Showing posts with label Ukoloni mamboleo. Show all posts
Showing posts with label Ukoloni mamboleo. Show all posts

Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

Tuesday, December 9, 2014

Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo

Siku hii ya leo, ambayo ni ya kumbukumbu ya siku ambapo Tanganyika ilijipatia Uhuru, nilitaka kuandika makala, "Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo." Nilianzza kuandika, lakini nilijikuta naandika insha ndefu, sio makala fupi ambayo nadhani inatakiwa katika blogu. Kutokana na jambo hilo, nimeifuta ile makala na badala yake nimeandika kwa ufupi mambo yafuatavyo.

Uhuru tulipata tarehe 9 Desemba, 1961. Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, na ninakumbuka msisimko, hata kule kijijini kwangu. Waalimu wetu, Charles Kinunda, John Pantaleon Mbonde, na Alois Turuka, walikuwa chanzo kikubwa cha ufahamu wetu wa mambo yaliyokuwa yanatokea.

Kati ya kumbukumbu ambazo haziwezi kutoweka akilini mwangu ni picha ya askari Alexander Nyirenda akiweka mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Sambamba na tukio hili la kihistoria ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, ambamo alisema:

Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.

Mwalimu Nyerere, alifanya kila juhudi kuliongoza na kulielimisha hili Taifa huru, akisema kuwa tunaingia katika mapambano na maadui watatu: ujinga, umaskini na maradhi. Miaka ilivyopita, alifafanua vizuri malengo mengine ya Taifa hili: kujenga jamii ya usawa kwa wote, isiyo na matabaka; jamii yenye kutoa fursa sawa kwa wote, katika nyanja mbali mbali, kama vile uchumi, elimu, na afya; kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wa kufanya kazi, chini ya kauli mbiu ya "Uhuru na Kazi," kujenga Taifa linalojitambua, kujiheshimu, na kujitegemea, Taifa huru lisilofungamana na upande wowote katika mazingira yale ya "Cold War," Taifa lenye kukaribisha urafiki na nchi yoyote kwa msingi wa kuheshimiana, Taifa ambalo halitamruhusu rafiki kutuchanguia marafiki au maadui, na tuwe mstari wa mbele kuunga mkono harakati za ukombozi Afrika na sehemu zingine duniani.

Hayo ndio yalikuwa malengo muhimu, ambayo Mwalimu Nyerere aliyaelezea katika hotuba zake, makala na vitabu mbali mbali. Alikuwa akienda na wakati, akizingatia mahitaji ya Taifa yalivyokuwa yanajitokeza. Kwa msingi huu, baada ya "Azimio la Arusha," aliendelea kuandika maandishi mengine, kama vile "Mwongozo," "Siasa ni Kilimo," "Elimu ya Kujitegemea," na "Binadamu na Maendeleo."

Hayo yote, tangu enzi za harakati za Uhuru hadi miaka ya mwisho mwisho ya sabini na kitu, yalifanyika chini ya uongozi wa chama cha TANU. Mtazamo na mwelekeo wa TANU ulikuwa wa kuongoza mapinduzi, kufuatana na mazingira ya kihistoria: kwanza ilikuwa kuwaunganisha wa-Tanganyika na kuwaongoza katika kupigania Uhuru, halafu, kuongoza harakati za kujenga ujamaa na kujitegemea.

Mwalimu Nyerere alifahamu fika kwamba Uhuru haukuwa mwisho wa safari. Kulikuwa na haja ya kupambana na urithi wa ukoloni, yaani ukoloni mamboleo na kuleta uhuru wa kweli, unaodhihirishwa na hali ya kujitegemea chini ya uongozi bora.

Miaka ilivyopita, baada ya chama kipya cha CCM kushika hatamu, hali ilikuwa hiyo kwa kipindi cha mwanzo. Lakini, pole pole, mwelekeo huu wa kuwa daima katika harakati za mapinduzi, ulianza kubadilika. Chini ya sera za CCM, kama vile "Azimio la Zanzibar," nchi imeendelea kuzama zaidi na zaidi katika mfumo wa matabaka na ukoloni mamboleo. Kwa lugha rahisi, CCM ni mhujumu wa Mapinduzi.

Ndoto na mategemeo ya Uhuru yametekwa nyara. Pamoja na kwamba tunasherehekea Uhuru tuliojipatia mwaka 1961, tutambue, kama TANU ilivyotambua, kuwa ule haukuwa mwisho wa safari. Enzi za TANU, tulitegemea kuwa tutajenga nchi ambayo iko chini ya mamlaka ya wakulima na wafanyakazi. Lakini, kama nilivyosema hapa juu, tunazidi kuzama katika ukoloni mamboleo. Wakulima na wafanyakazi, pamoja na washiriki wao, bado wana jukumu la kuendeleza harakati za kutafuta Uhuru wa kweli.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...