ushahidi wa kisayansi wa mambo mengi ya msingi, au yote, yaliyomo katika dini.
Wanaamini, kwa mfano, kwamba, tuna uthibitisho wa kisayansi wa kuwepo kwa Mungu (Allah). Binafsi, siamini tuna ushahidi au tunaweza kuthibitisha kisayansi. Ila ninaamini kwa 100% kuwa Mungu yuko, ambaye kwa ki-Arabu anaitwa Allah.
Nakubaliana nawe kuwa dini ukiziangalia kwa macho ya sayansi hazina mantiki. Na ndio maana msingi wa kila dini ni imani.
Kutokana na kusoma kwangu taaluma kama "Psychology" na "Folklore," imani inaonekana kuwa silika ya binadamu. Haikwepeki. Utamkuta mtu anakuambia hana dini, lakini utamkuta anaamini kuwa kuna mikosi katika maisha yake. Mwingine haamini dini, lakini utamkuta kwa Babu Loliondo anapata kikombe. Mwingine imani yake haiko kwenye dini, lakini utamkuta anatetemeka akisikia bundi wanalia mara kwa mara usiku kwenye paa la nyumba yake au kwa jirani.
Mwingine utamkuta kote kote: utamkuta msikitini au kanisani, na kwa Babu nako yuko. Au utamkuta kanisani yuko, au msikitini, na mfukoni ana hirizi. Kwa wengi, imani kwa Allah (Mungu) haitoshi. Ni lazima wapate kikombe cha Babu pia na hirizi kibindoni.
Hoja yangu ni kuwa binadamu ni kiumbe wa ajabu, hata awe mwanasayansi maarufu. Nami, pamoja na kusoma kwangu sana, ni muumini wa dini yangu ya Katoliki, na nitadumu humo maisha yangu yote. Sijui, labda ninawakera waumini wenzangu kwa baadhi ya mawazo yangu, lakini, kama wanayosema vijiweni, hatoki mtu hapa.
Kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu hii ninaheshimu na kutetea uhuru na haki ya kila binadamu kujiamulia mwenyewe masuala ya dini. Akitaka kuwemo katika dini, ana haki na uhuru. Akitaka kubadili dini, ana haki na uhuru. Akitaka kujitoa kwenye dini yoyote na kuwa bila dini, ana haki na uhuru. Pasiwe na kushinikizana wala kutishana.
Tofauti tu ni kuhusiana na watoto wadogo. Inatambulika kimataifa kwamba wazazi wana haki ya kumlea mtoto wao katika dini yao. Hiyo haki nami naiafiki. Kwa hivi ninapoogelea haki na uhuru hapo juu, ninaongelea watu wazima, sio watoto wachanga, au watoto ambao hajafikia umri wa kuhesabiwa kuwa wakomavu.

NN Mhango said...

Kaka nashukuru. Unapokuwa unaanza kuandika huwa kuna mihemko na vipindi vya miwako ambapo unachokazania ni kuweka neno kwenye karatasi kwanza na kuhariri baaaye. Nakubaliana, nilichochomoa si kazi ya mwisho ingawa bado kuna mhariri mwingine atakayefanya hiyo kazi baada ya mimi kujiridhisha kuwa nilichoandika kimewasilishwa kama nilivyolenga. Hiyo ni draft ya kwanza kabisa ambayo itapikuwa chiseled baadaye.

Khalfan Abdallah Salim said...

@ NN Mhango,

Nikukumbushe kuwa waislamu wanaamini kuwa Yesu/Issa, mola awe radhi naye, alikuwa mtume kwa wana wa israel (Yakubu) kama ulivyobainisha si kwa watu wote. Kuamini hivi si sawa na kusema kuwa mafunzo ya Yesu yanawahusu waislamu, hayawahusu bali ni imani kuwa yeye Yesu alifanya kazi ya kufikisha ujumbe wa Mungu kwa wanadamu japo ni wa kabila au kizazi cha Yakubu. Imani hii ni kwa sababu Qur'an inathibitisha kuwa Yesu alikuwa mjumbe wa Mungu kwa watu hao. Waislamu wanaamini hivyo hivyo juu ya Musa, Yusuf, Yakubu, Ibrahim na Mitume wengine waliotangulia kwa kuwa Qur'an inawatambua watu hao kama mitume ya Allah.

