Showing posts with label Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Show all posts
Showing posts with label Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Show all posts

Sunday, November 5, 2017

Hadithi Zetu za Jadi

Hadithi zetu za jadi ni hazina kubwa ya utamaduni wetu. Kila kabila lilikuwa na hadithi nyingi, pamoja na aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo, na methali. Hadithi zina tafakari juu ya maisha na tabia za binadamu ingawa mara nyingi wahusika wana taswira za wanyama, ndege au viumbe vingine. Zinaelezea masuala ya familia, malezi ya watoto, wajibu wa wazazi na watoto. Zinatoa tahadhari kuhusu tabia mbaya na maelekezo juu tabia njema. Zinafundisha huruma, maelewano, ushiriano na kusaidiana.

Hadith zinaelezea mahangaiko, mategemeo, mafanikio, ubora na udhaifu wa binadamu, Kuna hadithi za kusisimua hisia na fikra, zenye kuibua masuali kuhusu maana ya maisha, kama walivyoibua wanafalsafa wa mkondo uitwao "existentialism," kama nilivyogusia katika kitabu cha Matengo Folktales.

Kitabu hiki ni mkusanyo wa hadithi kumi za ki-Matengo, ambazo nilizitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliandika uchambuzi wa kila hadithi na nikaandika pia insha ya jumla kuhusu hadithi, ili kuwapa wasomaji kianzio cha kuzichambua.

Nilipokuwa ninaandaa kitabu hiki, nilikuwa mhadhiri katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Somo mojawapo nililokuwa ninafundisha ni "Oral Literature" (fasihi simulizi). Hapakuwa na kitabu cha kufaa kufundishia somo hilo kwa wanafunzi wa chuo kikuu. Hapakuwa na kitabu cha kufundishia hadithi za jadi, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Kwa hivyo, lengo langu lilikuwa ni kuziba pengo, kwa kuandika kitabu ambacho nilitaka kiwepo. Hii ni falsafa ambayo imekaa kichwani mwangu: kama hakuna kitabu ambacho ungetaka kiwepo, andika hicho kitabu. Au kama kitabu unachosoma hakikuridhishi, andika hicho ambacho kitakuridhisha.

Ingawa kitabu changu si kikamilifu, angalau kinakidhi mahitaji yangu ya kufundisha somo la hadith i za jadi kwa wanafunzi wa chuo kikuu. Ni faraja kwangu kuwa si mimi peke yangu mwenye wazo hilo. Kuna wengine ambao wanakitumia kama ilivyokuwa katika chuo kikuu cha Montana na chuo cha St. Benedict/St. John's.

Wednesday, September 6, 2017

Muhula wa Masomo Unaanza

Wiki hii hapa chuoni St. Olaf, tunaanza muhula mpya wa masomo. Nitafundisha madarasa matatu. Mawili ni ya "First Year Writing," na moja ni "Post-colonial Literature." Katika "First Year Writing," tunafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza.

Kozi ninayotaka kuongelea hapa  ni "Post-colonial Literature." Niliajiriwa hapa chuoni St. Olaf kuanzisha kozi hiyo, na nilianza kufundisha mwaka 1991. Ni kozi inayohusu fasihi kutoka nchi zilizokuwa katika himaya ya u-Ingereza wakati wa ukoloni ila zilikuja kuwa huru.

Ninapofundisha kozi hii, huwa ninaamua waandishi wepi kutoka nchi zipi nifundishe. Kwa muhula huu, niliamua kufundisha fasihi kutoka Afrika Kusini. Nilichagua waandishi wawili: Alex la Guma na Nadine Gordimer. Wote ni waandishi wa hadithi fupi na riwaya.

Nadhani tangu nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, nilisoma hadithi za Alex la Guma katika kitabu cha hadithi fupi kiitwacho Quartet. Baadaye, nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya Literature, chuo kikuu cha Dar es Salaam, Alex la Guma alikuja kutoka London akatufundisha kwa siku kadhaa. Alialikwa na mkuu wa idara, mwalimu Grant Kamenju wa Kenya.

