
Uhuru tulipata tarehe 9 Desemba, 1961. Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, na ninakumbuka msisimko, hata kule kijijini kwangu. Waalimu wetu, Charles Kinunda, John Pantaleon Mbonde, na Alois Turuka, walikuwa chanzo kikubwa cha ufahamu wetu wa mambo yaliyokuwa yanatokea.
Kati ya kumbukumbu ambazo haziwezi kutoweka akilini mwangu ni picha ya askari Alexander Nyirenda akiweka mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Sambamba na tukio hili la kihistoria ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, ambamo alisema:
Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.


Hayo yote, tangu enzi za harakati za Uhuru hadi miaka ya mwisho mwisho ya sabini na kitu, yalifanyika chini ya uongozi wa chama cha TANU. Mtazamo na mwelekeo wa TANU ulikuwa wa kuongoza mapinduzi, kufuatana na mazingira ya kihistoria: kwanza ilikuwa kuwaunganisha wa-Tanganyika na kuwaongoza katika kupigania Uhuru, halafu, kuongoza harakati za kujenga ujamaa na kujitegemea.
Mwalimu Nyerere alifahamu fika kwamba Uhuru haukuwa mwisho wa safari. Kulikuwa na haja ya kupambana na urithi wa ukoloni, yaani ukoloni mamboleo na kuleta uhuru wa kweli, unaodhihirishwa na hali ya kujitegemea chini ya uongozi bora.
Miaka ilivyopita, baada ya chama kipya cha CCM kushika hatamu, hali ilikuwa hiyo kwa kipindi cha mwanzo. Lakini, pole pole, mwelekeo huu wa kuwa daima katika harakati za mapinduzi, ulianza kubadilika. Chini ya sera za CCM, kama vile "Azimio la Zanzibar," nchi imeendelea kuzama zaidi na zaidi katika mfumo wa matabaka na ukoloni mamboleo. Kwa lugha rahisi, CCM ni mhujumu wa Mapinduzi.
Ndoto na mategemeo ya Uhuru yametekwa nyara. Pamoja na kwamba tunasherehekea Uhuru tuliojipatia mwaka 1961, tutambue, kama TANU ilivyotambua, kuwa ule haukuwa mwisho wa safari. Enzi za TANU, tulitegemea kuwa tutajenga nchi ambayo iko chini ya mamlaka ya wakulima na wafanyakazi. Lakini, kama nilivyosema hapa juu, tunazidi kuzama katika ukoloni mamboleo. Wakulima na wafanyakazi, pamoja na washiriki wao, bado wana jukumu la kuendeleza harakati za kutafuta Uhuru wa kweli.
2 comments:
Very well said ndugu Joseph Mbele. Katu asilani hujakosea kabisa. Nimeona ulivyojitahidi kuyaelezea kwa ustadi mkubwa, na kwa muhtasari (succinctly), maono ya Mwalimu Nyerere bila kupoteza uzito wake hata kidogo, kitu ambacho huwashinda waandishi wetu wengi.
Hata hivyo, binafsi nimependa zaidi ulivyolihitimisha andiko lako kwa kusema " Wakulima na wafanyakazi, pamoja na washiriki wao, bado wana jukumu la kuendeleza harakati za kuutafuta Uhuru wa kweli." Ninakubaliana na hiyo dhana kwa asimilia mia. Hii ni kwa vile ninatambua na kuona dhahiri kabisa kuwa, kwetu sisi Watanzania, kwa sasa hivi huo Uhuru tuliousherekea wiki hii hatunao. Tulionao ni 'Uhuru wa bandia.' Kwa maneno mengine, tumebadili rangi yetu ya wakoloni; kutoka katika makucha ya wakoloni weupe, kwenda kwenye makucha ya wakoloni weusi!
Ama kwa hakika, ni jukumu letu sasa kuanza tena harakati za kujikomboa kutoka katika aina hii ya ukoloni pia. Asante sana Mwalimu, nimelipenda sana hili andiko lako.
Ndugu Dennis Dotto,
Nakushukuru kwa kutembelea hiki kiblogu changu, kusoma hii makala yangu, na kuweka maoni yako.
Kama nilivyosema, nawe umeliona hilo, nimeandika kwa kifupi. Nina mengi ya kusema kuhusu suala hili, kiasi kwamba ningeweza kuandika kitabu.
Nakutakia kila la heri
kwa msimu huu wa Krismasi, Mwaka Mpya, na daima.
Post a Comment