Unasema "Kama waislamu watamkiri Yesu kuwa mtume wao basi watapaswa kumpa talaka Muhammad maana Yesu alisema kuwa yeye ndiye njia kweli na uzima pekee Yohana 14:6." Waislamu hawakiri kuwa mtume wao, bali wanaamini kuwa yesu ni mtume wa mungu aliyefunza imani ya Mungu mmoja ambayo inafunzwa na Uislam. Ndio maana mwandishi wa kitabu alikiita kitabu chake "Jesus: A prophet of Islam" Not of Muslims!

Kila mtume ana zama zake na kitabu chake, kwa kuwa aliyefuata baada ya Yesu kwa ujumbe wa Mungu mmoja ni Muhammad, waislamu wanafuata mafundisho yake na sio ya Yesu. Kadhalika, watu wengine wanakhiyari ya kumfuata au kumkataa japo kuwa watahadhari, kwa kumkataa bila ushahidi wa kufanya hivyo kunamatokeo yake, ambayo sio mazuri kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu.

Umeniita shehe, mimi si katika hao. Ni mwanafunzi na muumini wa dini ya Uislamu na najifunza kila siku na ninayoyajua ni wajibu kuyafikisha kwa wengine. Ningetamani kuona ulichoandika baada ya andiko langu katika makala zilizopita lakini kama ujuavyo hakuna namna ya kujua iwapo kuna mtu kajibu au kachangia juu ya yale uliyoandika. Nikumbushe kichwa cha habari, mwezi na mwaka, ili nione ulichochangia.



NN Mhango said...

Shehe Khalfan nashukuru kwa mchango wako ingawa umejichanganya sehemu. Kama waislam wanamkiri Yesu kuwa mtume wa Mungu mbona wanamkandia Paulo na wengine? Mbona wanampiga vita Gullam Mirza Muislam mwenzao wa Khadiyan? Ajabu wakati wakiwakandia mitume kama Paulo na wengine, hutumia maandiko yao kujenga hoja zao dhidi ya Ukristo. Hayo tuyaache. Kama kila zama ina mtume wake, kwanini Mtume Muhammad alijitangaza mtume wa mwisho kana kwamba umefika mwisho wa zama? Ninachosema ni kwamba hata Muhammad alitumwa kwa ajili ya waarabu na ndiyo maana alisema wazi wazi chini ya dhana ya kushushiwa ujumbe kuwa tumetelemsha Quran kwa kiarabu ili muielewe. Hapo sijui kama wamakonde na waswahili wengine wamo.
Nimekuita shehe kwa maana ya mtu mbukuzi na siyo wale wanaosimama mimbarini. Hata kaka Mbele kwa umri na elimu yake kwa kiarabu ni shehe sawa nami hata papa Francis.
Hoja niliozoongelea ni hapa hapa kwenye uga wa kaka Mbele ulipojibu hoja zangu kwenhye mada ya Mei 4, 2015 isemayo tuheshimu misahafu ya dini zote kama ilivyoanzishwa na shehe Mbele. Pia naomba kutofautiana nawe. Yesu alikuwa mtume wa Yule aliyejuu ambaye wengine humuita Yehova au Yahweh. Kama Yesu alikuwa mtume wa Allah kwanini kwenye mahubiri yake yote hakuna hata sehemu moja aliyotamka jina Allah au alisahau? Kimsingi, usemayo yanathibitisha madai yangu kuwa Quran ni Biblia iliyokopiwa kishairi na Muhammad kwani haina jipya ambalo Biblia haikulitaja ukiacha nyongeza ya Fulkhan aliyoongeza Muhammad. Umenishangaza ulipokana kuwa waislamu hawamkiri Yesu. Kama hawamkiri inakuwaje enjeel au injili yake wanaitumia kwenye kitabu chao ambacho wanapaswa kukifuata kila neno? Nadhani hapa ndipo utata ulipo na wakati mwingine kuchanganyikiwa kama aliyosema kaka Mbele kuwa kisaikolojia mwadamu anaweza kuwa vyote hata vile anavyovikana lakini akavishiriki bila kujua au kwa kujua tena kwa kificho. Nijuavyo mimi, Adam, Yakobo, Ibrahim, Musa na Yesu ndiyo nguzo za dini hizi mbili Ukristo na Uislam. Sasa leo mnapowakana nikama mnajiondoa kwenye uislam. Nadhani kinachopaswa kufanywa ni kutafuta muafaka wa imani hizi kwa ile zinachangia kila kitu. Bila Yesu, Ibrahim, Musa na wengine Muhammad asingepata utume. Maana bila wao hana ujumbe ingawa anadai alishushiwa. Angeshushiwa nini wakati Taurat, Zabur na Injil vilishushwa tayari miaka mingi kabla hajazaliwa? Hapa ndipo kasheshe ya kifikra inapoibuka na kuwafanya wenye kufikiri kwa uhuru nje ya imani kujenga hoja zenye mashiko na zisizoweza kupewa majibu sahihi bila kuubomoa mfumo mzima wa imani.