Nilifahamu kuwa Alex la Guma alikuja kuwa mwakilishi Uingereza wa chama cha ukombozi cha African National Congress cha Afrika Kusini, (ANC), kisha akawa mwakilishi wa ANC nchini Cuba. Alipofariki, nchini Cuba, nilikuwa ninasoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin Madison.

Nadine Gordimer ni mzungu aliyejihusisha na ANC. Alikuwa mpinzani wa utawala wa makaburu. Baada ya kuja Marekani kufundisha, nimebahatika kumwona Nadine Gordimer kwenye mkutano fulani wa kitaaluma. Sikumbuki ulikuwa ni mwaka gani. Nimefundisha hadithi zake fupi zilizokusanywa katika kitabu Six Feet of the Country, na riwaya zake, The Conservationist, The Pickup, na July's People.

Kufundisha juu ya waandishi hao wawili ni fursa ya kutafakari historia na siasa, hasa ukaburu na harakati za ukombozi katika Afrika Kusini. Yote hayo yamefungamana na fasihi, hasa katika karne ya ishirini, ambayo ndiyo kozi yangu itashughulikia. Tutafakari mitazamo ya waandishi hao wawili kuhusu siasa, mahusiano ya jamii, utamaduni, na itikadi katika Afrika Kusini. Tutaangalia athari za fasihi ya ulimwengu katika maandishi ya waandishi hao wawili na tutatambua mchango wa waandishi hao katika fasihi ya Afrika na ulimwengu.

Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

Thursday, November 24, 2016

"A Far Cry From Africa," Shairi la Derek Walcott

Tangu nilipoanza kufundisha katika chuo cha St. Olaf, mwaka 1991, nimepata fursa ya kusoma na kufundisha fasihi iliyoandikwa kwa ki-Ingereza kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni, kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyowezekana nilipokuwa ninafundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwandishi mmojawapo ambaye kazi zake nimezishughulikia sana ni Derek Walcott wa St. Lucia, pande za Caribbean, maarufu kwa utunzi wa mashairi na tamthilia, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1992.

Nimesoma na kufundisha mashairi yake mengi na tamthilia zake kadhaa. Moja ya mashairi hayo ni "A Far Cry From Africa," ambalo lilichapishwa mwaka 1962. Linaelezea mahuzuniko juu ya vita ya Mau Mau nchini Kenya iliyodumu kuanzia mwaka 1952 hadi 1960. Masetla wazungu walipigana na wa-Afrika waliotaka kuchukua ardhi yao iliyoporwa. Kwa kuwa Derek Walcott ni chotara, damu ya kizungu na ki-Afrika, alihisi vita hiyo ikitokea ndani ya nafsi yake. Uhasama na ukatili wa pande hizo mbili aliuhisi mithili ya sumu katika mishipa ya damu yake. Alijihisi kama mateka aliyekosa namna ya kujinasua.

Walcott anaimudu lugha ya ki-Ingereza kwa namna inayonikumbusha umahiri wa Shakespeare. Nitafurahi iwapo nitapata ujasiri wa kujaribu kulitafsiri shairi kwa ki-Swahili.
-------------------------------------------------------------------------------

A Far Cry From Africa

Derek Walcott


A wind is ruffling the tawny pelt 
Of Africa, Kikuyu, quick as flies, 
Batten upon the bloodstreams of the veldt. 
Corpses are scattered through a paradise. 
Only the worm, colonel of carrion, cries: 
'Waste no compassion on these separate dead!' 
Statistics justify and scholars seize 
The salients of colonial policy. 
What is that to the white child hacked in bed? 
To savages, expendable as Jews?

