Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

1 comment:

Emmanuel Kachele said...

Niwe muwazi tu juu ya nchi yangu na nchi nyingine za kiafrika. Kwanza, wasomi wake hatutumii usomi wetu. Badala yake tunasubiri tuongozwe na watu wenye utashi wa kisiasa huku tukiweka weledi wetu pembeni.
Kutokutumia Elimu huku au kutopata Elimu sahihi ndio kutengeneza mazalia na makazi ya kudumu ya madikteta. Hatuwezi kusema ukweli, ila tunajua sana kushabikia uongo. Hatuwezi hata kujivunia juu ya lolote ila siasa ndio imetawala.
Wito kwa kila msomi, ukiwemo wewe Profesa, ni kutuandaa vijana, ili baadae tube tufute mazalia ya madikteta hata kama sio sisi basi vizazi vijavyo.
Umuhimu wa watu kama nyie ni kutupa Elimu kama hivi. Tupeni ujuzi, vitabu na kadhalika ili hata mkiwa hampo duniani mbaki mmetuambukiza vitu muhimu katika kizazi hili na vijavyo.

Asante sana Profesa.