Khalfan Abdallah Salim said...


Bwana NN Mhango,

Nachelea kusema kuwa maandiko yako ni ishara kuwa unasafari ndefu iwapo unataka kuujua Uislam na Imani yake. Nilipata kukushauri usome vitabu katika mchango wangu uliopita. Baadhi ya vitabu nilivyokutajia wakati ule unaweza kuvipata bure katika www.kalamullah.com. Tafadhali soma kwanza Uislam alafu tujadili.

Lakini nashawishika kujibu baadhi ya maswali yako, kama ifuatavyo;

1. "Kama waislam wanamkiri Yesu kuwa mtume wa Mungu mbona wanamkandia Paulo na wengine? Mbona wanampiga vita Gullam Mirza Muislam mwenzao wa Khadiyan? Ajabu wakati wakiwakandia mitume kama Paulo na wengine, hutumia maandiko yao kujenga hoja zao dhidi ya Ukristo." Utume si kitu cha mchezo japokuwa wapo baadhi ya walinganiaji wa kikristo wanajiita hivyo kwa kinywa kipana. Suali la msingi ni kuwa je kila anayesema ni Mtume basi tumfuate? Au ni vigezo gani vya kuzingatiwa ili kukubali utume wa mtu? Uislamu unamajibu yake na huenda ukristo unajibu lake jingine. Paulo na Gullam mirza, hawajakidhi vigezo vya kuwa mitume iwapo unajua maana ya kuwa Mtume katika elimu ya theology. Mtume Yesu, alibashiri ujio wa Mitume wengi na akatahadharisha kuwa watakuja wa uongo kadhalika Mtume Muhammad, aliwahadharisha wafuasi wake, na baada yake walikuja waliodai utume huko uarabuni.

2. kwanini Mtume Muhammad alijitangaza mtume wa mwisho kana kwamba umefika mwisho wa zama? Hili ni swali zuri, lakini jawabu lake hupatikana kirahisi iwapo utasoma Uislamu hususani Qur'an kwa makini kama mtafiti huru na si mfuasi wa fikra za wengine. Ukifanya hivyo utagundua kama nilivyogundua mimi kuwa hakuna kiumbe anayeweza kuandika maadhui ya kitabu hicho na kwa namna hiyo iliyoandikwa wakati ilipoteremshwa na sasa hata Mtume Muhammad hakuwa na uwezo huo. Rejea vitabu vya watafiti, kama " A brief Illustrated Guide to Understanding Islam " unaweza kukisoma chote hapa: www.islam-guide.com. Chapter ya kwanza, inatosha kukupatia picha ya ajabu za Kitabu hicho, kisha jiuliza yawezekana vipi mtu katika arabia ya 670's A.C, kuweza kuyafahamu hayo, iwapo katika karne hii baadhi yake ndio yamegunduliwa na kuthibitishwa. Ukielewa hili, utatambua pia kuwa suala la Muhammad kuwa ni wa mwisho, si la kwake, bali yule aliyeteremsha kitabu hicho ndiye aliyesema hivyo kuwa hataleta Mtume mwingine.