Threshed out by beaters, the long rushes break 
In a white dust of ibises whose cries 
Have wheeled since civilizations dawn 
From the parched river or beast-teeming plain. 
The violence of beast on beast is read 
As natural law, but upright man 
Seeks his divinity by inflicting pain. 
Delirious as these worried beasts, his wars 
Dance to the tightened carcass of a drum, 
While he calls courage still that native dread 
Of the white peace contracted by the dead. 

Again brutish necessity wipes its hands 
Upon the napkin of a dirty cause, again 
A waste of our compassion, as with Spain, 
The gorilla wrestles with the superman. 
I who am poisoned with the blood of both, 
Where shall I turn, divided to the vein? 
I who have cursed 
The drunken officer of British rule, how choose 
Between this Africa and the English tongue I love? 
Betray them both, or give back what they give? 
How can I face such slaughter and be cool? 
How can I turn from Africa and live?

Monday, October 10, 2016

Ki-Ingereza Kama Lugha ya Ulimwengu

Jana, katika blogu hii, nilikiongelea kitabu cha Charles Derber, People Before Profit, ambacho kinahusu utandawazi. Katika kukisoma kitabu hiki, nilivutiwa na maelezo yake, na nikapata hamasa ya kufuatilia mada ya utandawazi kwa namna nyingine.

Nilikumbuka kwamba nina kitabu cha David Crystal, English as a Global Language, ambacho nilikinunua miaks michache iliyopita, ila nilikuwa nimekipitia juu juu tu. Leo nimeamua kukisoma, na ninaona jinsi maelezo yake kuhusu lugha ya ki-Ingereza yanavyofungamana na suala la utandawazi. Kwa mfano, katika utangulizi wake, mwandishi anasema,

"We have as yet no adequate typology of the remarkable range of language contact situations which have emerged as a consequence of globalization, either physically (e.g. through population movement and economic development or virtually (e.g. through Internet communication and satellite broadcasting)." (xi)

Kitu kimoja kilichonifanya nikumbuke kitabu cha David Crystal ni kuwa huyu ni mtaalam maarufu ulimwenguni wa masuala ya lugha. Nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikisomea "Literature" na "English," ndipo niliposoma maandishi ya Crystal, sambamba na mabingwa wengine, kama vile Frank R. Palmer, John Lyons, Noam Chomsky, Sydney Greenbaum, na Randolph Quirk. Kumbukumbu hiyo ndiyo ilinifanya ninunue kitabu cha Crystal, English as a Global Language miaka michache iliyopita. Sasa, kwa kuwa ninafuatilia suala la utandawazi, ninaona nilifanya vizuri kununua kitabu hiki.

Pamoja na kuelezea jinsi ki-Ingereza kilivyofanikiwa kuenea duniani na kinavyoendelea kuiteka dunia kama lugha ya mawasiliano ulimwenguni iliyo muhimu kuliko zote, Crystal anabainisha pia kuwa hatuwezi kuwa na uhakika kama hali hii itaendelea hivi siku za usoni. Kama nilivyoeleza katika ujumbe wa jana, nikinukuu kitabu cha People Before Profit, utandawazi hausambai bila upinzani kutoka katika jamii na tamaduni mbali mbali zinazotaka kulinda jadi na misingi yao.

Ni hivi hivi katika kuenea kwa ki-Ingereza. Crystal anatuelekeza kwenye kitabu cha Tom McArthur, The English Language, na anatumabia kuwa McArthur

"adopted a more synchronic perspective, moving away from a monolithic concept of English. His primary focus was on the kinds of variation encountered in the language as a consequence of its global spread. He suggested that English was undergoing a process of radical change which would eventually lead to fragmentation into a 'family of languages.'" (x)

Hilo wazo la ki-Ingereza kugawanyika katika vilugha mbali mbali linasisimua akili. Lakini, hata kama ki-Ingereza kitaishia kuwa vilugha vingi, ninategemea kuwa bado kutakuwa na misingi itakayodumu katika vi-Ingereza hivyo na kuendelea kuwawezesha watumiaji kuwasiliana na kuelewana. Hata wakati huu, tayari ki-Ingereza kina lahaja nyingi, sawa na ki-Arabu, ki-China, ki-Swahili, na lugha zingine.