3. "Ninachosema ni kwamba hata Muhammad alitumwa kwa ajili ya waarabu na ndiyo maana alisema wazi wazi chini ya dhana ya kushushiwa ujumbe kuwa tumetelemsha Quran kwa kiarabu ili muielewe." Hebu jiulize, ulitaka ujumbe wa Muhammad uwe katika lugha gani ili uwe ni ujumbe wa Ulimwengu wote? Ulitaka aseme Kiswahili na kiingereza, kiyahudi n.k? Tafiti zinaonesha kuwa mitume yote ilitumwa kwa lugha za watu wao. Pili, maandiko yao au vitabu vyao na wao wenyewe walisema kwa kinywa kipana wametumwa kwa watu gani. Unajua aliyosema Yesu katika Mathayo 15:24. Je unajua aliyosema Mungu juu ya ujumbe aliompa Muhammad? Katika Qur'an tunasoma hivi " Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui" (Sura ya 34: Aya ya 28) Je wewe ni katika hao wasiojua? Ili ujue tafiti ndugu yangu, ukweli wowote unasifa yake nayo ni kutafutwa.

Kwa kweli maswali yako na maneno yako ni mengi yenye hukitaji kurekebishwa na kujibiwa lakini hayo ya juu ni mfano tu. Waingereza wanapochoshwa na makosa ya mwandishi, husema "your article is full of mistakes, so hard to correct by pen." Natumai unajua makusudio yao!

Juu ya mada ya Tarehe 4 mei, 2015. Nashukuru kwa kunikumbusha nitasoma ulichoandika.

Ahsante.







NN Mhango said...

Ndugu Khalfan,
Shukrani kwa mchango wako makini japo kuna mambo sikubaliani nayo. Kwa mfano unaposema "kisha jiuliza yawezekana vipi mtu katika arabia ya 670's A.C, kuweza kuyafahamu hayo, iwapo katika karne hii baadhi yake ndio yamegunduliwa na kuthibitishwa." Hayo ni mambo yapi? Kama ni dhana kuwa Quran ina mambo mengi ya kisayansi kama namna ya mimba inavyotungwa na hatua zake hili si hoja. Hata waswahili waliijua hili hata wanyama. Ndiyo maana kwenye lugha za kiafrika utakuta pale mimba inapotoka huwa na majina tofauti kulingana na umri wake. Hata ndege wanajua hatua inazopita mimba ndiyo maana hata ulaji wao wakati wa ujauzito huendana na mahitajio ya kiumbe tumboni. Isitoshe si jambo lenye mashiko kulinganisha wakati wa Muhammad na aliyosema kwa vile haya kuwa mapya. Wengine tena wasio mitume katika himaya za Uyunani na Ugiriki walishaandika mambo mazito kuliko hayo. Nilijua utawakana akina Paulo ambao wengi huwakana wanabonwa ingawa huwarejea wanapopata upenyo. Hii ndiyo tabia ya watetezi wa dini. Kuhusu kipande nilichochomoa kwenye mswaada wangu kuwa na makosa, hili ni jambo la kawaida katika uandishi. Si kwetu sisi ambao Kiingereza si lugha ya kwanza hata kwa waingereza wenyewe. Mara nyingi staili za uandishi hutofautinana na hakuna mwandishi asiyekosolewa wala kukosea. Ndiyo maana kuna wahariri. Hivyo, hili lisikupe taabu.
Kwa ufupi nafurahishwa na namna unavyozielekea hoja zangu bila munkari japo sikubaliani na mengi ya majibu yako. Nashukuru kwa ushauri wako kuwa kuhariri na kuhariri na kuhariri ni sehemu mojawapo ya uandishi kama alivyodokeza shehe Mbele.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim
Ni wazi kuwa umesoma vitabu vya u-Islam kuliko asili mia kubwa ya wa-Islam. Vile vile, ni wazi Ndugu Mhango naye, ingawa si mu-Islam, amesoma kuliko asili mia kubwa ya wa-Islam. Mimi pia ninajaribu kusomma hiki na kile kuhusu u-Islam, lakini sijamfikia Ndugu Mhango. Sijakufikia Ndugu Khalfan Abdallah Salim. Ndugu Khalfan Abdallah Salim, nadhani tutakubaliana kwamba ni wa-Islam wachache wanaojua hayo mnayoeleza hapa. Lakini ni wa-Islam.
Na katika dini yoyote ni hivyo hivyo. Wanaosoma vitabu vya dini yao kwa juhudi namna hii ni wachache sana. Wakipewa mtihani watafeli. Lakini wanaamini kuwa wao ni wa-Kristu, wa-Hindu, na kadhalika.
Jambo moja linalojitokeza ni kwamba inaonekana hatuwezi kujua ukweli uko wapi katika haya masuala ya mitume na tafsiri ya misahafu. Ndio maana kuna madhehebu mbali mbali. Ndio maana, kwa mfano, ingawa wako wa-Islam wanaoamini kuwa Muhammad ndiye mtume wa mwisho, kuna ambao hawaamini kuwa Muhammad ni mtume wa mwisho.
Kadhalika katika u-Kristu. Kuna madhehebu mbali mbali, ingawa wote wanasema wanatumia Biblia hiyo na mafundisho ya Yesu huyo huyo.
Kwa hali hiyo, naona ni vema tukubali kuwa tafsiri ni nyingi, na labda hali itaendelea kuwa hiyo. Kila kundi liking'ang'ania kuwa tafsisi yake ndiyo pekee ya kweli, matokeo yake ni magomvi na uhasama, kama inavyodhihirika katika historia, hadi leo.
Ni hatari kuamini kuwa tunachokijua sisi ndio sahihi na ukweli. Ni hatari kuamini kuwa wenzetu wamepotosha imani ya dini yetu. Anayejua kwa uhakika ni Mungu tu.