Jambo la muhimu la kuzingatia, kwa nchi kama Tanzania, ni hoja ya msingi ya English as a Global Language, kwamba hakuna namna ya kukizuia ki-Ingereza kutawala dunia kama lugha ya mawasiliano. Tupende tusipende, lazima tutafute namna ya kuhakikisha kuwa tunaijua lugha hiyo. Tusipumbazwe na siasa reja reja zilizovaa gwanda la utaifa, tukasahau kwamba ki-Ingereza ndiyo nyenzo na silaha itakiwayo katika mapambano ya ulimwengu wa utandawazi wa leo na kesho.

Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

Thursday, October 8, 2015

Wanafunzi Wangu wa Ki-Ingereza

Ni yapata mwezi sasa tangu tuanze muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Ninafundisha kozi mbili, South Asian Literature na "First Year Writing." Hii ya kwanza ni kozi ya fasihi ya ki-Ingereza kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Ya pili ni kozi ya uandishi wa ki-Ingereza. Picha hii kushoto, ya darasa la ki-Ingereza (FYW), tulipiga leo. Mwanafunzi mmoja hayumo. Niliweka picha ya darasa kama hili katika blogu hii.

Nilipenda ualimu tangu utotoni. Ninawapenda wanafunzi. Ninawaambia hivyo tangu siku ya kwanza ya masomo, nao wanashuhudia hivyo siku zote. Wanajionea ninavyojituma kuwaelimisha kwa uwezo wangu wote na kwa moyo moja. Sina ubaguzi, dhulma, wala upendeleo. Hiyo imekuwa tabia yangu tangu nilipoanza kufundisha, mwaka 1976, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ninajivunia jambo hilo.

Kwa miezi mingi, hasa mwaka jana, afya yangu haikuwa njema, na nilichukua likizo ya matibabu. Ingawa nimeanza tena kufundisha, inatokea mara moja moja kwamba sijisikii vizuri. Juzi ilitokea hivyo, ikabidi niwaambie wanafunzi hao waendelee kuandika insha niliyowaagiza kabla, nikawaaga.

Jana, nilipofika ofisini, nilikuta kadi mlangoni pangu, ambayo picha yake inaonekana hapa kushoto. Wanafunzi hao walikuwa wameniandikia hiyo kadi na ndani walikuwa wamesaini majina yao. Maneno yanayoonekana pichani yanatokana na michapo yangu darasani. Nilivyoipata kadi hii, niliguswa. Nimewaambia hivyo leo, tulipoanza kipindi.

Ualimu si kazi rahisi. Inahusu taaluma. Inahusu malezi. Inahusu kuwashauri na kuwasaidia wanafunzi katika hali mbali mbali za maisha. Lakini, hayo ndiyo mambo yanayonivutia katika ualimu. Mafanikio ya wanafunzi masomoni na maishani ndio mafanikio na furaha yangu.

Saturday, May 23, 2015

Leo Nimenunua Kitabu: "Jesus: Prophet of Islam"

Leo nilikwenda Minneapolis kwenye mkutano mdogo wa watu wanne ambao tulifanyia katika jengo la maduka na biashara mbali mbali liitwalo Somali Mall. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jingo hili. Nilipata fursa ya kuingia katika duka la vitabu liitwalo Akmal Bookstore, ambalo limejaa vitabu vya ki-Islam katika ki-Arabu na ki-Somali.

Niliuliza iwapo kuna vitabu vya ki-Ingereza, nikaonyeshwa. Niliviona vingi vilivyonivutia, nikanunua kimoja, Jesus: Prophet of Islam, kilichoandikwa na Muhammad 'Ata' ur-Rahim na Ahmad Thomson.

Nimefahamu kwa miaka mingi kuwa katika u-Islam, Yesu anatambulika kama mtume maarufu, ila sio mwana wa Mungu, kama tunavyomwona sisi wa-Kristu. Sioni tatizo, wala sikosi usingizi kwa sababu hiyo. Ninachozingatia ni waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kila mtu na imani yake. Tukumbuke kwamba dini zinatofautiana, na kuna dini ambazo hamzimjui Yesu kabisa, iwe ni kama mtume au mwana wa Mungu.

Mara yangu ya kwanza kuelewa namna wa-Islam wanavyomwona Yesu ni wakati nilipokuwa nafundisha somo la "Epic" kwa wanafunzi wa uzamili (M.A.) katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1986-88. Kati ya maandishi ya kitaaluma niliyoyaongelea darasani ni insha maarufu ya Alan Dundes, "The Hero Pattern and the Life of Jesus."

Ulipofika muda wa kuandaa tasnifu, mwanafunzi mojawapo, Hamza Njozi, aliniambia kuwa angepnda kuandika kuhusu masimulizi juu ya Yesu (Issa) katika Qur'an. Niliona ni mada murua. Alifanya utafiti na uchambuzi mzuri akamaliza tasnifu yake. Katika kumwelekeza kwa miezi yote ya utafiti na uandishi wa tasnifu, nami niliweza kufahamu msimamo wa Qur'an juu ya Yesu (Issa).

Hii leo, nilipokiona kitabu cha Jesus: Prophet of Islam, nilikumbuka yote hayo, nikakinunua bila kusita. Nangojea kwa hamu kukisoma.

Saturday, February 21, 2015

Lugha na Mwamko wa Elimu Tanzania

Katika kuendelea kutekeleza ombi nililopata kutoka kwa mdau wa blogu hii, juu ya sera ya lugha ya kufundishia nchini Tanzania, napenda kuongelea suala la lugha na mwamko wa elimu. Huu ni mwendelezo wa ujumbe nilioandika katika makala yangu, "Tatizo si Lugha ya Kufundishia, ni Uzembe." ambayo niliichapisha katika blogu hii.

Kwanza, nasisitiza mtazamo wangu kuwa tatizo si lugha ya kufundishia, bali uzembe.

Mimi kama mwelimishaji, nimeshuhudia tatizo hili lilivyo katika jamii ya wa-Tanzania. Nitaanza kwa kutoa mfano. Mwaka 1980, nilipokuwa mhadhiri katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilifika kusomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani.

Niliondoka Tanzania wakati jamii ikiwa bado inazingatia mafundisho ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa miaka sita niliyokuwa masomoni, nilifanya bidii katika masomo na pia nilinunua vitabu vingi sana, nikijua kuwa ndio nyenzo itakayonifanya nifundishe kwa kiwango cha juu kabisa pindi nitakaporejea tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nilipohitimu masomo, nilirejea nchini nikiwa na shehena yangu ya vitabu. Badala ya kuniulizia kuhusu masomo niliyosomea au elimu niliyoipata, watu waliniuliza kama nimeleta "pick-up." Walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari. Haikutegemewa kuwa mtu ukae "majuu" miaka yote ile halafu usirudi na gari.

Hapo nilitambua wazi kabisa kuwa mwamko wa elimu, ambao alikuwa ameuchochea Mwalimu Nyerere, ulikuwa umedidimia. Niliendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku nikishuhudia mwamko wa elimu ukiendelea kudidimia nchini.