Anonymous said...

Ndugu mbele kwa maoni yako hapojuu umefafanua vuzuri kuhusu lile nililolisema. Kuwa wanadamu tunauelewa tofauti. Na kamwe hata kama tukisoma vitabu vyote vya imani fulani hatuwezi wote tukaona mambo katika jicho moja.
Sasa imani ni hulazimisha watu waone mambo katika jicho moja.

Mbele said...

Ndugu Anonymous uliyeandika May 28, 2015 at 6:02, shukrani kwa ujumbe wako. Kwa kweli yeyote mwenye akili timamu na mwenye kuheshimu haki za binadamu ni lazima aheshimu haki na uhuru wa kila mtu kujiamulia mwenyewe kuhusu haya mambo ya dini.

Dini ni uhusiano wa mtu na Muumba wake. Ni lazima iwe hiari. Ni vizuri kuelimishana kuhusu imani za dini mbali mbali. Ni vizuri kufanya juhudi za kuwashawishi wengine watambue ubora wa dini yako, kama unaamini ni bora.

Lakini ushawishi bora zaidi ya maneno matupu ni ule wa matendo na mahusiano na wanadamu wengine. Maneno matupu, malumbano kuhusu msahafu wa nani ni bora kuliko msahafu wa nani ni mambo ambayo thamani yake ni hafifu. Maneno matupu hayavunji mfupa.

Kwa mfano, wa-Islam wakidhihirisha kwa tabia, matendo na mahusiano yao na watu wengine wa kila aina kuwa wao ni watu bora zaidi, hata mtu asiye na dini anaweza kuvutiwa kuingia katika u-Islam.

Vile vile, wa-Kristu tukidhihiridha kwa matendo, tabia na mahusiano yetu na wanadamu wa aina zote kuwa sisi ni bora kuliko wengine, kuna uwezekano mkubwa wa kuwavuta wengine waingie katika u-Kristu.

Dhamiri ya kila mtu iheshimiwe. Bila hivyo, kwa mtazamo wangu, tunakuwa tumepotoka vibaya sana.

Kizito Mpangala said...

Asante sana bwana Mbele. Mimi wakati ule nipo Seminari kwa kweli tulifundishwa mengi mno. Lakini ufundishaji wa hayo mengi tulihimizwa sana kuitumia maktaba kwa uhakika. Ndipo nilipojua kinagaubaga maana ya sisi tusemapo "tunda la katikati", kipo kitabu lilifafanua vizuri sana.

Kuhusu suala la mwalimu Emmanuel (Yesu) kila upande umempokea kadiri ya muongozo wa imani husika. Maandiko ya zamani ya Mt. Barnabas yanasema kwamba mtu aliyeandaliwa kuendeleza mahubiri baada ya Yesu ni Mtume Mohamed, hii maana yake ni kwamba upo ukubaliano wa mtu wa Mungu kwa watu fulani kadiri ya walivyomwelewa.

Jambo la msingi ni kuelekezana kwa utulivu na kufundishana vema. Hii ni kama vile ipo dini nchini India inaheshimu sana ng'ombe na inakataza kuchinjwa kwa ng'ombe. Lakini zipo zingine zimempokea Ng'ombe kama kitoweo! Tafakari