Jadi ya kuthamini mali na vitu badala ya elimu iliendelea kushamiri. Wasomi wakipata fursa ya kwenda nje, inayojulikana kama "sabbatical," walitegemea na walitegemewa kutumia fursa hiyo kujitafutia vitu, hasa magari. Mwenye kuleta gari au magari alionekana ndiye msomi bora. Ni tofauti kabisa na hapa Marekani, ambapo profesa unathaminiwa kwa ujuzi wako, hata kama unatembelea baiskeli au unapekua kwa miguu. Binafsi, kwa kuwa kipaumbele changu elimu na taaluma nimeridhika kufundisha hapa Marekani, tangu nilipoanza, mwaka 1991.

Tanzania, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa walimu kushughulikia shughuli zao za kujipatia pesa hata kama walipaswa wawe darasani wakifundisha. Jambo hili limekuwa likitajwa na wanafunzi wetu wa ki-Marekani tunaowapeleka kusoma Tanzania, kwani katika vyuo vyao hapa Marekani, profesa hawezi kukosa kuingia darasani bila sababu ya maana kama vile kuumwa. Na akikosa kipindi, hufanya mpango wa kukifidia.

Katika jamii ya wa-Tanzania, nilishuhudia kushamiri utamaduni wa kutafuta vyeti kwa njia yoyote, badala ya kutafuta elimu. Nilishuhudia jinsi watu walivyokuwa tayari kutafuta hata vyeti feki. Hata baadhi ya wale wanaoitwa viongozi wamejipatia hivyo vyeti feki, kutoka  vyuo ambavyo havina hadhi itambulikanayo katika ulimwengu wa taaluma.

Kama ambavyo nimekuwa nikilalamika tena na tena katika blogu hii, utamaduni wa kununua na kusoma vitabu umekosekana katika jamii ya wa-Tanzania. Wazazi, ambao wangetegemewa kuwa wanunuaji wa kuaminika wa vitabu na wawe wanawasomea vitabu watoto wao, kama wafanyavyo wa-Marekani, hawafanyi hivyo.

Hao tunaowaita viongozi Tanzania, na wa-Tanzania wengine wengi, hutembelea nchi za nje. Sijui ni wangapi wanatumia fursa hii kununua vitabu na kurudi navyo Tanzania. Katika miji wanayopita na katika viwanja vya ndege, kuna maduka ya vitabu. Sijui ni wangapi wanapita katika maduka hayo na kununua vitabu. Nimewahi kusafiri mara kwa mara na wa-Tanzania, na nimeona kuwa zawadi wanazonunua ni vitu kama vipodozi, marashi, na mizinga ya vinywaji vikali. Wa-Tanzania hupenda zawadi za aina hiyo. Vitabu je? Jibu mwenyewe.

Sijui ni nyumba zipi katika Tanzania ambazo zina maktaba. Sijui ni nyumba ngapi ambazo zina vitabu angalau 50 au 100, kwa ajili ya watoto na wazazi. Kutegemea kuwa utamwona m-Tanzania amekaa sebuleni, bustanini, ufukweni, ndani ya basi au ndege, anasoma kitabu, ni kama kutegemea kumwona jogoo amevaa suruali.

Niliwahi kuhudhuria tamasha la vitabu Dar es Salaam, mwaka 2004. Watoto walikuwepo, na waalimu, lakini watu wazima walikuwa wachache sana. Hata hao wanaoitwa viongozi, wa ngazi yoyote, hawakuwepo. Watoto walifanya maonesho mbali mbali na waliimba nyimbo. Katika wimbo mmojawapo, waliwasihi wazazi wawe wananunua vitabu na kusoma pamoja na watoto wao majumbani. Wazazi wenyewe hawakuwepo kwenye tamasha. Lakini jioni, nilipokuwa naelekea nyumbani, niliwaona hao watu wazima wamekusanyika kwenye mabaa.

Katika hali hii, tatizo linalohitaji kushughulikiwa ni mwamko wa elimu. Bila mwamko wa elimu, hata lugha ya kufundishia ikibadilishwa mara ngapi, hata tukisema tutumie lugha zetu za ki-Nyaturu, ki-Nyasa, ki-Zaramo, na kadhalika, tusitegemee kuwa tutaleta mapinduzi yatakiwayo. Kinachohitajika ni mwamko wa elimu. Huu ndio msingi, ambao tumeuharibu.

Wednesday, May 8, 2013

Nimekutana na Mjukuu wa Mahatma Gandhi

Jioni hii tumepata bahati ya kuwa na Ela Gandhi, mjukuu wa Mahatma Gandhi. Alikuja kutoa mhadhara chuoni Carleton hapa mjini petu. Mada ya mhadhara wake ilikuwa, "The Challenges Facing Post-Apartheid South Africa."

Mama Ela Gandhi, ambaye alizaliwa Durban, ni mwanaharakati wa masuala ya amani na maendeleo. Aliongelea historia ya Mahatma Gandhi na mafundisho yake kuhusu namna ya kukabiliana na matatizo ya hujuma dhidi ya haki. Alisisitiza kuwa njia aliyofundisha Gandhi ya kutotumia mabavu na vita inatujengea mtandao wa urafiki na kuheshimiana, tofauti na vita, ambayo matunda yake ni kujenga mtandao wa maadui.

Alielezea umuhimu wa mafundisho ya watu kama Mahatma Gandhi, Albert Lutuli, Martin Luther King, na Nelson Mandela. Kisha alielezea changamoto zinazoikabili Afrika Kusini leo, kwani mategemeo ya wengi wakati wa kupambana na mfumo wa ukaburu hayajapatiwa ufumbuzi.

Nilikwenda kwenye mhadhara huu na baadhi ya wanafunzi wangu, ambao muhula huu tunasoma fasihi ya Afrika Kusini. Tumefurahi kumsikia Mama Ela Gandhi akiongelea masuala ambayo tumekuwa tukiyajadili darasani. Kwa mfano, katika kipindi cha leo, wakati tunasoma hadithi ya Nadine Gordimer iitwayo "A Chip of Glass Ruby" katika kuelezea dhamira mbali mbali zilizomo, nilikuwa nimewaelezea dhana ya  "Group Areas" inayotajwa katika hadithi hiyo. Kwa bahati nzuri, Mama Ela Gandhi katika mhadhara wake alifafanua dhana hiyo ya "Group Areas" vizuri kabisa.

Baada ya mhadhara wake, watu tulipata fursa ya kupiga naye picha. Nilipomwambia kuwa mimi ni m-Tanzania, alifurahi akakumbushia historia njema ya mahusiano baina ya nchi yake na Tanzania, akataja kazi nzuri iliyofanywa na Julius Nyerere. Nami niliongelea jinsi tulivyopata bahati Tanzania ya kujumuika na wakimbizi kutoka Afrika Kusini, baadhi wakiwa wahadhiri wetu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na wengine wakiwa viongozi wa vyama vya ukombozi ambao walifika kutoa hotuba. Kwa mfano, niliwataja Albie Sachs na Gora Ebrahim.

Monday, March 25, 2013

Toleo Jipya la "Kioo cha Lugha"

Siku chache ziilizopita, nilipata nakala ya jarida la Kioo cha Lugha, kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mimi ni mwanakamati katika kamati ya uhariri wa jarida hilo. Ni furaha kubwa kwangu kushirikiana na wanataaluma wenzangu katika mambo ninayoyapenda. Masuala ya la lugha, fasihi, utamaduni, na falsafa yana nafasi ya pekee katika maisha yangu.















Toleo hili la Kioo cha Lugha lina makala nyingi, kama inavyoonesha katika picha hii hapa kushoto. Wanaodhani kuwa ki-Swahili kina mapungufu katika kuelezea taaluma mbali mbali, watafakari upya suala hilo, hasa kwa kusoma machapisho kama yale yatokayo katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, ambayo ni ya taaluma mbali mbali. Niliwahi kugusia suala hilo katika ujumbe huu hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...